·Mwenyeji wake Mustapher Siyani atoa ujumbe muhimu
Na.
Faustine Kapama-Mahakama na Sade Soka- UDSM
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Uganda, Mhe.
Dkt. Flavian Zeija, amesema ushirikiano uliopo kati ya Mahakama ya Uganda na
Tanzania unapaswa kuendelea ili kukuza na kuimarisha malengo ya pamoja katika kutoa
haki kwa wananchi.
Akizungumza katika siku ya pili ya ziara yake
ya Mahakama nchini Tanzania baada ya kukutana na mwenyeji wake, Jaji Kiongozi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Mhe. Dk. Zeije amesema
kuna mengi ya kushirikiana kati ya Mahakama hizo mbili.
"Nawakaribisha katika nchi yetu, hizi ni
nchi mbili za kidugu, kuna mengi ambayo tunaweza kushirikiana. Asanteni sana,
tuendeleze uhusiano wetu," amesema.
Jaji Kiongozi wa Uganda ambaye amefuatana na
Katibu Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Dk. Pius Biligimana, ameshukuru kwa ukarimu
alioupata kutoka kwa wenyeji wake tangu alipowasili nchini jana tarehe 15
Agosti, 2023.
"Tutalipiza kisasi ukifika Uganda,"
amesema na kuibua vicheko kutoka kwa viongozi mbalimbali waliohudhuria ugeni
huo. Mhe. Dkt. Zeija alitoa shukrani zake kwa kupata fursa ya kutembelea
Mahakama ya Tanzania ili kujifunza masuala mbalimbali ya kimahakama yaliyopo.
Amebainisha kuwa waliwahi kuja Tanzania mwaka
mmoja nyuma na walipelekwa katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, lakini
walipofika huko walishangaa kwani walichokiona ukulinganisha na Taasisi yao waligundua
ipo sawa na jiko.
“Tuligundua kuwa Tanzania ina mambo mengi ya
kutuonyesha na, kwa kweli tulipotoka huko tulikwenda kupata eneo la hekta 20
kama lile tuliloliona Lushoto. Kwa hivyo, unaweza kuona kuna mengi tunajifunza
kutoka Tanzania,” Jaji Kiongozi wa Uganda amesema.
Akizungumza baada ya kumpokea mgeni wake,
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliwakaribisha viongozi hao wawili wa
Uganda na kusema ziara yao ina umuhimu wa kipekee, yenye dhamira ya usawa na ya
pamoja ya Mahakama hizo mbili katika kukuza ushirikiano na kujifunza kwa
pamoja.
Aliwashukuru wageni wake kwa nia
waliyoionesha, hasa katika mikakati ya Mahakama ya Tanzania ya kuendeleza
miundombinu ya Mahakama katika kushughulikia ipasavyo ucheleweshaji wa mashauri
na mlundikano.
Alidokeza kuwa ziara hiyo ni muhimu, kwani
watabadilishana maarifa na ujuzi ili kuendeleza malengo ya pamoja ya Mahakama
hizo mbili.
"Tunashuhudia utimilifu wa nia yenu ya
kurudi na kuzama zaidi katika yale tunayofanya. Tunathamini sana uwepo wenu na
fursa ya ushirikiano kati ya Mahakama zetu mbili,” Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania alisema.
Jaji Kiongozi wa Uganda yuko nchini Tanzania
kwa ziara ya siku tano ya kikazi. Kwa mujibu wa ratiba iliyopo, leo pia ameenda
kutembelea Kituo Jumushi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia Temeke jijini
Dar es Salaam na pia kujionea jinsi Mahakama inayotembea (Mobile Court)
inavyofanya kazi.
Pia anatarajiwa kuondoka kesho kuelekea
Dodoma kutembelea jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma kabla ya
kurejea jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa kwa ajili ya masuala mengine ya kimahakama
katika ziara yake.
Hii ni mara ya pili kwa viongozi wakuu wa
Mahakama Uganda kuitembelea Mahakama ya Tanzania. Ziara ya kwanza ilifanywa na
Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo tarehe 24 Mei 2022 kwa lengo
la kubadilishana uzoefu wa mambo mbalimbali.
Mhe Owiny-Dollo alikutana na mwenyeji
wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake jijini
Dar es Salaam na baada ya maongezi mafupi yenye lengo la kujenga ushirikiano
katika masuala mbalimbali ya kimahakama alielekea Tanga kutembelea Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Akiwa Lushoto, Jaji Mkuu Uganda na ujumbe
wake alitapata fursa ya kubadilishana uzoefu na viongozi wa Chuo hicho, ikiwemo
namna kinavyofanya kazi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto) akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Dk.Pius Biligimana.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto)
na mgeni wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Uganda, Mhe. Dkt.Flavian Zeija
(wote waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto)
na mgeni wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Uganda, Mhe. Flavian Zeija
(wote waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama,
Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto), Katibu Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Dkt .Pius
Biligimana (katikati) na Msajili Mkuu, Mhe. Wilbert Chuma.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto)
na mgeni wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Uganda, Mhe. Dk. Flavian Zeija
(wote waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wengine waandamizi wa Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni