Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija amekitembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke-Dar es Salaam ambapo amepongeza utendaji kazi mzuri pamoja na uzuri wa jengo hilo.
Akizungumza mara baada ya ziara yake fupi katika Mahakama hiyo aliyofanya leo tarehe 16 Agosti, 2023, Mhe. Dkt. Zeija amesema amefurahishwa na mpangilio wa utendaji kazi wa Mahakama hiyo na kusema kuwa, ni mfano mzuri wa kuigwa.
“Hakika nimestaajabishwa na uzuri wa jengo hili, namna ambavyo limejengwa na kupangiliwa ama kwa hakika hiki ni kitu kizuri ambacho kupitia ziara hii tunakichukua kwa ajili ya kuangalia namna ya kuwa na majengo kama haya kwa Mahakama yetu,” amesema Jaji Kiongozi huyo.
Ameongeza kuwa, amevutiwa na jinsi ambavyo Mahakama hiyo inavyohudumia wananchi kupitia matangazo mbalimbali yanatolewa kuwaelekeza wateja wanachotakiwa kufanya ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Mahakama kujua kama wananchi wanaridhishwa na huduma zinazotolewa na Kituo hicho.
Mhe. Dkt. Zeija amesema kwamba, Mahakama ya Tanzania imepiga hatua hususani katika miundombinu ya majengo yake na kuongeza kuwa, ziara yao ya kujifunza imekuwa ya manufaa na wamepata mengi ya kujifunza na kuyapeleka Mahakama ya Uganda.
Jaji Kiongozi huyo aliyeambatana na Katibu Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Mhe. Pius Bigirimana walipata nafasi ya kutembezwa katika maeneo mbalimbali ya jengo hilo na mwenyeji wao Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.
Kadhalika Mhe. Zeija amepata fursa pia ya kutembelea na kujionea huduma zinazotolewa katika Mahakama Inayotembea ‘Mobile Court’ iliyokuwa ikitoa huduma zake katika eneo la Buza jijini Dar es Salaam.
Aidha; katika mwendelezo wa ziara yake ya siku tano nchini, Mhe. Zeija anatarajia pia kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na pia kujionea jengo jipya la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania lililopo mkoani humo.
Hii ni mara ya pili kwa Viongozi Wakuu wa Mahakama ya Uganda kuitembelea Mahakama ya Tanzania. Ziara ya kwanza ilifanywa na Jaji Mkuu wa Nchi hiyo, Mhe. Alfonse Chigamoy Owiny-Dollo tarehe 24 Mei 2022 lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu wa mambo mbalimbali.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (wa pili kushoto) akikagua jengo la Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC)-Temeke, Dar es Salaam leo tarehe 16 Agosti, 2023. Kushoto kwake ni Mwenyeji wake Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (aliyevaa ushungi), wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Mhe. Pius Bigirimana, nyuma ya Jaji Mfawidhi ni Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, aliyesimama kulia ni Naibu Msajili Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Martha Mpaze.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kushoto) akifurahia jambo wakati alipokuwa katika moja ya Kumbi za Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, katikati ni Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, kulia ni Katibu Mkuu Mahakama ya Uganda, Mhe. Pius Bigirimana na kulia kwake ni Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.
Naibu Msajili Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Martha Mpaze (kulia) akizungumza jambo wakati Viongozi hao kutoka Uganda walipotembelea Kituo hicho leo tarehe 16 Agosti, 2023. Katikati ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, kushoto ni Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwani na kulia ni Katibu Mkuu wa Mahakama ya Uganda, Mhe. Pius Bigirimana.
Afisa TEHAMA Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Bi. Amina Ahmad akiwasilisha mada kuhusu Kituo hicho kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija alipotembelea 'IJC' Temeke leo tarehe 16 Agosti, 2023.
Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (kulia) pamoja na Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kushoto) wakifuatilia wasilisho kuhusu 'IJC' Temeke lililokuwa likitolewa kwa Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija alipotembelea Kituo hicho leo tarehe 16 Agosti, 2023.
Sehemu ya Watendaji, Naibu Wasajili na watumishi wengine wa Mahakama wakifuatilia wasilisho lililokuwa likitolewa na Bi. Amina Ahmad (hayupo katika picha) wakati wa ziara ya Jaji Kiongozi Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (hayupo katika picha).
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (wa kwanza kulia) akizungumza jambo na Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa (aliyeketi mbele) pamoja na sehemu ya Maafisa wengine kutoka Mahakama ya Tanzania.
Ukaguzi ukiendelea.. ndani ya chumba cha Jaji cha kusikilizia mashauri (Judge's Chamber).
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kushoto mwenye tai ya bluu) akipata maelezo kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Watoto Temeke, Mhe. Vicky Mwaikambo (kulia).
Ukaguzi katika chumba cha kunyonyeshea watoto (breast feeding room).
Jaji Kiongozi wa Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Ustawi wa Jamii anayehudumu katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia- Temeke.
Picha ya pamoja baada ya ziara. Katikati ni Jaji Kiongozi Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC)-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa, wa pili kulia ni Katibu Mkuu Mahakama ya Uganda, Mhe. Pius Bigirimana, wa kwanza kulia ni Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na wa kwanza kushoto ni Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni