Na Amani Mtinangi Mahakama Kuu Tabora
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, jana tarehe
30 Julai, 2023 ilishiriki kikalilifu katika Bonanza la Michezo lililoandaliwa
na Chama cha Riadha mkoani hapa na kuibuka mshindi wa kwanza katika mbio za
mita 100 na mita 200 kwa wanawake.
Bonanza hilo lililofanyika katika Uwanja wa Ally
Hassan Mwinyi lilihudhuriwa na Taasisi za Umma, Vyuo na Sekondari mbalimbali za
Mkoa wa Tabora. Pamoja na riadha, mashindano mengine yaliyofanyika ni kurusha
Tufe na Mkuki.
Ushindi huo wa Mahakama Kuu Tabora ni salamu kwa timu
zitakazishiriki katika Bonanza la Michezo litakalofanyika katika Mkoa wa Bukoba
hivi haribuni.
Akizungumza wakati anafungua Bonanza hilo, Afisa Elimu
wa Mkoa, Mwl. Juma Kaponda, kwa niaba ya Katibu Tawala, aliwapongeza washiriki na
kueleza jinsi michezo inavyoboresha afya.
Alieleza jitihada mbalimbali za Serikali katika kukuza
na kuendeleza michezo mkoani Tabora, ikiwemo uwekezaji wa takribani milioni 800
za Kitanzania katika sekta ya michezo kama ukarabati wa viwanja vya shule
yalipofanyikia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA kwa miaka miwili mfululizo.
“Michezo ni Afya, michezo ni udugu na mshikamano, kwa
kulitambua hilo, Serikali imedhamiria kukuza michezo na kuwekeza fedha na nguvu
ili kila mwananchi na watumishi na Umma kwa ujumla wapate fursa ya kushiriki
kikamilifu,” alisema.
Katibu wa Riadha Mkoa wa Tabora, Zuberi Kalugutu aliwapongeza
watumishi wa Mahakama kwa jinsi walivyoitikia wito wa kushiriki katika Bonanza
hilo na kuwaasa watumishi wa taasisi zingine kuiga mfano huo.
“Leo tumeshirikiana vyema na watumishi wa taasisi
mbalimbali, lakini kipekee ninayofuraha kuwapongeza wenzetu wa Mahakama kufika
na kushiriki kikamilifu katika shughuli hii, kwa kweli ni jambo la kuigwa,”
alisema.
Akizungumzia mashindano hayo, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo
Tabora Mjini, Bumi Mwakatobe aliwashukuru waandaaji wa Bonanza hilo na kuwaomba
hilo lisiwe la mwisho. Aliwaasa wanawake kushiriki katika michezo.
“Mimi binafsi niwashukuru waandaaji na waliotoa wazo
la kuandaa Bonanza hili. Tumefurahi kushiriki ninaomba mabonanza kama haya
yaendelee kufanyika, hili lisiwe la mwisho. Lakini pia wanawake wenzangu
wajitahidi sana kushiriki michezo ili wasipitwe na fursa za kimichezo,”
alisema.
Hakimu Mkazi Mwandamizi Christopher Mdoe akishiriki katika mashindano ya kuruka umbali.
Afisa Utumishi wa Mahakama Kuu Kabora Amani Mtinangi akishiriki mashindano ya kurusha mkuki.
Watumishi wa Mahakama (wenye tisheti za bluu bahari) wakimsikiliza Mgeni Rasmi (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Bonanza hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni