Jumatatu, 14 Agosti 2023

MAHAKAMA KUU DODOMA YAFANYA KIKAO KAZI NA WADAU


Na Arapha Rusheke - Mahakama Kuu Dodoma

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo amefanya kikao kazi na wadau wake jijini Dodoma na kuwataka wajumbe wa kikao hicho, kutoa uzoefu wao ili kufanikisha kazi ya utoaji haki kwa wananchi na wadau.

 

Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao kazi hicho na wadau  ambacho kimefanyika tarehe 11 Agosti, 2023 katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma Mhe.Dkt Juliana Massabo alisema anawashukuru  kwa kukubali kuhudhuria.

 

Aidha aliongeza kuwa Mahakama hiyo hupokea mashauri mbalimbali ya jinai na madai kwa mamlaka yake ya awali, rufaa, mapitio na marejeo. Mashauri hayo huwa ama yamefunguliwa na/dhidi ya watu binafsi, serikali, mashirika/taasisi za umma, mamlaka ya serikali za mitaa, makampuni na mashirika binafsi n.k.

“Ni jukumu letu la kikatiba, kuyashughulikia mashauri hayo na kuyatatua kwa haki na kwa wakati.  Aidha, Mahakama inatambua kuwa, utekelezaji na ufanisi wa jukumu hili unahitaji ushirikiano wa karibu sana na wadau ambao ndio nguzo muhimu katika mafanikio yetu,” alisema Mhe. Jaji Dkt.  Juliana.

Aliwakumbusha wadau hao kuwa umuhimu wa ushirikiano huo, kama ulivyoelezwa katika ufunguzi wa Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau mkoani Arusha, uliofanyika tarehe 16 Aprili, 2021 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

“Ushirikishwaji wa wadau ni jambo muhimu na Mahakama inalizingatia hilo ili kuweza kutekeleza majukumu yake ya upatikanaji wa haki kwa urahisi”, alinukuu.

Mhe. Jaji Dkt. Juliana aliongeza kwamba katika muktadha huo Mahakama hiyo imekuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na wadau wake wa haki jinai na haki madai.

“Mara kwa mara tunafanya vikao na wadau wetu, vikao ambavyo hujulikana kwa jina maarufu la ‘vikao vya kusukuma mashauri,’alisisitiza.

Alifafanua kuwa   kupitia vikao hivyo, Mahakama na wadau hupitia mashauri kwa  kuanisha viini vya migogoro, changamoto za utatuzi wa migogoro hiyo na  pamoja hupanga na kutekeleza mipango mahususi ya kuondoa changamoto hizo. 

Hivyo Mahakama hiyo  na wadau wake wamekuwa wakijielekeza kuangalia umuhimu wa matumizi ya utatuzi wa migogoro kupitia njia mbadala za utatuzi wa migogoro kwa njia ya  usuluhishi (non-litigation) sambamba na matakwa ya Ibara ya 107A (2)(d), Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977 ambayo inatamka bayana kuwa;

katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, mahakama zitafuata kanuni zifuatazo, yaani kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro”.

Naye Wakili Mkuu wa Serikali (Solicitor General) Dkt .Boniphace Luhende alisema  kuwepo kwa kikao hicho ni jambo la kujivunia  kwani  kitasaidia kufahamu changamoto ambazo wanakutanazo wadau kwa ujumla.

Kikao hicho cha siku moja kilihusisha wajumbe kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi,Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma pamoja na Mahakama ya Tanzania Kanda ya Dodoma.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt.Juliana Massabo (katikati) akiongea neno wakati wa ufunguzi wa kikao kazi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.Kushoto kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe Dkt. Adam Mambi na kulia kwake ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe Sylvia Lushasi.
 Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Dodom,a Mhe. Sylvia Lushasi akisoma taarifa ya mashauri yaliyopo Mahakama Kuu Dodoma.
 Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma Mhe. Dkt.Fatma Khalfani, akichangia mada katika kikao kazi hicho.
   Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Suleimani Hassan akichangia mada katika kikao kazi hicho.
  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt.Juliana Massabo (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wadau walioudhuria kikao kazi hicho (kushoto kwake) ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma Mhe. Dkt. Adam Mambi, anayefuatia ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Dkt.Fatma Khalfani (kulia wa pili) ni Jaji wa Mahakama Kuu Dodoma, Mhe. Suleimani Hassan, (kulia) ni Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Kanda ya Dodoma.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni