Na Faustine Kapama-Mahakama
Mwenyekiti wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama
Sports) Wilson Dede amewataka wanamichezo wote kuanza kufanya mazoezi ili
kujiandaa na mashindano yajao ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za
Serikali (SHIMIWI) yanayotarajia kufanyika kitaifa mkoani Iringa mwaka huu wa
2023.
Katika taarifa yake aliyoitoa juzi jioni kwa wanaichezo
wote katika Mahakama zote nchini, Dede amesema mazoezi rasmi katika michezo
mbalimbali yanatakiwa kuanza mara moja ili kujiwinda na mchaka mchaka wa
mashindano hayo, ambayo yanatarajia kuanza tarehe 27 Septemba, 2023 hadi tarehe
14 Octoba, 2023.
“Kuanzia tarehe 17 Julai, 2023 hadi tarehe 31 Julai, 2023
tutafanya mazoezi mara tatu kwa wiki, yaani Jumatatu, Jumatano na Ijumaa. Ifikapo
tarehe 01 Agosti, 2023 tutafanya mazoezi kila siku za kazi kuanzia Jumatatu
hadi Ijumaa,” Dede ameeleza kwenye taarifa yake.
Tayari viongozi wa Mahakama Sports wameshaenda mkoani
Iringa kukagua na kutembelea maeneo mbalimbali watakayokuwa wanayatumia wakiwa
kwenye mashindano hayo, ikiwemo sehemu nzuri ya malazi, chakula na viwanja vya
kufanyia mazoezi.
“Hivyo basi nawaomba wanamichezo wa Mahakama Mikoa
yote tujitokeze kwa pamoja na kushiriki katika mazoezi ya kuandaa timu yetu. Upatapo
taarifa hii mjulishe na mwenzako. Asanteni, nawatakia maandalizi mema,” Mweyekiti
Dede anahitimisha kwenye taarifa hiyo.
Michezo ambayo Mahakama Sports inatarajia kushiriki ni
Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata,
Tufe, Riadha Wanaume na Wanawake pamoja na Baiskeli. Taarifa kamili kuhusu
ushiriki katika michizo hiyo itatolewa baadaye.
Katika mashindano ya SHIMIWI
yaliyofanyika mwaka jana jijini Tanga, timu ya Mahakama ya Tanzania ilizoa
makombe saba baada ya kuibuka washindi katika michezo mbalimbali.
Michezo ambayo Mahakama
Sports ilipata medali na makombe ni Kamba Wanawake walioibuka mshindi wa
kwanza, Riadha Wanawake mita 3,000 mshindi wa kwanza, Tufe Wanawake mshindi wa
kwanza, Kamba Wanaume walioshika nafasi ta pili, Mpira wa Miguu Wanaume
walioshika nafasi ya pili na Bao Wanaume mshindi wa tatu.
Anakufa mtu safari hii.
Mzigo huu hapa, lazima urudi wote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni