Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Menejimenti ya Mahakama Mkoa wa Pwani imetakiwa kuhakikisha kuwa kila Kiongozi anafanya kazi katika mazingira yanayoridhisha kwakuwa wao ndio wasimamiaji wakubwa wa rasilimali watu, fedha, majengo na vyote vinavyohusika.
Kauli hiyo ilitolewa
hivi karibuni na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani,
Mhe. Joyce Mkhoi katika kikao cha robo ya pili ya mwaka cha menejimenti.
Mhe. Mkhoi
amewataka viongozi hao kuwasimamia vizuri walio chini yao kwa kuhakikisha wanatekeleza
majukumu yao kwa kufuata misingi na kanuni za kazi wanazozifanya na pia
kutekeleza majukumu hayo kwa uadilifu na weledi.
Aidha, Hakimu
Mfawidhi aliwaasa wajumbe kujitahidi katika Mahakama zao kusikiliza mashauri kwa
njia ya mtandao ili huduma hiyo iweze kuzoeleka na kuwahudumia wateja bila
kujali umbali walipo. Aliwataka kwenda kidijitali ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea
katika Mahakama ya Tanzania.
Mhe. Mkhoi aliwahimiza
kuhakikisha ukaguzi wa Mahakama za Mwanzo unafanyika kwa kila robo ya mwaka ili
kujua changamoto na mapungufu na kuyatolea taarifa yale ambayo hayatatuliki
katika ngazi zilizopo kama kutekeleza sera za Mkoa kwa Mahakama hizo hutokuwa na
kesi zilizozidi miezi mitatu.
Kadhalika, aliwakumbusha
wajumbe hao kusimamia na kukagua mfumo wa uingizaji wa mashauri kwa Mahakama za
Mwanzo. Akisisitiza jambo hilo, Mhe. Mkhoi alisema “Isiwepo Mahakama ambayo
haiingizi taarifa hizo katika mfumo husika kwa usahihi.”
Kikao hicho cha
menejimenti kinahusisha Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya, Mtendaji
wa Mahakama Mkoa pamoja na Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni