Na Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametaka wanafunzi wanaohitimu katika Shahada ya
Sheria kubadilika na kujitafutia maarifa mapya na ujuzi ili kujiongezea sifa
ziada za kuajirika kiushindani katika soko la ajira ndani na nje ya Tanzania.
Mhe. Prof. Juma ametoa
wito huo leo tarehe 21 Julai, 2023 katika hafla ya kuzindua Kliniki ya Msaada
wa Sheria Chuo Kikuu Kishiriki Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO).
Jaji Mkuu amesema kuwa matayarisho
ya Wanafunzi wa Shahada ya Sheria ya kuwa wataalamu wa sheria na kushindana
katika soko la ajira baada ya kuhitimu yaanzie katika Chuo kwa juhudi zao
binafsi za kutambua mabadiliko makubwa ya teknolojia yanayotokea kila siku.
“Mabadiliko haya
yanawataka wanafunzi kujisomea ziada na kujitafutia maarifa mapya, ujuzi na
uelewa zaidi wa yale yaliyomo katika mitaala, lengo liwe kujiongezea sifa ziada
za kuajirika kiushindani,” amesema.
Mhe. Prof. Juma ameeleza
kuwa baadhi ya Vyuo Vikuu nchini Marekani, Canada, Bara la Ulaya na Australia vimeanza
kusanifu upya mitaala kwa kuongeza masomo katika fani zingine, mfano biashara
na matumizi ya teknolojia na Akili Mnemba (Artificial Intelligence), kama
sehemu ya masomo ya Shahada ya Sheria.
“Mnayo nafasi nzuri sana
ya kujisomea na kujiongeza nje ya mitaala ya sheria. Kwa mfano, uwepo wa Shule
ya Masomo ya Biashara ni nafasi muhimu sana ya kuanza kufikiria kusanifu upya
mitaala ya Shahada ya Sheria ili mhitimu ajazwe pia ujuzi na umahiri wa fani ya
biashara ambayo itamuongezea uajirikaji wake,” amesema.
Jaji Mkuu amebanisha
kuwa ushindani wa nafasi za ajira ndani na nje ya Tanzania umefika katika hali
kuwa mhitimu wa Sheria bila kuwa na uwezo na ujuzi zaidi ya kutegemea masomo uliyosomea,
atashindwa kushindana katika dunia ambayo inahama kutoka utoaji wa huduma kwa
makaratasi kwa njia ya analojia hadi huduma zote kutolewa na kupatikana
kidijitali.
Amesema kuwa Wanafunzi
wanaosoma Sheria ni lazima wafahamu kuwa tayari yapo maeneo ambayo Wanasheria
wenye kutumia ‘Legal Tech’ wameonyesha uwezo mkubwa zaidi, ufanisi zaidi na
ubora shindani zaidi ya wale wanaotegemea elimu na ujuzi wa kawaida wanayopata
kutoka mitaala ya elimu ya Sheria.
“Mifano ya ushindani
ziada unaowezeshwa na ‘Legal Tech’ ni pamoja na kujiridhisha na hali ya
biashara au uwekezaji wa upande wa pili wa makubaliano, kusoma na kupitia
mikataba mingi au migumu au katika maeneo yanayohitaji utaalamu wa aina
mbalimbali, utafiti wa kisheria hususan unaohusisha nyaraka nyingi, sheria na
maamuzi mengi kwa wakati mmoja na kuchunguza na kufahamu ushahidi utakaotegemewa
na upande wa pili kabla ya shauri kuanza,” amesema.
Jaji Mkuu amesisitiza
kuwa eneo jipya katika elimu ya sheria “Legal Tech”ndiyo elimu ya Sheria Tanzania
inatakiwa kutumia kuwatayarisha wahitimu wa sheria kushiriki kiushindani kutoa
huduma kisheria katika eneo huru la biashara la Afrika.
“Wanafunzi wa Sheria ni
lazima watayarishwe sasa na leo ili waweze kutoa huduma katika Tanzania ya
Kidijitali, Mahakama ya Tanzania ya Kidijitali na Eneo Huru la Biashara
Kidijitali la Afrika,” amesema.
Aidha, Mhe. Prof. Juma
amebainisha kuwa leo na sio kesho, wanafunzi wa Sheria lazima wafahamu mwelekeo
na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhimili wa
Mahakama ya Tanzania kuhusu kutoa huduma za umma kwa njia ya kidijitali
itakayoendeshwa na matumizi makubwa ya teknolojia ya kisasa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi
ya Uongozi TUDARCO na Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Baba Askofu, Dkt. Alex Malasusa, akizungumza
kabla ya Jaji Mkuu kuzungunza katika hafla hiyo, alisema lengo la kuanzishwa kwa
Kituo cha Msaada wa Kisheria ni kutoa huduma za kisheria kwa Watanzania maskini
ambao hawawezi kumudu gharama za huduma za kisheria.
Amesema uanzishwaji wa
Kituo hicho unaenda sambamba na Mpango Mkakati wa Chuo wa miaka mitano
(2020-2025) katika kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ya Watanzania, hasa wale wanaokizunguka
Chuo.
“Hivyo ni matumaini yangu
kuwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na hasa maeneo yanayotuzunguka na mengine
nchini watatumia fursa hii kupata huduma za kisheria na kutatua changamoto za
kisheria zinazowakabili,” amesema.
Amemhakikishia Jaji Mkuu
kuwa Bodi ya Uongozi ya TUDARCO kwa kushirikiana na menejimenti ya Chuo
watasimamia Kituo hicho kwa dhati ili kuhakikisha kinatoa huduma iliyo bora na
bure kwa wateja wake ambao ni wahitaji.
Awali, akizungumza
katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo cha TUDARCO, Prof. Buton Mwamila alimweleza
Jaji Mkuu kuwa uwepo wa Kituo cha Msaada wa Kisheria chuoni utakuwa ni sehemu
muhimu ya Wanafunzi kujifunza kwa vitendo yale wanayosoma darasani kuhusiana na
utoaji wa huduma kwa jamii.
Prof. Mwamila amesema
kuwa kuzinduliwa kwa Kituo hicho ni uthibitisho wa dhamira ya Chuo wa kukuza
mwitikio na uwajibikaji wake kwa jamii.
Amesema kuwa ili
kuhakikisha ubora wa ufanisi katika utoaji wa msaada wa kisheria katika Kituo hicho,
uongozi wa Chuo utajitahidi kuhakikisha kuwa msaada huo wa kisheria unatolewa
na watu wenye sifa na uwezo unaotakiwa kwa mujibu wa Sheria na taratibu za nchi
na miongozo ya Chuo.
“Uwepo wa Kituo cha Msaada
wa Kisheria utatoa fursa kwa wananchi kunufaika na uwekezaji mkubwa wa rasilimali
watu iliyopo hapa chuoni. Hivyo, natoa wito kwa jamii na kuwakaribisha kutumia Kituo
hiki ili kuweza kupatiwa msaada wa kisheria na wataalam wetu,” amesema.
Jaji Mkuu aliwasili
katika maeneo ya Chuo cha TUDARCO majira ya saa 4.30 asubuhi na kupokelewa na
uongozi wa Chuo kabla ya kukaribishwa ofisini kusaini kwenye kitabu cha wageni.
Baadaye, Jaji Mkuu akiwa ameongozana na wenyeji wake alisindikizwa na bendi ya Jeshi la Magereza kutoka ofisini kwa Mkuu wa Chuo kuelekea kwenye jukwaa kuu ili kuendelea na hafla ya uzinduzi wa Kituo hicho.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anazungumza kwenye hafla ya kuzindua Kliniki ya Msaada wa Sheria Chuo Kikuu Kishiriki Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO) leo tarehe 21 Julai, 2023.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni