Na Arapha Rusheke-Mahakama Kuu, Dodoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija leo
tarehe 17 Agosti, 2023 ametembelea Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.
Mara baada ya kuwasili katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania,
Jaji Kiongozi wa Uganda amepokelewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Elisante Ole Gabriel kisha akapata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za
kiutendaji zinazoendelea mahali hapo.
Mhe. Dkt. Zeija alikagua baadhi ya miundombinu na maeneo, ikiwemo
Ofisi za Viongozi na watumishi wa Mahakama katika jengo hilo.
Akiwa ofisini kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Jaji Kiongozi alipata
wasaa wa kupokea maelezo mafupi ya mradi wa ujenzi wa jengo hilo la Makao Makuu
ya Mahakama lenye thamani ya billioni 129 za Kitanzania ikiwa fedha kutoka
mapato ya ndani.
"Nakushuru sana Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt.
Flavian Zeija kwa kuja leo kututembelea, ujio wako ni faraja kwetu sisi
watumishi tunaotoa huduma katika jengo hili, ni matumaini yetu shughuli zote za
kiutendaji kwa watumishi wa Mahakama upande wa Makao Makuu zitaendelea
kushamiri," alisema Prof. Ole Gabriel.
Alisema matokeo ya ujenzi wa jengo hilo ni ushirikiano mzuri
uliopo katika ya mihimili mitatu ya Dola na kuongeza kuwa Serikali imekuwa
ikijitahidi kuhakikisha kuwa inatoa fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu
mbalimbali ya Mahakama ili kuwa na mazingira mazuri ya utoaji haki kwa
wananchi.
Kwa upande wake, Mhe. Dkt. Zeija amesema kwamba, Mahakama ya
Tanzania imepiga hatua hususani katika miundombinu ya majengo yake na kuongeza
kuwa, ziara yao ya kujifunza imekuwa ya manufaa kwani wamejifunza mengi ambayo
watayapeleka katika Mahakama yao ya Uganda.
Baada ya kutembelea Makao Makuu ya Mahakama, Jaji Kiongozi pia
alitembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma na kupokelewa na
mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe.
Dkt Juliana Massabo.
Akiwa katika Mahakama hiyo, Mhe. Dkt. Zeija alijionea shughuli za
baadhi ya wadau wa Mahakama na sehemu maalumu zilizotengwa, ikiwemo Mahakama ya
Watoto na Chumba cha kunyonyeshea Watoto, sehemu ya kuhifadhia mahabusu pamoja
na wafungwa wakiwa mahakamani kufuatilia mashauri yao.
Akiwa ofisini kwa Jaji Mfawidhi alipata taarifa mbalimbali,
ikiwemo ya ujenzi wa Jengo la IJC Dodoma pamoja na miundombinu katika Jengo
hilo.
Mhe. Dkt. Juliana alisema kukamilika kwa jengo hilo kunawasaidia
wadau wakiwemo wananchi kupunguza gharama wanapokuwa na mashauri yao mahakamani
kwani ndani ya IJC kuna ngazi sita tofauti kuanzia Mahakama ya Mwanzo, Mahakama
ya Wilaya, Mahakama ya Watoto, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na
masijala ndogo ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Alisema IJC inajumuisha ofisi na vyumba vya Majaji na Mahakimu,
kila Hakimu ana ofisi yake, vyumba ni 12 na Mahakama za wazi ni tano.
Mhe. Dkt. Juliana alisema mbali na ofisi za Majaji na Mahakimu,
zipo ofisi za wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Wanasheria Tanganyika, Ofisi ya
Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Magereza na Msaada
wa Kisheria.
Alisema uwepo wa IJC una manufaa ikiwemo kupunguza umbali kutoka
ngazi moja hadi nyingine, kupunguza gharama, mazingira mazuri ya kufanya kazi
miongoni mwa watumishi wa Mahakama.
Mhe. Dkt. Juliana alisema kuanzia Januari 2023 hadi jana tarehe 16
Agosti, 2023 takwimu za mashauri za Mahakama ndani ya IJC inaonyesha Masjala
ndogo ya Mahakama ya Rufani zilizofunguliwa zilikuwa 25, kesi zilizoamuliwa
hakuna na kesi 25 zinazoendelea.
Aliongeza kuwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Dodoma zilifunguliwa
kesi 597 na kuamuliwa 604 na zinazoendelea 761.
Mahakama ya Hakimu Mkazi zilifungua 52 na kuamuliwa 60 na kesi
zinazoendelea ni 31 na Mahakama ya Wilaya ya Dodoma zilifunguliwa ni kesi 641
na zilizotolewa maamuzi ni 666 na zinazoendelea ni 341.
Mhe.Dkt. Juliana alisema kwa upande wa Mahakama ya Watoto ya
Dodoma zilizofunguliwa zilikuwa kesi 73 na zilizoamuliwa ni 73 na zinazoendelea
ni 26 na Mahakama ya Mwanzo Dodoma mjini zilifunguliwa ni kesi 671 na kuamuliwa
kesi ni 503 na kesi 80 zinazoendelea.
Akizungumza mara baada ya ziara yake fupi katika Mahakama hiyo,
Mhe. Dkt. Zeija ameelezea kufurahishwa na mpangilio wa utendaji kazi wa
Mahakama hiyo na kusema kuwa, ni mfano mzuri wa kuigwa.
"Hakika nimependezwa na uzuri wa miundombinu ya jengo hili,
namna ambavyo limejengwa na kupangiliwa ama kwa hakika hiki ni kitu kizuri sana
nimejifunza mengi sana kupitia ziara hii," amesema Jaji Kiongozi huyo.
Mhe. Dkt Flavian Zeija aliambatana na viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt na Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni, Bi. Mary Shirima na Mtendaji Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Bw.Sumera Manoti na Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe.Silivia Lushasi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel
(aliyenyoosha mikono) akitoa ufafanunuzi kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kushoto) baada ya kutembelea Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 17 Augusti 2023, ikiwa ni ziara
yake ya kujifunza.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel
(aliyenyoosha mikono) akitoa maelezo kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda,
Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kushoto) baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya
jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Wengine katika
picha ni Msajili Mkuu wa Mahakama Mhe. Wilbert Chuma (wa pili kutoka kulia) na Msajili
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kulia).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kushoto)
akitoa maoni yake kwa baadhi ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania mara baada ya
kutembelea maeneo mbalimbali ya Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania
jijini Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (katikati)
akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania mara
baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya
Tanzania jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel (kushoto) akitoa ufafanunuzi kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda,
Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kulia) wakati akimuonyesha maeneo mbalimbali ya Jengo
la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 17 Augusti 2023.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kushoto)
akifurahi jambo na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel wakati ziara yake.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kulia)
akimuonyesha kitu Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante
Ole Gabriel (kushoto) wakati ziara yake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt
Juliana Massabo (kushoto) akiwa na mgeni wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kulia) wakati alipotembelea Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dodoma,
Mhe.Dkt Juliana Massabo (aliyenyoosha mkono) akitoa maelezo kwa mgeni wake,
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (mwenye suiti ya
kijivu).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe.Dkt. Flavian Zeija (kulia)
akiwa na mwenyeji wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Dodoma
Mhe. Dkt Juliana Massabo (kushoto) wakitazama michoro katika chumba maalumu cha
Mama kunyonyeshea katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (katikati)
akiwa na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Dodoma,
Mhe. Dkt Juliana Massabo (wa tatu kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja
na Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Wilbert Chuma (wa pili kutoka kulia), Msajili
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (wa pili kutoka kushoto)
na baadhi ya viongozi wa Menejimenti ya Kituo Jumuishi cha Utojai Haki Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (kulia) akiwa na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma Mhe. Dkt Juliana Massabo (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt. Flavian Zeija (katikati) akiwa na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Juliana Massabo (wa pili kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama Mhe. Wilbert Chuma (wa pili kutoka kulia), Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt (kushoto) na Naibu Msajili Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Silivia Lushasi.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni