Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Hakimu Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi amewataka Wasaidizi
wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya Mkoa wa Pwani kutumia
muda wao kujifunza zaidi mifumo yote ya kimahakama ili kuendana na Mpango
Mkakati wa Mahakama.
Mhe. Mkhoi alitoa
wito huo mwishoni mwa wiki alipokua akifungua mafunzo kwa Wasaidizi wa
Kumbukumbu wa Mahakama za Wilaya na Mkoa huo katika ukumbi namba mbili wa Mahakama
ya Wazi.
Alieleza kuwa kwa
sasa Mahakama ya Tanzania inatekeleza mpango mkakati wake wa 2020/2021-2024/25
ambapo moja ya malengo yake makuu ni kuhakikisha na kurahisisha huduma za
kimahakama ziwe karibu zaidi na wananchi.
Akiongea kuhusu
malipo ya mirathi, Mhe. Mkhoi alisema ni muhimu pia Wahasibu kuzingatia viambatanisho
muhimu katika kuhakikisha fedha za warithi
zinatoka kwa wakati na kuingia kwenye akaunti zao kama
zilivyoorodheshwa bila makosa
yoyote ili kuwaepusha kukosa haki zao,
hatua ambayo itapunguza malalamiko.
Naye Mkufunzi wa
mafunzo hayo, Hakimu Mkazi Manfred Sanga kutoka Kituo Jumuishi Temeke amewataka
wasaidizi wa kumbukumbu kukagua nyaraka za kufungua mirathi na kujiridhisha kkama
ziko sahihi kabla ya kufungua ili kuepuka usumbufu utakaojitokeza baada ya
kumalizika kwa shauri.
Amewataka hasa Wasaidizi
wa Kumbukumbu wa Mahakama za Mwanzo kufanya kazi hizo kwa weledi maana wao ni
kama Mawakili wa waombaji na kuwataka kujaza fomu kwa ufasaha zaidi.
“Fomu zotekatika Mahakama
za Mwanzo zinajazwa na Wasaidizi wa Kumbukumbu, hivyo kuwezi makini katika
ujazaji wa fomu hizo maana nyie ni kama mawakili wa waombaji,” alisema.
Naye mratibu wa
mafunzo hayo, Afisa Tawala wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Bi, Stumai Hozza alisema
mafunzo hayo ni mwanzo wa mafunzo zaidi yatakayotolewa na mahakama Pwani katika
kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma katika mahakama hiyo.
Mafunzo hayo ya
siku mbili yalilenga kuwajengea uwezo Wasaidizi wa Kumbukumbu 25 kuhusu mfumo
wa usajili wa mshauri (JSDS) na mfumo wa E-office pamoja na ufunguaji wa kesi
za mirathi.
Hakimu Mkazi katika Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Manfred Sanga akisistiza jambo wakati wa mafunzo hayo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni