Na Hilari Herman-Mahakama, Lindi
Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) Kanda ya Kusini hivi karibuni kilifanya kikao kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji katika mustakabali mzima wa utoaji haki kwa wananchi.
Mada
kadhaa ziliwasilishwa na wawezeshaji waliobobea katika maeneo mbalimbali wakati
wa kikao hicho kilichohudhuriwa na Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Mtwara, Naibu Msajili na Mahakimu wote wa Mahakama kutoka Kanda hiyo.
Miongoni
mwa mada zilizowasilishwa zilihusu nidhamu, kanuni zinazowaongozo Majaji na
Mahakimu, madhara ya rushwa, matumizi ya fedha na jinsi ya kujiwekeza kiuchumi,
faida na hasara za matumizi ya mitandao ya kijamii pamoja jinsi ya kukabili
msongo wa mawazo.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Sultan ulioko
Wilaya ya Kilwa, Mkoa wa Lindi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim aliwapongeza Mahakimu kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Aliwakumbusha
kuishi katika maadili kama miongozo, sheria na kanuni zinavyowataka. Kadhalika, Mhe. Ebrahim alisisitiza ushirikiano miongoni
mwao ili kuendeleza jukumu muhimu la utoaji haki kwa wakati.
Miongoni mwa wawezeshaji waliowasilisha mada katika
kikao hicho ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara, Mhe.
Cyprian Phocas Mkeha na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Dkt. Eliamini
Laltaika.
Akiwasilisha mada kuhusu miongozo na kanuni
zinazoongoza Majaji na Mahakimu, Mhe. Mkeha alisisitiza Mahakimu kutotumia
vibaya madaraka waliyopewa kisheria, akilenga hasa kifungu kinachozungumzia kudharau
Mahakama (Contempt of Court).
Alisema Mahakimu wengi wanatumia kifungu hicho
vibaya na kuwaasa wajitahidi kuelekeza zaidi wananchi kuhusu taratibu wanapokuwa
mahakamani badala ya kutumia kifungu hicho kama fimbo ya kuwaadhibu.
Vilevile, Jaji Mkeha alikemea suala la rushwa na kueleza
hasara zake katika jamii. Alimnukuu Jaji
Mkuu mstaafu, Mhe. Barnaba Samatta akisema, “Rushwa ni uovu mbaya sana
lakini uovu huo unakuwa mbaya zaidi pale wale ambao wanawajibu wa kushiriki
katika vita dhidi yake wanashiriki katika uovu huo. Jaji au Hakimu anayepokea
rushwa anafanya biashara haramu, anauza uhuru wa Mahakama......”
Naye Mhe. Dkt. Laltaika, akiwasilisha mada kuhusu matumizi
ya mitandao ya kijamii, alieleza faida na hasara zake na kuwataka Mahakimu kuitumia
zaidi katika kujijenga katika kazi zao na siyo kufanya mambo ambayo yanakinzana
na maadili.
Mahakimu walioshiriki kikao hicho pia walipata
darasa kuhusu uchumi kutoka kwa mwezeshaji ambapo aliwafundisha sababu
mbalimbali za mtu au taasisi kushuka kiuchumi. Aligusia baadhi ya sababu,
ikiwemo kutokuwa na elimu ya kutosha ya nanma ya utumiaji na utunzaji wa fedha.
Alisema watu wengi hawajui kujiwekea sehemu ya
mishahara yao na kuweka kama amana kwa muda ili kuweza kujizalisha. Pia
alipambanua kwa kina jinsi gani Mahakimu hao wanaweza kuweka asilimia kidogo ya
mishahara kwa muda fulani ili kuwasaidia katika kujikuza kiuchumi na
kimaendeleo.
Mada nyingine iliyowasilishwa ilihusu jinsi ya
kukabili msongo wa mawazo ambapo mwezeshaji alielezea sababu mbalimbali
zinazoweza kupelekea hali hiyo. Hata hivyo, aliwataka washiriki kukubaliana na
hali halisi ya maisha na mitazamo yao na siyo kuiga maisha ya wengine ili
wasijikute kwenye wimbi la msongo wa mawazo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni