Na. Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Morogoro Mhe. Augustina Mmbando awahimiza wateja wa Mahakama walioteuliwa kuwa
wasimamizi wa Mirathi kwa Kanda ya Morogoro kufika katika Mahakama husika
zilizomaliza kusikiliza shauri hayo ili kufunga Mirathi hiyo kama utaratibu wa
kisheria unavyoelekeza.
Akitoa elimu ya sheria ya msingi kwa wateja wanaofika kupata huduma za Kimahakama ndani ya Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo Morogoro jana tarehe 15 Agosti, 2023, Mhe. Mmbando alisema kuwa kufunga mirathi ni jambo la msingi na linapaswa kutekelezwa na msimamizi wa Mirathi na kusisitiza mirathi inafungwa katika Mahakama iliyomaliza kusikiliza shauri hilo na sio mahali pengine.
“Wasimamizi wa mirathi wanapoacha kufunga mirathi ni chanzo cha migogoro na muendelezo wa kesi nyingi za mirathi jambo linalopoteza muda mwingi wa wananchi kutofanya shuguli za maendeleo kwa kusuluhisha migogoro na kuzalisha kesi za mara kwa mara, hivyo wanaweza kutatua sehemu ya changamoto hiyo kwa kufunga mirathi mara shauri linapotolewa maamuzi na taratibu zote kukamilika kwa wakati”, alisisitiza Mhe. Mmbando.
Aidha, Mhe. Mmbando aliwaomba Wasimamizi wa Mirathi waisaidie Mahakama kuwapata warithi wa mali za marehemu kwa wakati ili waweze kunufaika na mgao unaotolewa ikiwa ni sehemu ya mali za Marehemu hasa kwa upande wa fedha ambazo zinapitia kwenye Akaunti ya Mahakama ndipo ziweze kulipwa kwa warithi kwakuwa kumetokea changamoto ya pesa nyingi za Mirathi kukwama kwenye Akaunti za Mahakama kutokana na warithi kutofahamishwa taratibu sahihi zinazostahili na kushindwa kukamilisha vigezo ili waweze kulipwa mafao hayo.
“Wakati mwingine unakuta wale tegemezi wa marehemu wamekwama ada, chakula, makazi au matibabu wakati pesa zao za mirathi zipo kwenye akaunti ya Mahakama zikingojea msimamizi wa mirathi akamilishe taratibu ili pesa hizo zilipwe kwa wanufaika lakini masimamizi hafatilii, hii ni changamoto kubwa hivyo basi niwaombe wasimamizi kuonesha ushirikiano ili wanufaika wafikiwe na mirathi kwa wakati”, alifafanua Mhe. Mmbando.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro Mhe. Lameck Mwamkoa alifundisha somo la umiliki wa ardhi kwa kutaja hatua zinazoweza kufuatwa ili mtu atambulike kama mmiliki halali wa eneo husika.
Mhe. Mwamkoa aliwasisitiza wananchi kutatua migogoro ya ardhi kwa njia ya usuluhishi kwakuwa mara nyingi inatokea baina ya ndugu na pale inaposhindikana ndipo hatua za kisheria zifuatwe ili kumtambua mmiliki halali wa eneo husika.
Elimu hii ya mirathi na umiliki wa ardhi ilikuwa kivutio kwa wateja hao ambao walijitokeza kuchangia mawazo yao sanjari na kuuliza maswali mbalimbali ambayo yalitolewa ufafanuzi palepale huku wakiomba kuwa somo hilo lifundishwe ndani ya wiki nzima ili waweze kujifunza kwa kina zaidi wajibu na haki zao za msingi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni