Ijumaa, 28 Julai 2023

MKUU WA MKOA WA SHINYANGA AMKABIDHI JAJI MFAWIDHI VITENDEA KAZI

 

Na Emmanuel Oguda – Mahakama - Shinyanga

 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme jana tarehe 27 Julai, 2023 amekabidhi mashine za uchapaji (printer) tano za kisasa kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Mhe. Frank Mahimbali. 

 

Makabidhiano hayo yamefanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni ahadi iliyotolewa na Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa ya Kahama, Halmashauri ya Ushetu na Halmashauri ya Msalala ambapo waliahidi kutoa ‘’Printers’’ 10 na kwa kuanzia tayari wametoa ‘’printers’’ tano (5) ambazo zimekabidhiwa.

 

Mhe. Mndeme amesema kuwa, anatambua kazi kubwa inayofanywa na Mahakama ya Tanzania katika kutoa haki kwa wananchi, hivyo kwa vitendea kazi  vitawezesha Mahakama za Mwanzo kuongeza kasi zaidi katika utendaji wa kazi wa kila siku. Mhe. Mndeme kama alivyoahidi kushirikiana na Mahakama Mkoa wa Shinyanga hivi karibuni, ameendelea kusisitiza kuwa ataendelea kutoa ushirikiano kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kwenye masuala mbalimbali ya utoaji haki kwa wananchi wa Shinyanga.

 

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Mhe. Frank Mahimbali, kwa niaba ya watumishi na Menejimenti ya Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, ametoa shukrani za dhati kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zilizochangia upatikanaji wa vitendea kazi hivyo na kuendelea kuwaomba ushirikiano katika masuala yahusuyo utoaji haki kwa wananchi.

 

‘’Mhe. Mkuu wa Mkoa kipekee kabisa nikushukuru wewe pamoja na Wakurugenzi hawa ambapo kwa namna ya kipekee wamewezesha kupatikana kwa vitendea kazi hivi ambavyo vyote vitaenda kufanya kazi Mahakama za Mwanzo, kwa sasa Mahakimu wote wanazo Kompyuta mpakato (Laptop), kwa kupata vitendea kazi hivi, kasi ya utoaji wa nakala za hukumu itaongezeka zaidi kwa kuwa mashine hizi zinaenda kusukuma kasi zaidi,’’ amesema Mhe.  Jaji Mahimbali.

 

Akiongea kwa niaba ya Wakurugenzi waliochangia upatikanaji wa ‘’printer’’ hizo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Bw. Anderson Msumba, amesema kuwa vitendea kazi hivyo ni miongoni mwa ‘’printers’’ 10 zilizoahidiwa kutolewa kwa ajili ya kuwezesha Mahakama za Mwanzo kutenda kazi zake kwa ufanisi zaidi, printers tano zilizobaki zitatolewa na kukabidhiwa kwa Mahakama hivi karibuni. Aidha, ameongeza kuwa Halmashauri hizo zitaendelea kushirikiana na Mahakama ya Tanzania kwa mambo mbalimbali yanayolenga kusaidia wananchi katika kupata haki zao kwa wakati.

 

Kwa upande wake Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Shinyanga, Bi. Mavis Miti, amewashukuru Wakurugenzi hao kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama. ‘’niwashukuru sana wadau wetu muhimu kwa kuendelea kutuunga mkono na kutusaidia katika masuala mbalimbali, hata jengo la Mahakama ya Wilaya Kahama tunalotumia kwa sasa limetoka Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, hii inaonyesha ni jinsi gani Halmashauri hizi zinashirikiana vyema na Mahakama katika kuboresha huduma kwa wananchi.

 

Utoaji wa vitendea kazi hivyo (printers) ni muondelezo wa ushirikiano baina ya Mahakama na wadau katika kufanikisha lengo la utoaji haki kwa wakati kama ilivyoainishwa katika nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa miaka mitano  wa awamu ya kwanza na pili wa mwaka 2020/2021 – 2024/2025 inayosema Kuongeza Imani ya Wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau katika Shughuli za Mahakama.

 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Christina Mdeme akiongea jambo wakati wa makabidhiano ya vitendea kazi (printers).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akifurahia jambo alipokuwa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
 Mtendaji wa Mahakama Bi. Mavis Miti akifuatilia kwa makini makabidhiano ya vitendea kazi.
 Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Bw. Anderson Msumba, akisisitiza jambo wakati wa makabidhiano ya vitendea kazi hivyo.
   Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme (kushoto) akimkabidhi vitendea kazi (printers) kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga Mhe. Frank Mahimbali.
    Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (kulia), Wengine ni) Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Prof. Cizer Tumbo (wa kwanza kulia), Mtendaji wa Mahakama Shinyanga, Bi. Mavis Miti (wa tatu kulia, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Bw. Anderson Msumba (wa nne kushoto) Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu Bi. Hadija Kabojela (wa tatu kushoto) Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Bw. Khamis Katimba (wa pili kushoto), Msaidizi wa Sheria wa Jaji na Bi. Nashilaa Mollel (wa pili kulia na Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Bw. Dushi Lugoye (wa kwanza kushoto).


(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama).

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni