Jumatatu, 31 Julai 2023

JAJI MFAWIDHI TABORA ATAKA WATUMISHI WAPYA KUZINGATIA WELEDI, UADILIFU, UWAJIBIKAJI

Na Amani Mtinangi Mahakama Kuu Tabora

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Athuman Matuma amewataka watumishi ajira mpya kuzingatia weledi, uadilifu na uwajibikaji katika kuteleza majukumu yao.

Mhe. Matuma alitoa wito huo kwa watumishi hao alipokutana nao ofisini kwake hivi karibuni kwa mazungumzo mafupi. Jaji Mfawidhi pia aliwaasa kuipenda kazi yao wakati wote.

“Nianze kwa kuwapongeza wote mliopata fursa adhimu ya kuajiriwa katika utumishi wa Umma na kwa umahsusi kabisa ndani ya Mahakama ya Tanzania. Pamoja na pongezi hizo kila mmoja wenu akazingatie mambo makuu matatu…

“…. weledi, uadilifu na uwajibikaji. Katika mambo hayo, mkizingatia miongozo ya kazi zenu ndipo msingi wa utumishi wa Umma uliotukuka umejengwa,” alisema.

Mhe. Matuma aliwaasa pia watumishi hao kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao, kwani Dunia ya sasa inahitaji watu wenye uelewa wa hali ya juu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mambo mengine.

Aliyataja mambo hayo kama kutenda haki bila kubagua, kuwa na uwezo wa kufanya kazi kama timu, kutokuwa na hulka za ubinafsi, kuheshimu viongozi, kuacha mienendo mibaya kama wanayo na kufanya lililo bora na kukubaliwa na jamii.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Tabora, Mhe Niku Mwakatobe aliwaeleza ajira mpya wawe tayari kujifunza kwa vitendo utendaji kazi na kuwa wabunifu katika shughuli zao ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli zao.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu, Bi. Hawa Mang’ombe aliwakaribisha watumishi hao wapya na kuwahakikishia kuwa Tabora ni mahali pazuri pa kufanya kazi, hivyo wasiwe na hofu.

Aliwaeleza kuwa uongozi wa Mahakama Kanda upo tayari kuwasaidia kwa kadri ya uwezo wake iwapo watakutana na changamoto yoyote.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Athuman Matuma akieleza jambo wakati akizungumza na watumishi ajira mpya.

Baadhi ya watumishi ajira mpya wakiwa katika kikao cha ukaribisho katika Ofisi ya Jaji Mfawidhi.

Afisa Tawala Mahakama ya Wilaya Tabora, Bi. Bhoke Makondo akiwafanyia mafunzo ya awali watumishi hao.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni