Na Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Mfawidhi Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewaomba Majaji
wenzake na watumishi wa Mahakama kwa ujumla kwenda na mabadiliko ya kimfumo na
teknolojia ili kuleta mafaniko katika kazi ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Maghimbi ametoa ombi
hilo leo tarehe 7 Julai, 2023 alipokuwa akiwakaribisha Majaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania wanaounda kundi la tatu kushiriki kwenye mafunzo kuhusu mfumo mpya
wa kielektoniki ulioboreshwa, ‘advanced e-case management system’ yanayofanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.
“Mafanikio yetu kama Mahakama
yatategemea sana utayari wetu katika kukabili mabadiliko ya kimfumo. Mfumo huu mpya
wa kielekrioniki wa kuratibu mashauri utarahisisha kazi ya utoaji haki katika
nchi yetu. Kwa hiyo, tusichukulia kwamba kitu kinachokuja kitafanya kazi iwe
ngumu,” amesema.
Jaji Mfawidhi amesema kuwa
kama Majaji watauelewa vizuri mfumo huo na kuutumia wataendelea kuwa mabalozi na
vinara wa mabadiliko ya kiteknolojia, siyo tu kwa Mahakama ya Tanzania, bali
pia kwa taasisi nyingine ndani na nje ya nchi.
Alielezea matumaini yake
kuwa watakaporejea kwenye maeneo yao ya kazi, kila kituo kitakuwa na utaratibu
maalum wa uhamasishaji wa namna nzuri ya kupokea mabadiliko hayo makubwa ili
kuondoa uwezekano na mkwamo wowote katika safari kuelekea Mahakama Mtandao.
“Kila mmoja wetu
atajibeba atakuwa balozi kwa walioko chini yake kuanzia karani na wote waliopo mahakamani
kuhakikisha kwamba mfumo huu unafikia lengo ambalo limekusudiwa,” Mhe. Maghimbi
amesema.
Jaji Mfawidhi
amebainisha kuwa maboresho makubwa ya mfumo huo yamejikita katika kurahisisha
usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao kupitia nyaraka pepe za kimahakama, upangaji
wa mashauri kwa Majaji na Mahakimu, usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao
na kuruhusu mienendo ya mashauri kuandikwa moja kwa moja.
Amesema pia kuwa ujenzi
wa mfumo huo umezingatia mchakato mzima wa shughuli za kimahakama kwa ngazi
zote ili kuhakikisha kwamba hatua za usikilizaji wa mashauri zinachakatwa
kimfumo na kuondokana na matumizi ya karatazi.
Mhe. Maghimbi amesema kukamilika
kwa ujenzi huo ni moja ya mafanikio makubwa ambayo Mahakama ya Tanzania
inapaswa kujivunia, hasa pale wanapopiga hatua kuelekea kwenye matumizi kamili
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji haki nchini.
“Mfumo huu utasaidia kutatua
changamoto na mapungufu mbalimbali, ikiwemo kuelemewa na uzito wa nyaraka,
kushindwa kuhifadhi kumbukumbu za mienendo ya mashauri na matatizo mengine
mengi yaliyokuwa yanaonekana kwenye mifumo iliyokuwa inatumika hapo awali,”
amesema.
Hivyo, Jaji Mfawidhi amewapongeza
watalaam kutoka Kurugenzi za Teknolojia ya Habari na Mawasiliamno (TEHAMA) na
Usimamizi wa Mashauri kwa kufanya kazi kubwa ya kujenga mfumo huo.
Awali akiwasilisha neno
la utangulizi, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema
mafunzo hayo yanafanyika kwa Majaji wote wa Mahakama Kuu kuwapa uelewa wa mfumo
huo wa advanced case management system, kwa vile wao ni miongoni mwa watumiaji
wakubwa.
Alisema Majaji wamekuwa
mstari wa mbele katika kusaidia kutoa maoni pale wanapokutana na hoja
mbalimbali zinazohusu mifumo ambayo inaendelea, hivyo wanategemea wakati wa
mafunzo kupata mrejesho kutoka kwao kwenye maeneo ya kufanyia maboresho.
Msajili Mkuu aliwaambia Majaji
hao kuwa mfumo ambao watapitishwa umejengwa na wataalam wa ndani ya Mahakama ya
Tanzania, hivyo alichukua fursa hiyo kuwapongeza kwa kazi hiyo nzuri.
“Maeneo mengi, hata katika
nchi zingine hawaamini mifumo hii imejengwa na watalaam wetu wa ndani. Baadhi
ya maeneo ambayo tumeenda wameonyesha shauku ya aidha kuja kujifunza au kuomba
wataalam wetu waende wakawape elimu wamefanyaje mpaka kuunda mifumo hii ambayo
kwa sasa inafanya kazi kwa ufanisi,” alisema.
Kufanyika kwa mafunzo
kuhusu mfumo huo mpya ni mwendelezo wa yale yaliyotolewa kwa Majaji wa Mahakama
ya Rufani na makundi mawili ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika ukumbi
huo hivi karibuni. Mafunzo hayo yalifunguliwa kwa mara ya kwanza na Jaji Mkuu
wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya nyingine ya Majaji wanaoshiriki mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni