Na. James Kapele – Gauteng Johannesburg
Mahakama ya Tanzania
inashiriki Mkutano wa 27 wa Baraza la Nyaraka la Kimataifa la Kanda ya
Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika (Eastern and Southern Africa Regional
Branch of International Council on Archives -ESARBICA) ambalo linawaleta pamoja
wataalamu wa kumbukumbu na nyaraka jijini hapa, Afrika ya Kusini.
Mkutano huo ulifungungiliwa
na Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika ya Kusini, Mhe, Nocawe Mafu ambaye, pamoja na
mambo mengine, amewataka washiriki na wanachama kujadili kwa mapana maudhui ya
mkutanao huo“Archives, Records and Memory in Digital spaces and global chaos.”
Alisema kuwa washiriki
wanapaswa kuja na mapendekezo mahsusi yatakayochochea maboresho chanya katika
utunzaji na uhifadhi wa nyaraka kwa ustawi wa vizazi vijavyo.
Aidha, Mhe. Mafu alisisitiza
washiriki katika yale watakayojadili kukumbuka sehemu muhimu ya kutunza historia
kwa vizazi vijavyo katika eneo la utunzaji kumbukumbu na nyaraka, hasa kwa kuzingatia
kukuwa kwa TEHAMA.
“Katika kipindi hiki mapinduzi
ya viwanda na maendeleo makubwa ya TEHAMA lazima yaende sambamba na mbinu
mbadala za utunzaji, uhifadhi na utumiaji wa nyaraka na kumbukumbuku zetu
katika mifumo ya kidigitali (digital spaces) kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema Naibu Waziri.
Awali, akimkaribisha
mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Nyaraka Afrika ya Kusini, Bi. Dr.
Cynthia Khumalo, amesema Afrika ya Kusini ni moja kati ya nchi wanachama katika
jukwaa hilo la ESARBICA na waliteuliwa na Bodi kuandaa Mkutano huo wa 27, huku jumla
ya washiriki 600 wakiwa wanatarajiwa kushiriki.
Akizungumza baada ya
ufunguzi wa Mkutano huo, Mkurugenzi wa Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo
Manyambula ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa kushiriki katika
Mkutano huo.
Alisema kuwa Mkutano huo ndiyo
jukwaa kubwa Barani Afrika ambalo nchi wanachama wanakutana kubadilishana
uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za kuboresha na kuimarisha mifumo ya
utunzaji wa kubukumbu na nyaraka za Mahakama.
Kwa upande wao, watumishi
wa Mahakama walioshiriki katika Mkutano huo wameishukuru Mahakama kwa kuona
umuhimu wa wao kushiriki katika jukwaa hilo la wahifadhi na watunza kumbukumbu
vijana.
Mkutano huo umetanguliwa
na semina ya siku mbili kwa watunza kumbukumbu na nyaraka kwa vijana (Young
records and archives management professionals) kujadiliana masuala mbalimbali
ya utumiaji na utunzaji kumbukumbu na nyaraka.
Majadiliano hayo yaliyohusisha
ukusanyaji na utunzaji wa kumbukumbu kupitia simulizi (Oral history) na
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasilano (TEHAMA) ikiwemo mifumo ya
kidigitali.
Tanzania ni mwanachama wa
Baraza hilo lililoanzishwa mwaka 1969 kwa lengo la kushirikiana katika masuala
ya utumiaji na utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, likijumuisha jumla ya nchi wanachama
20 ambalo Makao Makuu yake yako nchini Botswana.
Washiriki wengine kutoka Tanzania ni Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firmin Msiyangi na watumishi wengine kutoka katika idara hiyo ambayo ndiyo taasisi simamizi ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika utumishi wa umma kwa Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Nyaraka Afrika ya Kusini, Bi. Dr. Cynthia Khumalo akitoa salamu za ufunguzi na kumkaribisha mgeni rasmi katika Mkutano huo.
Naibu Waziri wa
Michezo Sanaa na Utamaduni, Mhe. Nocawe Mafu akitoa hotuba ya ufunguzi wa
Mkutano wa 27 wa ESARBICA kwa washiriki wanaohudhuria Mkutano huo.
Sehemu ya washiriki katika Mkutano huo kutoka Mahakama ya Tanzania pamoja na watumishi kutoka Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Aliyesimama katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firmin Msiyangi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE
KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni