Jumanne, 11 Julai 2023

KIWANGO CHA WANANCHI KURIDHISHWA NA HUDUMA ZA MAHAKAMA CHAPAA

Na Faustine Kapama – Mahakama.

Kiwango cha kuridhika kwa watumiaji wa huduma zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali ya utoaji haki nchini kimepanda kwa asilimia 10 kutoka asilimia 78 kwa mwaka 2019 hadi asilimia 88 kwa mwaka 2023.

Hayo yamebainika leo tarehe 11 Julai, 2023 baada ya Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Jamii na Uchumi (REPOA) kuwasilisha mahakamani taarifa ya utafiti wao walioufanya kuhusu kuridhika kwa watumiaji wa huduma za Mahakama kwa mwaka 2023.

Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dkt. Donald Mmari na Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo, Dkt. Lucas Katera wamekabidhi taarifa ya utafiti huo kwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma kwenye hafla fupi iliyofanyika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania, akiwemo Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Silvester Kainda, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, Watendaji pacha wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha na Bi Mary Shirima na wajumbe wengine wa menejimenti ya Mahakama.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mhe. Chuma amesema kuwa kupanda kwa kiwango cha kuridhika kwa watumiaji wa huduma za Mahakama kuhusu huduma zitolewazo na Mahakama ni zao la maboresho makubwa yanayofanywa na Mahakama katika maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na wadau.

“Kiwango hiki kinadhihirisha kuongezeka kwa uwajibikaji, uweledi na uwazi. Upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati kwa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kupitia mfumo wa taarifa za sheria na maamuzi wa Mahakama ya Tanzania (TanzLII),” amesema.

Msajili Mkuu amebainisha kuwa Mahakama ya Tanzania inaendeshwa na dira yake ya utoaji haki sawa kwa wote na kwa wakati na ili kufikia dira hiyo imekuwa ikiendelea kufanya maboresho mbalimbali ili kutoa huduma bora inayomlenga mwananchi.

Amesema kuwa maboresho yanayofanywa na Mahakama yanatekelezwa kupitia Mpango Mkakati wa Miaka Mitano, awamu ya kwanza ambayo ilikuwa kwa kipindi cha 2015/2016-2019/2020 na kwa sasa ni kipindi cha pili, kwa maana kuanzia 2020/2021 – 2024/2025 na moja ya malengo ni kuongeza kiwango cha kuridhika kwa wananchi kuhusu huduma zitolewazo na Mahakama.

“Katika kujipima kiwango cha kuridhika kwa wananchi kuhusu huduma zitolewazo, Mahakama imekuwa ikifanya utafiti kupitia mtafiti huru REPOA. Lengo la utafiti huo ni kupata maoni ya wananchi juu ya kuridhika kwao na huduma zinazotolewa na Mahakama ili kubaini maeneo yenye mafanikio na yenye changamoto yanayohitaji kufanyiwa maboresho ili kuweza kufikia dira ya Mahakama ya haki sawa kwa wote na kwa wakati,” amesema.

Mhe. Chuma amebainisha kuwa utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2015 ambao ulionyesha kuwa asilimia 61 ya watumiaji wa huduma za Mahakama waliridhika na huduma zitolewazo, huku ripoti hiyo ikiainisha baadhi ya maeneo yenye kuhitaji kufanyiwa kazi, ambapo Mahakama ilichukua hatua na kufanya maboresho katika maeneo husika.

Amesema kuwa mwaka 2019 ulifanyika utafiti mwingine ambapo matokeo yalionyesha kuwa asilimia 78 ya wananchi waliridhika na huduma zitolewazo, huku ripoti hiyo ikibainisha maboresho mengi ambayo yalikuwa yamefanyika kama vile matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hasa uendeshaji wa mashauri kwa njia ya kielekroniki na kuanzishwa kwa Mahakama inayotembea (mobile court).

Msajili Mkuu amesema utafiti huo pia ulibaini maeneo ambayo yalihitaji maboresho kama vile miundombinu na Mahakama iliyafanyia kazi maeneo yenye changamoto kwa kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo uimarishaji wa miundombinu ulioambatana na ujenzi wa Vituo Jumuishi sita (6) vya Utoaji Haki.

“Hatua zingine ni kujenga Mahakama mpya za Wilaya na Mwanzo, kuimarisha matumizi ya TEHAMA, kuanzisha kituo cha huduma kwa wateja, kutoa elimu kwa umma, kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa huduma za Mahakama kwa asilimia 98, kutoa nakala za hukumu bure, kupunguza mlundikano wa mashauri kutoka asilimia 11 hadi 4 na kuajiri watumishi wapya,” amesema.

Awali, akizungumza katika tukio hilo, Mtendaji Mkuu wa REPOA alibainisha kuwa kwa ujumla matokeo ya utafiti waliofanya yanaonyesha mabadiliko makubwa katika huduma za Mahakama. Ameipongeza Mahakama kwa usikivu na kuwasikiliza wananchi na watumiaji wa huduma za kimahakama, sehemu ambapo haki inapatikana kwa usawa.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo wa REPOA, akiwasilisha taarifa kwa ufupi ya utafiti huo alisema watu wengi wanaridhika na huduma za Mahakama kutegemea na jinsi wanavyohudumiwa na haki inavyotolewa bila kujali matokeo ya mashauri yao.

“Kwa mfano, mtu akifika mahakamani akiwa na uhakika kwamba yeye ni mkosaji, akahukumiwa na akajua kwamba amekosa bila kujali nafasi yake na ushawishi wake, basi ataridhika na utendaji wa Mahakama. Vile vile akifika mtu mahakamani na anajua siyo mkosaji awe na imani kwamba atatoka hapo akiwa salama, hali ambayo itamfanya aridhike,” amesema.

Amependekeza mambo kadhaa yafanyike ili kukidhi matakwa ya wananchi, ikiwemo upanuzi wa miundombinu ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji, kuwa na matumizi makubwa ya Mahakama Inayotembea kama suluhu ya muda, uboreshaji wa muda unaotumika katika kukamilisha mashauri na kufanya ukaguzi hasa katika Mahakama za chini ili kuthibiti maadili ya watumishi.

REPOA pia wamependekeza Mahakama kutoa elimu kwa watumishi kuhusu vigezo vya kupandishwa vyeo na uelewa juu ya mipango ya upandishaji vyeo, ​​kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu njia za mawasiliano, kwani zina ufanisi mkubwa, kukuza matumizi ya TEHAMA katika mawasiliano na mambo mengine ya kimahakama na kuongeza ufahamu wa uwepo wa kituo cha huduma kwa mteja ‘call centre’ cha Mahakama.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (kushoto) akipokea taarifa ya utafiti kuhusu kuridhika kwa watumiaji wa huduma za Mahakama kwa mwaka 2023 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dkt. Donald Mmari.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma akisisitiza jambo alipokuwa anaongea kwenye hafla ya kupokea taarifa ya utafiti kutoka REPOA.


Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dkt. Donald Mmari akieleza jambo kwenye hafla hiyo.

Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo, Dkt. Lucas Katera akifafanua jambo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utafiti huo.

Mkurugenzi wa Usimamizi, Ukaguzi wa Huduma za Mahakama, Maadili na Malalamiko, Mhe. Anna Magutu akitoa maelezo ya utangulizi kabla ya REPOA kuwasilisha taarifa ya utafiti wao.
Sehemu ya wajumbe wa menejimenti ya Mahakama ya Tanzania (juu na chini) ikifuatilia uwasilishaji wa taarifa ya utafiti wa REPOA.

Sehemu ya utafiti wa REPOA (juu na chini).

Meza Kuu ikiongozwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa REPOA. Wengine waliokaa ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Silvester Kainda (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Dkt. Donald Mmari (kulia).
Meza Kuu ikiongozwa na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wajumbe wa menejimenti ya Mahakama ya Tanzania (juu na chini) waliohudhuria hafla hiyo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni