·Kati ya watu 100 watatu ndiyo wenye mtazamo hasi
·Mtandao kuunganisha Mahakama wasambaa nchi nzima
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro
Mahakama ya Tanzania imepata mafanikio makubwa katika utoaji haki nchini
kiasi cha kuongeza kwa kiasi kikubwa imani ya Wananchi kuwa wanaweza kupata
huduma za kimahakama bila kutoa rushwa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu
wa Kitengo cha Maboresho cha Mahakama ya Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha alipokuwa
akiwasilisha taarifa ya Mkakati wa Maboresho siku ya pili ya Mkutano wa Mwaka wa
Mahakama ya Rufani unaofanyika mjini hapa.
Mhe. Dkt. Rumisha
amewaambia Wajumbe wa Mkutano huo kuwa tafiti ambazo zimezifanyika mwaka 2015,
2019 na 2023 zinaonyesha maendeleo chanya kwa kila eneo, ikiwemo suala la
rushwa ambalo mwaka 2015 ilikuwa asilimia tisa, mwaka 2019 ikashuka hadi asilimia
sita na mwaka 2023 imefika asilimia tatu.
“Hii ina maanisha kuwa kati
ya watu 100 wanaoulizwa kwa sasa ni watatu tu wanaosema hawawezi kupata haki
mpaka watoe rushwa, kitu ambacho ni tofauti kwa mwaka 2015 ambao walikuwa watu
tisa,” Mkuu wa Kitengo cha Maboresho amesema.
Mhe. Dkt. Rumisha ameeleza
kuwa kwa ujumla idadi ya watu wanaoridhika na huduma za Mahakama imeongezeka. Amesema
mwaka 2015 ilikuwa asilimia 61 ya watu waliokuwa wanaamini wakienda mahakamani
watapata haki.
“Tumefanya utafiti tena
mwaka 2019, watu asilimia 78 wakasema wakienda mahakamani wanaweza kupata haki,
sasa hivi mwaka huu wa 2023 ni asilimia 88 wanasema wakienda mahakamani
watapata haki. Haya ni mafanikio makubwa sana,” amesema.
Amebainisha kuwa Mahakama
ya Tanzania ilikuwa imejiwekea lengo la kufikia asilimia 82 kwa mwaka 2023
kutoka asilimia 78 kwa mwaka 2019, lakini kiwango kimepanda hadi asilimia 88
kuliko matarajio, hali inayoonyesha wananchi wanaiamini zaidi Mahakama kuliko yenyewe
ilivyotarajia.
Kuhusu mlundikano, Mhe. Dkt. Rumisha ameeleza kuwa takwimu zimekuwa zikishuka kila mwaka na mpaka mwezi
Juni, 2023 imefikia asilimia tatu ya mashauri yote ambayo hakuna nchi nyingine
katika Ukanda wa Afrika Mashariki imefikia.
Amewaambia wajumbe wa
Mkutano huo kuwa idadi hiyo imeendelea kushuka mfululizo, mfano mwaka 2022
ilikuwa asilimia sita na kufikia mwezi Juni 2023 imekuwa asilimia tatu na itaendelea
kushuka kufikia mwezi wa 12, 2023.
“Ukilinganisha na miaka
ya nyuma, mwaka 2015 ilikuwa asilimia 15, mwaka 2021 ikaja asilimia 10, mwaka
2022 ikawa asilimia sita na sasa Juni 2023 imekuwa asilimia tatu ya mashauri
yote,” Mkuu wa Kitengo cha Maboresho amesema.
Mhe. Dkt. Rumisha amefafanua
kuwa mlundikano huo haupo kwenye Mahakama za Mwanzo ambazo zinasikiliza
mashauri kwa asilimia kubwa. Amebainisha kuwa asilimia 68 ya mashauri au mashauri
asilimia 68 ya wananchi wanaoenda mahakamani yanaisha kabla hayajawa mlundikano.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Kalege Enock, akiwasilisha
mada katika Mkutano huo, amesema Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kujenga
mtandao mpana na kuwezesha Mahakama karibu zote kuunganishwa.
“Mtandao huu umeunganisha
Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu na Mahakama za Hakimu Mkazi kwa asilimia 100,”
Bw. Kalege amewaambia wajumbe wa Mkutano alipokuwa anawasilisha mada kuhusu Hali
ya Mifumo na Matumizi ya TEHAMA kuelekea Mahakama Mtandao.
Amebainisha kuwa Mahakama
za Wilaya zimeungwa kwa asilimia 97 na zilizobakia zitaunganishwa mpaka ifikapo
mwezi Oktoba, 2023, huku uunganishwaji wa Mahakama za Mwanzo ukiendana na uboreshaji
wa hali ya majengo.
Amependekeza Mahakama ya
Rufani kuendelea kujitathimi na kuboresha mtiririko wa kazi zake (workflow) ili
kuendelea kunufaika na matumizi ya TEHAMA na pia kuendelea kuonesha mfano kwa vitendo
katika matumizi ya TEHAMA mahakamani.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jacobs Mwambegele akichangia hoja.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani naye hakuwa nyuma kuchangia kwenye taarifa hizo mbili zilizowasilishwa kwenye Mkutano huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni