Ijumaa, 21 Julai 2023

JAJI MKUU AZINDUA KLINIKI YA MSAADA WA SHERIA CHUO KIKUU TUMAINI

·Ahimiza matumizi ya teknolojia katika utoaji huduma

Na Faustine Kapama-Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 21 Julai, 2023 amezindua Kliniki ya Msaada wa Sheria Chuo Kikuu Kishiriki Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO) na kuhimiza Wanafunzi wa Sheria kutumia teknolojia ya kisasa katika kuwahudimia wananchi.

Mhe. Prof, Juma amesema kuwa Wanafunzi wa Sheria watakapokuwa wanatumia teknolojia kutoa msaada wa kisheria watakuwa wakati huo huo wanajijengea pia uwezo na ujuzi wa kutumia teknolojia za kisasa katika shughuli za kisheria, ujuzi ambao utawasaidia baada ya kuhitimu Shahada ya Sheria.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuwakumbusha Wanafunzi wa Shahada ya Sheria kuwa Kliniki ya Msaada wa Kisheria ni darasa, sio tu la kuwawezesha kuangalia misuguano katika maisha ya kila siku, bali pia kujifunza matumizi ya teknolojia, sheria na taratibu za kimahakama kutatua migogoro ya wananchi,” amesema.

Jaji Mkuu amesisitiza kuwa Kliniki ya Msaada wa Kisheria itumie teknolojia ya kisasa kuwasaidia wasio na uwezo kutayarisha nyaraka za kusajili mashauri mahakamani.

Ameuomba uongozi wa Chuo hicho kutafuta teknolojia itakayosaidia kuongeza wigo wa huduma za kisheria, huku njia zitakazotumika kutoa huduma katika Kliniki hiyo kutokuegemea kutoa ushauri kwa kukutana uso kwa uso pekee yake.

“Teknolojia iwasaidie kuwasikiliza na kutoa huduma kwa wananchi walio mbali ili nao wapate huduma za ushauri wakiwa huko walipo, kwa wakati wowote na waweze kuuliza na kujibiwa maswali wakati wowote kupitia teknolojia,” amesema.

Jaji Mkuu ameupongeza uongozi wa Chuo, chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi TUDARCO na Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Baba Askofu, Dkt. Alex Malasusa, wanataaluma na wafanyakazi wote kwa kuamua kuanzisha Kituo hicho kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.

Mhe. Prof. Juma ameahidi kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kufuatilia ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwa Kliniki hiyo yanatimia kama ilivyotarajiwa.

Akizungumza katika halfa hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo, amesema uwepo wa Kliniki nyingi za msaada wa kisheria ni faraja kwani Serikali ilitunga Sheria ya Msaada wa Kisheria kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania hapotezi haki yake kwa kuwa hana uwezo wa kugharamia huduma ya sheria.

“Niliposema Kliniki hii ni faraja kwetu nilikuwa na maana kuwa vituo vya aina hii tunavihitaji vingi ili kuendeleza kutoa msaada wa kisheria na kuwakilisha Watanzania wengi wasio na uwezo katika vyombo vya utoaji haki (Mahakama na Mabaraza) ...

“.... kwa Mikoa mitatu tuliyopita tumebaini Watanzania wengi wanahitaji huduma hii adhimu. Nichukue nafasi hii kusihi Kituo hiki cha Msaada wa Kisheria ambacho tumekisajiri wizarani kwetu kuongeza wigo wa utoaji huduma hususan katika maeneo ya vijijini,” amesema.

Katibu Mkuu alisema pia kuwa Kliniki hiyo na vituo vingine vyote na watoa msaada wa kisheria wote kushirikiana na Wizara katika kutekeleza kampeni kubwa inayoitwa ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’ katika Mikoa yote nchini ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Awali, akielezea kuhusu Kliniki hiyo, Naibu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Prof. Andrew Mollel alisema kuwa majukumu ya msingi ya Chuo Kikuu yamegawanyika katika sehemu kuu tatu, zikiwemo ufundishaji na ujifunzaji, utafiti na ubunifu na huduma na ushauri wa huduma ya jamii inayokizunguka chuo.

Amesema kuanzishwa kwa Kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu la tatu la Chuo Kikuu la kutoa huduma kwa wanajamii wanaokizunguka chuo walioko karibu na wale walioko mbali.

Prof, Mollel ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria, Legal Aid Act, Cap 21, 2016, Kliniki za Msaada wa Kisheria zinakusudiwa kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa mashauri ya jinai na madai kwa watu wasio na uwezo wa kumudu gharama za huduma hizo kwa malipo.

Amesema upatikanaji wa haki na kwa wakati ni moja wapo katika haki za msingi za binadamu yoyote na kwa mujibu wa Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu ni moja ya haki muhimu.

“Hata hivyo, ni ukweli usiofichika kwamba wananchi wengi hukosa haki hiyo ya kusikilizwa kikamilifu kwa sababu tu ya kutokujua taratibu za kufuata na pia kukosa uwezo wa kifedha kulipa gharama za huduma za kisheria,” Naibu Mkuu wa Chuo amesema.

Amebainisha kuwa Kituo cha Msaada wa Kisheria TUDARCO kimeanzishwa kwa lengo kuu la kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi, hasa wenye kipato cha chini na ambao hawawezi kumudu gharama za huduma za kisheria kwa malipo.

Prof. Mollel ametaja huduma zinazotolewa katika Kituo hicho kama kutoa elimu ya sheria kwa wananchi, kutoa ushauri wa kisheria katika masuala mbalimbali ya kisheria yanayowakabili wananchi mmoja mmoja na makundi na kuandaa nyaraka mbalimbali zinazohitajika mahakamani.

Huduma zingine ni kuandaa majibizano ya kimahakama, kuwakilisha wananchi mahakamani pale itakapobidi kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Msaada wa Kisheria na kuongeza upatikanaji wa haki kwa kupitia utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, ikiwemo maridhiano, usuluhishi na upatanishi kwa mujibu wa sheria.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akikata utepe kuzindua Kliniki ya Msaada wa Sheria Chuo Kikuu Kishiriki Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO) leo tarehe 21 Julai, 2023. Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi TUDARCO na Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Baba Askofu, Dkt. Alex Malasusa (wa tatu kulia), Mkuu wa Chuo cha TUDARCO, Prof. Burton Mwamila (wa pili kushoto),  Naibu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Prof. Andrew Mollel ( wa pili kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo ( wa kwanza kushoto).
Mmoja wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO) akitoa maelezo kwa Jaji Mkuu wa Tanzania namna watakavyokuwa wanatoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akiwa na wenyeji wake ndani ya moja ya vyumba vya Kliniki hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo akizungumza na Wanafunzi wa Chuo pamoja na wananchi (hawapo katika picha) wakati wa uzinduzi wa Kliniki hiyo.

Naibu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Prof. Andrew Mollel akieleza jambo katika hafla hiyo.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Chuo Kikuu Kishiriki Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO) na Wakuu wa Majimbo. Wengine waliokaa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi TUDARCO na Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Baba Askofu, Dkt. Alex Malasusa (wa tatu kulia), Mkuu wa Chuo cha TUDARCO, Prof. Burton Mwamila (wa tatu kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo ( wa pili kulia), Naibu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Prof. Andrew Mollel ( wa pili kushoto), Msaidizi wa Askofu Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dean Chediel Lwiza na Mwakilishi wa Naibu Mkuu wa Chuo Utawala, Dkt. Abdiel Abayo.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Maandalizi.

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wanafunzi wa Chuo hicho (juu na chini).


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiongozwa na bendi ya Jeshi la Magereza kuondoka katika eneo lililokuwa limeandaliwa kwa ajili ya sherehe ya ufunguzi wa Kliniki hiyo baada ya uzinduzi. 





 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni