Jumatatu, 24 Julai 2023

JAJI MAHIMBALI AAGWA MAHAKAMA MUSOMA

Na. Francisca Swai – Mahakama Musoma.

Watumishi na viongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, hivi karibuni walifanya tafrija fupi kumuaga Mhe. Frank Mahimbali, ambaye ameteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga.

Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Mahimbali alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma ambaye amehudumu kwa kipindi cha miaka miwili.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mahimbali aliwashukuru viongozi na watumishi kwa ushirikiano waliomuonesha wakati wote alipokuwa Musoma. 

Aliwaasa kuendeleza utamaduni mzuri uliopo wa upendo, ushirikiano, umoja na pia kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili kuleta tija katika kazi zao na kwa mteja wanayemhudumia.

Naye Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya alimshukuru Jaji Mahimbali kwa moyo wake wa upendo, majitolea na ushirikiano mkubwa aliouonesha kwa watumishi na wadau katika kazi za kila siku. 

Hafla hiyo fupi ilihudhuriwa na viongozi, watumishi na wadau mbalimbali wa Mahakama ambao walipata nafasi ya kutoa maneno ya shukrani, kutakiana heri, zawadi mbalimbali na kufurahi pamoja.


Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya (wa kwanza kushoto), Jaji Marlin Komba (wa kwanza kulia) pamoja na Mhe. Frank Mahimbali (katikati) wakitakia heri na afya njema kwa kukonga glasi zao kwa furaha.

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akifurahi pamoja na watumishi na wadau wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma katika zoezi la kutakiana heri na afya njema (cheers).

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi waliokuwa wakihudumia katika chemba yake alipokuwa Mahakama Kuu Musoma.

Viongozi na sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu Musoma waliofanya kazi na Mhe. Frank Mahimbali wakiwa katika picha ya pamoja.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Festo Chonya (aliyeshika kipaza sauti) akizielezea zawadi mbalimbali zilizotolewa kwa Mhe. Mahimbali na watumishi wa Mahakama Kuu Musoma kama ishara ya upendo na ukumbusho kwake.

Moja ya zawadi alizokabidhiwa Mhe. Mahimbali katika hafla hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya akisema neno la shukrani na kwaheri kwa Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (hayuko pichani).

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali (aliyesimama) akisema neno la shukrani na kuwaaga watumishi na wadau wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni