Ijumaa, 4 Agosti 2023

MKUU WA CHUO CHA IJA AWAPA NENO WATAALAMU MFUMO WA KUJIFUNZIA MTANDAONI

 Na Yusufu Ahmadi- Mahakama IJA

 

Mkuu wa Chuo cha (IJA) awapa neno Wataalamu na Maafisa Mfumo wa kujifunza mtandaoni

 

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe.Dkt. Paul F. Kihwelo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, amefanya mazungumzo na timu ya Wataalamu  inayofanya kazi ya ujenzi wa Mfumo wa kujifunzia kwa njia ya mtandao (E-learning Platform).

 

Mhe. Dkt. Kihwelo amezungumza na timu hiyo wakati  alipoitembelea tarehe 03 Agosti, 2023 katika kikao maalumu kinachofanyika kwenye ukumbi wa Mhe. Mohamed Chande Othman uliopo hapa Chuoni wilayani Lushoto mkoani Tanga.

 

Timu hiyo inahusisha wataalamu kutoka Mahakama ya Tanzania, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo).

 

Akizungumza na timu hiyo Mhe. Dkt. Kihwelo amesema kuwa Mahakama ya Tanzania na Chuo vina matarajio makubwa na wataalamu hao katika kufanikisha ujenzi wa mfumo huo, kwani unawawezesha watu kupata maarifa bila kujali sehemu waliyopo, kwa njia rahisi na kwa gharama nafuu zaidi.

 

Pia Mhe. Dkt. Kihwelo ameongeza kuwa Mahakama ya Tanzania kwa sasa imejikita katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na hivyo ujenzi wa mfumo huo unakuja kwa wakati sahihi huku akibainisha kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekuwa akisisitizia sana kwenye eneo hilo la kujifunza kwa njia ya mtandao. 

 

Aidha amesema kuwa Chuo hicho, kitahakikisha kazi hiyo inafanikiwa kama ilivyokusudiwa.


Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu amesema kuwa kikao hicho kinaendelea vema na kazi hiyo ya ujenzi wa Mfumo wa kujifunza kwa njia ya mtandao na kwamba wana matarajio kazi itakamilika ndani ya muda uliopangwa.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Kurugenzi ya TEHAMA, Mahakama ya Tanzania Bw. Allan Machella amebainisha kuwa kazi hiyo ni ya siku 60 na kwamba maafisa hao wanaendelea kubadilishana uzoefu katika eneo hilo.

 

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo(aliyekaa mbele mwenye suti nyeusi) akiwasikiliza  Wataalamu wanaofanya kazi ya ujenzi wa Mfumo wa kujifunzia kwa njia ya mtandao (E-learning Platform). Kulia mwa Mhe. Dkt. Kihwelo ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu. 

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Teknolojia ya habari na Mawasiliano (Tehama) Mahakama ya Tanzania Bw. Allan Machella(katikati) akifafanua jambo mbele ya Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA)(hayupo picha) kuhusu ujenzi wa Mfumo wa kujifunzia kwa njia ya Mtandao(E-learning).

Kulia ni Hakimu Mkazi na Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda.

 

 

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo akizungumza na Wataalamu wanaofanya kazi ya ujenzi wa Mfumo wa kujifunzia kwa njia ya mtandao (E-learning Platform) alipowatembelea Chuo cha IJA Lushoto. 

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo(kulia) akiwasikiliza  Wataalamu wanaofanya kazi ya ujenzi wa mfumo wa kujifunzia kwa njia ya mtandao (E-learning Platform). Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu.

Baadhi ya  Wataalamu wanaofanya kazi ya ujenzi wa Mfumo wa kujifunzia kwa njia ya mtandao (E-learning Platform) wakiwa katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA cha Chuo cha Serikali za Mitaa(Hombolo) Mhandisi Emmannuel Mbosso, Afisa TEHAMA wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Bw.Kimaro na Afisa TEHAMA wa IJA, Bi. Elizabeth Mbiu.

                             (Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni