Na Sade Soka – Mahakama(UDSM)
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza Mahakimu Wakazi wapya 38 walioapishwa kufuata sifa za mahakimu na kuzitunza katika kutoa maamuzi yao kama Hakimu ili kuzingatia Maadili ya Sheria.
Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki katika hafla ya uapisho wa mahakimu hao, iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, iliyopo jijini Dar es salaam.
“Inawezekana kabisa sifa uliyokuwa nayo ukaipoteza kwa sababu mbalimbali zikiwemo uvivu, pengine hata kuingia kwenye mambo ambayo hayaendani na maadili” amesema Mhe. Prof. Juma.
Aidha Mhe. Jaji Mkuu amewaasa mahakimu hao kuwa wajitambue kwamba wao ni watu muhimu kwa Mahakama kwa sababu uso wa Mahakama wa miaka 25 au 30 ijayo ni wao. Hivyo wao ndio kesho ya Mahakama kwa hiyo wasipoteze muda, waanze kujifunza namna inavyofanya kazi, inavyotoa maamuzi, sheria zote na miongozo yote ambayo inasimamia utoaji wa haki.
Mhe. Prof. Juma amewakumbusha kwamba kazi ya uhakimu inafanywa ndani ya Tanzania.
Hivyo wanawajibu wa kuhifahamu Tanzania na kuifahamu wanapaswa kujisomea masuala mbalimbali mbali na majalada ya mahakamani.
“Kanuni za Maadili za Maafisa Mahakama, 2020 hazihusu maadili peke yake. Zinahusu pia uwezo na bidii. Kanuni za Maadili zinawataka Mahakimu (na Maafisa wengine wa Mahakama, kuchukua hatua stahiki kudumisha na kuimarisha ujuzi, sifa na uwezo,” amesisitiza huku akiongeza kwamba wakipoteza ujuzi, sifa na uwezo watakuwa wanakiuka Kanuni za Maadili.
Mahakamu hao wameaswa kujisomea, kujiongeza, kujiendeleza kila siku, ikiwemo kujishindanisha na kujilinganishi na Mahakimu wengine nadni nan je ya nchi.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amesema mahakimu hao waliopita usaili ni 39, kati yao hao 10 wamebadilisha kada.
Mhe. Chuma amesema watapatiwa mafunzo ya semina elekezi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) kuanzia kesho tarehe 14-18 Agosti, 2023.Miongoni mwa mada watakazofundishwa ni maboresho yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania.
Sehemu ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni