Alhamisi, 6 Julai 2023

IGP WAMBURA ATEMBELEA BANDA LA MAHAKAMA YA TANZANIA ‘SABASABA’

Apongeza maboresho ya utoaji huduma za Mahakama

Na Mary Gwera, Mahakama

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura amepongeza hatua ya maboresho mbalimbali yanayofanywa na Mahakama nchini yanayolenga kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi. 

IGP Wambura amebainisha hayo leo tarehe 06 Julai, 2023 alipotembelea banda la Mahakama ya Tanzania lililopo katika maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa almaarufu ‘Sabasaba’ yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Akiwa katika sehemu ya banda la Kurugenzi ya Usimamizi, Ukaguzi wa Huduma za Mahakama, Maadili na Malalamiko iliyopo ndani ya banda kuu la Mahakama, Mkuu huyo amepongeza taratibu wanazotumia katika ushughulikiaji wa malalamiko.

“Niwapongeze Mahakama mnafanya kazi nzuri, hata hivyo tusichoke kujitoa katika kushughulikia malalamiko ya raia kwa sababu Polisi na Mahakama ni Taasisi zinazolalamikiwa sana kwakuwa zinagusa haki za watu hivyo tusione kama kero bali tushughulikie malalamiko hayo kwa moyo,” amesema IGP Wambura.

Kadhalika akiwa sehemu ya Kituo cha Huduma kwa Mteja ‘Call centre’ cha Mahakama ambacho pia kinapatikana ndani ya banda la Mahakama, Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi ameonesha kufurahishwa na kupongeza ufanyaji kazi wa Kituo hicho na kusema kuwa Jeshi hilo litaiga mfano wa Mahakama wa kuwa na mfumo maalum wa kushughulikia malalamiko ya wananchi.

Mkuu huyo alitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo ndani ya banda la Mahakama ikiwa ni pamoja na banda la Maboresho ambapo alielezwa miongoni mwa maeneo ambayo Mhimili huo umezingatia katika uboreshaji wa huduma zake ni pamoja na kufanya mafunzo ya wadau wa ndani na nje ya Mahakama ili kwenda pamoja katika safari ya maboresho, uanzishwaji wa Kurugenzi ya kushughulikia malalamiko na kadhalika.

Katika hatua nyingine; IGP Wambura alipotembelea banda la Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke alielezwa na moja ya mtoa elimu wa banda hilo ambaye ni Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Kituo hicho, Mhe. Simon Swai amemueleza Mkuu huyo kuwa, kwenye malipo ya mirathi kwa Askari Polisi kuna changamoto ambayo inasababisha ucheleweshaji wa haki ya kurithi hasa kwa wajane na Watoto.

Kuhusu changamoto hiyo, Mkuu huyo amependekeza kuwe na kikao cha pamoja kati ya Mahakam ana Jeshi hilo ili changamoto tajwa iweze kufanyiwa kazi.

“Naomba muitishe kikao na Jeshi la Polisi ili tuweze kuangalia namna bora ya kuishughulikia changamoto hii kwa haraka,” amesisitiza IGP Wambura.

Mahakama ya Tanzania ni miongoni mwa washiriki wa maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa, 2023 yanayoendelea, banda la Mahakama lipo mkabala n abanda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ndani ya Viwanja vya ‘Sabasaba’.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura (kulia) akipata maelezo kuhusu maboresho mbalimbali ya Mahakama kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Ufuatiliaji, Bi. Gladys Qambaita. IGP Wambura ametembelea banda la Mahakama leo tarehe 06 Julai, 2023 katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere 'Sabasaba' jijini Dar es Salaam.


Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura akipata maelezo kutoka kwa Maafisa wanaohudumu katika Kurugenzi ya Usimamizi, Ukaguzi wa Huduma za Mahakama, Maadili na Malalamiko pamoja na Kituo cha Huduma kwa Mteja 'Call Centre' ya Mahakama. IGP Wambura amepata maelezo ya huduma mbalimbali za Mahakama leo tarehe 06 Julai, 2023 alipotembelea banda la Mahakama ya Tanzania katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba'.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura akizungumza jambo na Maafisa wanaotoa elimu ya masuala ya familia na mirathi wakati Mkuu huyo wa Polisi alipotembelea banda la Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke lililopo katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa 'Sabasaba'.
IGP Camillus Wambura akipata maelezo kutoka Mwakilishi wa banda la Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
IGP Camillus Wambura akipata maelezo kutoka Mwakilishi wa banda la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) lililopo ndani ya banda la Mahakama ya Tanzania alipotembelea Mkuu huyo wa Polisi.
IGP Wambura akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.
Maelezo kutoka banda la Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri-Mahakama ya Tanzania. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msajili Usimamizi wa Mashauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Moses Ndelwa na kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Hawa Mnguruta.

(Picha na Dhillon John, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni