Jumatatu, 10 Julai 2023

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI LINDI YAANZISHA ‘CLUB’ YA MAZOEZI

Na Hilari Herman-Mahakama, Lindi

Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi imeanzisha Club ya Mazoezi inayohusisha watumishi wa kada zote kushiriki katika mazoezi kila siku ya Jumamosi kwa malengo ya kuimarisha afya ya mwili na akili ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuhudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Juzi tarehe 8 Julai, 2023 mapema asubuhi watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi, wakiongozwa na Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Maria Batulaine pamoja na Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bi. Quip Mbeyela, walianza kushiriki katika mazoezi hayo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Club hiyo, Mhe. Batulaine aliwaasa watumishi si tu kushiriki katika mazoezi ya Club siku za Jumamosi bali kujijengea utaratibu wa kufanya mazoezi binafsi walau mara tatu kwa wiki ili kujiimarisha kiafya ya mwili na akili.

“Kufanya mazoezi mara kwa mara kunaimarisha kinga ya mwili na hivyo kutukinga na maradhi yasiyoambukiza. Siyo hivyo tu, mazoezi hutibu maradhi yatokanayo na mtindo mbovu wa maisha. Kwa maneno mengine, mazoezi ni kinga dhidi ya maradhi na ni tiba ya maradhi pia. Hivyo, tuone umuhimu wa kushiriki katika mazoezi mara nyingi iwezekanavyo,” alisisitiza Mhe.Batulaine.

Naye Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi aliwahakikishia watumishi kuwa atawezesha vifaa vyote muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya mazoezi.

 

Baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi (juu na picha mbili chini) nwakiwa mazoezini.


Mwalimu wa Club ya Mazoezi ya watumishi wa Mahakama Lindi Rashid Chituhuma akiwa anafuatilia kwa karibu wakati mazoezi yakiendelea.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni