Jumanne, 11 Julai 2023

TUMIENI NAFASI MNAZOPATA KUTOA ELIMU KUHUSU ARDHI: JAJI NGWEMBE

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe awasihi Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi mkoani hapa kutumia fulsa wanazopata kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu umiliki wa ardhi. 

Mhe. Ngwembe ametoa wito huo wakati wa kikao cha kusukuma mashauri ya jinai na madai kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mikutano kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro. Alisema takwimu zinaonesha asilimia 70 ya mashauri yaliyokatiwa rufaa kwenda Mahakama Kuu yanahusu migogoro ya ardhi.

“Mkoa huu wa Morogoro una kesi nyingi zinazohusu migogoro ya ardhi, nafikiri mingi inachangiwa na wananchi kutokuwa na uelewa wa sheria zinazohusu umiliki wa ardhi na wakati mwingine baadhi ya wananchi kuwa na tamaa ya kujipatia ardhi kwa njia ya udanganyifu, tumieni majukwaa yenu kuwaelimisha wananchi hawa,” alieleza. 

Aliongeza kuwa Mahakama Kanda ya Morogoro haitorudi nyuma katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na hadi sasa wanaendelea kusikiliza mashauri kwa njia ya teknolojia na tayari mifumo ya kutumia imefungwa katika Magereza mawili ya Morogoro mjini na utaratibu unafanyika kuyaunganisha yale yaliyopo wilayani. 

Akizungumza katika jukwaa hilo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messe Chaba aliwapongeza Mahakimu Wafawidhi ambao wamekuwa wakisaidia kupatikana kwa nakala halisi za kesi zilizokatiwa rufaa, hivyo kurahisisha usikilizaji wa mashauri ndani ya muda mfupi. 

Alisema kuwa ushirikiano baina ya Mahakama na wadau ni muhimu kwa wote na wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kupigania haki za wananchi na kuwa huru kutoa mawazo yao. 

Nao Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi walichangia namna wanavyokumbana na mashauri ya migogoro ya ardhi na kueleza jitihada wanazotumia katika kutatua changamoto hiyo, huku wakiahidi kushirikiana na Mahakama katika kutatua migogoro ya ardhi ili wamiliki halali wapatiwe haki zao. 

Awali, wakati akisoma taarifa fupi ya hali ya mashauri, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando alisema kuwa hadi kufikia Juni 22, 2023, Mahakama Kuu Kanda kwa upande wa mashauri ya jinai haikuwa na shauri la mrundikano. 

Alieleza kuwa kuanzia Januari hadi Juni 22, 2023, mashauri ya jinai yaliyofunguliwa yalikuwa 113, yaliyoamuliwa ni 131 na yanayoendelea ni 89, huku kwa upande wa madai kuanzia kipindi cha Aprili 1, 2023 hadi Juni 22, 2023 yalifunguliwa mashauri 130, yalimalizika mashauri 141 na yanayoendelea yapo 307, idadi ambayo inajumlisha mashauri 281 yaliyobaki ndani ya kipindi cha Disemba 2022. 

Kikao hicho kilichohudhuliwa na wajumbe mbalimbali kutoka taasisi ambazo ni wadau wa Mahakama kilijadili masuala mbalimbali, ikiwemo namna ambavyo Mahakama Kanda ya Morogoro ilivyoboresha katika utoaji huduma na hasa elimu ya msingi ya sheria kwa wananchi ambayo imesaidia kupunguza idadi kubwa ya makosa yaliyokuwa yakijirudia kipindi cha mwaka 2021/2022.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe akizungumza wakati wa kikao vya kusukuma mashauri.

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Messeka Chaba akifuatilia taarifa ya kikao cha kusukuma mashauri.

 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mmbando akisoma taarifa fupi kuhusu mwenendo wa mashauri wakati wa kikao hicho.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana akifuatilia kikao cha kusukuma mashauri.

 

Wajumbe wa kikao cha kusukuma mashauri (juu na chini) wakifuatilia.

 

( Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama).

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni