Jumanne, 1 Agosti 2023

MAHAKAMA KANDA YA MUSOMA YAFANYA KIKAO CHA MENEJIMENTI

Na Francisca Swai – Mahakama, Musoma

Menejimenti ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, hii karibuni ilifanya kikao kutathmini utendaji kazi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na kuweka malengo ya mwaka mpya wa fedha 2023/2024.

Kikao hicho kilichofanyika wilayani Serengeti kilifunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya ambaye alihimiza uadilifu, weledi na uwajibikaji kazini.

Mhe. Mtulya aliwataka wajumbe wa kikao hicho cha menejimenti kuzingatia yale yote watakayokubaliana ili kuimarisha utendaji na kufikia malengo yanayokusudiwa.

Jaji Mfawidhi alitumia nafasi hiyo kuwapongeza watumishi wote kwa kuzingatia maelekezo ya Jaji Mkuu na viongozi wa ngazi za juu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika huduma za utoaji haki.

Alibainisha kuwa mashauri yote yaliyosajiliwa yalifunguliwa kwa njia ya mtandao, jumla ya mashauri 205 yamesikilizwa kwa njia ya simu na video conference na maamuzi mbalimbali yamepandishwa kwenye mfumo wa TANZLII.

Mhe. Mtulya alieleza pia kuwa matumizi ya mifumo ya mjue wakili wako (e-wakili), maktaba mtandao (e-library), matumizi ya ofisi mtandao yamesaidia masuala mbalimbali kushughulikiwa kwa wakati na kudhibiti upotevu wa nyaraka.

Katika kikao hicho, wajumbe walipokea taarifa mbalimbali, ikiwemo ya Mkaguzi wa Ndani na ile ya shughuli za ugavi na manunuzi zilizobainisha maeneo yaliyofanywa vema na yanayohitaji maboresho na umakini zaidi.

Pia kulikuwepo na taarifa ya hali ya mashauri iliyowasilishwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Moshi ambaye alielezea namna kazi kubwa iliyofanyika katika usikilizaji wa mashauri kuanzia ngazi ya Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama Kuu.

Mhe. Moshi alisema kuwa mwezi Desemba 2021 Mahakama Kuu ilivuka na mashauri 554 na mwaka 2022 yalisajiliwa 981, yaliyoamuliwa na Majaji watatu yalikuwa 1,007. “Kwa takwimu hizi, kila Jaji aliamua wastani wa mashauri 336 na kufafanya wastani wa uondoshaji Mahakama Kuu peke kuwa asilimia 103,” alisema.

Aidha, Naibu Msajili alieleza kuwa kwa mwaka 2023 katika kipindi cha Januari hadi Juni yamefunguliwa mashauri 426 Mahakama Kuu na mashauri 546 yalishatolewa maamuzi. Kwa mtazamo huo, Mhe. Moshi aliwapongeza Majaji, Mahakimu na watumishi wote kwa utendaji kazi mzuri.

Naye Mtendaji wa Mahakama Kanda, Bw. Festo Chonya alisema katika mwaka wa fedha 2022/2023 yamefanyika mambo mengi ya kujivunia, ikiwemo upatikanaji wa hati sita za viwanja vya Mahakama, kuimarisha ushirikiano kati ya watumishi na viongozi na ushirikiano kati ya Mahakama na Taasisi nyingine.

Kadhalika, Bw. Chonya alieleza uwepo wa maboresho ya Mahakama, hasa katika Mahakama za Mwanzo Kenkombyo, Musoma Mjini na Kiagata, utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti zaidi ya 10,000 katika Mahakama mbalimbali zilizoko ndani ya Kanda na mambo mengine mengi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe Fahamu Mtulya akisisitiza jambo wakati wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma kilichofanyika wilayani Serengeti hivi karibuni.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Moshi akitoa tathmini ya hali ya usikilizwaji wa mashauri katika Kikao cha Menejimenti.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Festo Chonya akielezea mafanikio yaliyopatikana upande wa utawala katika kikao cha menejimenti.

Wajumbe wa kikao wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (aliyenyoosha mkono) akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Butiama, Mhe. Judith Semkiwa akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama ya Wilaya na taarifa ya Mahakama ya Mwanzo Butiama.

Wajumbe wa kikao cha menejimenti wakifurahia uwasilishaji wa taarifa kutoka kwa Afisa Tawala Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Bw. Ezekia Kaduma (aliyesimama).

Wajumbe wa kikao wakifuatilia kwa makini taarifa ya maboresho ya Mahakama za Mwanzo iliyowasilishwa na Afisa Tawala wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Kandana Lucas.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe Fahamu Mtulya (katikati mstari wa kwanza) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao cha menejimenti, Kanda ya Musoma.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni