Na Faustine Kapama-Mahakama
Majaji watano wa Mahakama Kuu ya Tanzania jana tarehe
6 Julai, 2023 wameungana na Watanzania kutembelea banda la Mahakama ya Tanzania
kwenye Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba) yanayofanyika katika Viwanja
vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa, Mkoa wa Dar es Salaam.
Majaji hao walifika katika banda hilo la Mahakama
lililopo mkabala na Banda la Jeshi la Kujenga Taifa kwa nyakati tofauti tofauti
na kukutana na watumishi kutoka kurugenzi, idara na vitengo mbalimbali wakiwa wanatoa
huduma na elimu kwa wanannchi kuhusu mambo mbalimbali ya kisheria.
Aliyekuwa wa kwanza kuwasili katika banda hilo alikuwa
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza
Luvanda aliyefuatiwa na Jaji Arafa Msafiri ambaye pia anatoka katika Divisheni
hiyo.
Jaji mwingine ni Mhe. Lusungu Hemed, ambaye pia
anatoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi na kufuatiwa na Jaji
Mfawidhi Mahakama ya Biashara, Mhe. Cyprian Mkeha, kabla ya Mhe. Dkt. Zainab
Mango kutoka Divisheni ya Ardhi kukamilisha ziara ya Majaji kutembelea Banda
hilo.
Viongozi wengine waandamizi wa Mahakama walioungana na
Majaji hao kutembelea banda la Mahakama ni Watendaji pacha wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Bw. Leonard Magacha na Bi. Mary Shirima ambaye alifika katika
maonesho hayo tarehe 5 Julai, 2023.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante
Ole Gabriel ndiye aliyefungua pazia la viongozi wa Mahakama kutembelea banda la
Mahakama tarehe 4 Julai, 2023 na kufuatiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kituo
Jumuishi cha Masuala ya Familia, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina alikuwa wa tatu kufika katika maonesho hayo ambapo
alitembelea banda la Mahakama mapema tarehe 6 Julai, 2023.
Katika maonesho hayo, Mahakama ya Tanzania ipo katika
banda moja na baadhi ya wadau wake muhimu, wakiwemo Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Wadau wengine ni Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA),
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Shule ya Sheria kwa Vitendo
Tanzania na wengine, ambao wanatoa elimu ya sheria kwenye maeneo yao.
Huduma zinazotolewa na Mahakama katika maonesho hayo
ni Mahakama Inayotembea kusikiliza mashauri mbalimbali, kutoa elimu kuhusu
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) mahakamani na safari
kuelekea Mahakama Mtandao, e-Judiciary.
Kadhalika, kuna utoaji wa elimu kuhusu huduma na
taratibu mbalimbali za ufunguaji wa mashauri, yakiwemo ya mirathi na utoaji wa
elimu kuhusu masuala ya ndoa, talaka, wosia na mirathi.
Wataalamu wa Mahakama pia wanaelezea mfumo ulioboreshwa
wa kusajili, kuratibu na kusimamia uendeshaji wa mashauri na kuelezea huduma
zinazotolewa na ngazi mbalimbali za Mahakama, ikiwemo Divisheni zake.
Katika kipindi hicho cha maonesho, watalaam hao wanatoa
elimu kwa wananchi kutambua umuhimu wa kutumia Kituo cha Huduma kwa Mteja, ‘Call
Centre’ cha Mahakama ya Tanzania katika kutoa maoni na malalamiko na namna ya
kupata mrejesho.
Mahakama pia, kupitia Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto, itatoa fumu za udahili na kuzipokea zile ambazo zimeshafanyiwa kazi,
huku Chama cha Mawakili Tanyanyika kikiwa bega kwa bega kutoa msaada wa kisheri
kwa wananchi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni