Na Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro
Mkutano wa Mwaka wa Mahakama ya Rufani Tanzania uliokuwa
unafanyika mjini hapa katika Hoteli ya Nashera kutathmini na kujadili utendaji
wa Mahakama hiyo katika maeneo mbalimbali kimehitimishwa leo tarehe 28 Julai,
2023.
Akizungumza wakati anafunga Mkutano huo, Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesisitiza kuendelea kufanyia kazi suala
la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mahakama ya
Rufani ili kuimarisha utendaji katika utoaji wa haki kwa wananchi.
“Taarifa ya Msajili wa Mahakama inaonyesha kuwa bado
mashauri katika Mahakama ya Rufani yanafunguliwa kwa njia ya kawaida, Masjala Kuu
na Masjala ndogo hazisomani. Hili ni eneo ambalo tunatakiwa kulifanyia kazi,” Mhe.
Prof. Juma amesema.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa katika karne ya 21 utoaji wa
huduma, zikiwemo haki zinahamia kwenye mifumo ya kidigitali, hivyo kuanzia sasa
itakuwa kawaida kutumia mifumo hiyo kama njia muhimu ya kuleta ufanisi,
kuongeza uwazi na umahiri katika utoaji wa huduma.
“Hili ni eneo ambalo kila mmoja wetu ajielekeze. Mahakama
ilikofikia sasa na baada ya taarifa ya Tume ya Haki Jinai kupendekeza mfumo
jumuishi wa haki jinai haina budi kuhakikisha kwamba tunaendelea kuwa mstari wa
mbele katika hili eneo ambalo wenzetu wanatusifu tumepiga hatua kubwa sana,” amesema.
Jaji Mkuu amewataka wajumbe wa Mkutano huo kuwasilisha
mawazo yao ya kimaboresho kwenye kamati ya TEHAMA ambayo inasaidia kuangalia
katika eneo hilo kila siku.
Kadhalika, Mhe. Prof. Juma amewahimiza wajumbe hao kuyafanyia
kazi yale yote yaliyojitokeza katika Mkutano huo, ikiwemo maoni na mapendekezo
ambayo yatasaidia katika kuimarisha utendaji mahakamani.
“Mada zote na mawasilisho yote yaliyotolewa
yametuongezea uelewa na kutusaidia sana katika kufunga mkanda vyema ili kukabiliana
na mlundikano wa mashauri katika Mahakama ya Rufani,” amesema.
Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa ataendelea kufuatilia
maazimio yote yaliyofikiwa ili kujua namna yanavyotekelezwa kabla ya Mkutano
ujao wa Mahakama ya Rufani.
Awali, akimkaribisha Jaji Mkuu kufunga Mkutano huo, Mwenyekiti
Mwenza, Mhe. Augustine Mwarija alieleza kuwa baada ya kutathmini na kutokana na
mada zilizotolewa wameona utendaji wa Mahakama ya Rufani umekuwa mzuri.
Mhe. Mwarija, kwa niaba ya Majaji wengine wa Mahakama
ya Rufani, amemshukuru Jaji Mkuu kwa uongozi wake mahiri ambao umepelekea uwepo
wa mafanikio makubwa katika utendaji kazi.
“Mafanikio haya yametokana na uongozi wako mzuri.
Nitoe shukrani pia kwa kamati ya maandalizi kwa ufanisi mkubwa,” amesema.
Katika Mkutano huo wa
siku mbili ulioanza jana tarehe 27 Julai, 2023, taarifa na mada mbalimbali ziliwasilishwa,
ikiwemo inayohusu mashauri kwa kipindi cha Januari hadi Disemba, 2022.
Taarifa nyingine ilihusu hali
ya mifumo ya TEHAMA, maboresho yanayoendelea na safari ya kuelekea Mahakama
mtandao.
Pia kulikuwepo na
uwasilishaji wa mada mbalimbali kutoka kwa wawezeshaji wabobezi, wakiwemo Majaji
wa Mahakama ya Rufani wastaafu, Mhe. Edward Rutakangwa na Mhe January Msoffe.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama walialikwa kwenye Mkutano huo, akiwemo Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni