- Jaji Mkuu azindua kikao cha Mahakama hiyo kwa mara ya
kwanza
- Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea wafurahishwa
na ujio wa huduma hiyo
Na Tiganya Vincent-Mahakama -Songea
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 14 Agosti, 2023 amezindua rasmi kikao
cha kwanza cha Mahakama ya Rufani sambamba na ufunguzi wa Masjala ndogo ya
Rufani katika Mahakama Kanda ya Songea hatua ambayo inatanua wigo wa
upatikanaji wa haki karibu na wananchi.
Akizungumza wakati na
Viongozi wa Mkoa wa Ruvuma kabla ya uzinduzi huo wa kihistoria Jaji
Mkuu, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, tukio hilo ni sehemu
ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025
katika kusogeza huduma ya utoaji haki karibu zaidi na
wananchi, hivyo Mahakama imejipanga kukabiliana na changamoto ya
umbali unaowalazimu wananchi kutumia gharama na muda mwingi kuifuata
huduma ya haki.
“Siku ya leo ni siku
ya historia kuanzia tulipoanza huduma ya Mahakama mwaka 1920 ambako
Mahakama ya Rufani ilipatikana Dar es Salaam pekee. ambako Majaji walilazimika
kutumia usafiri wa aina mbalimbali ili kupeleka huduma ya Mahakama
ya Rufani kwa wananchi, lakini hivi leo huduma hii imefika hapa Songea,”
ameeleza Jaji Mkuu.
Amesema
kuwa, kuanzia sasa wananchi wa mkoa wa Ruvuma
hawatalazimika kuifuata huduma ya Mahakama ya Rufani mkaoni Iringa
bali huduma hiyo itapatikana ndani ya Kanda hiyo.
Msajili wa Mahakama ya
Rufani (T), Mhe. Sylivester Kainda ameeleza kuwa jumla ya
mashauri ya aina mbalimbali 34 yatasikilizwa katika kikao cha Mahakama ya
Rufani ambacho kimezinduliwa leo na kusema kuwa uzinduzi
huo ni nafuu kwa wananchi wa Mkoa huu ambao wengi walikuwa
wakipiga simu kuomba mashauri yao yahairishwe kutokana na kutokuwa na
nauli ya kufika Iringa ambapo yalikuwa yakisikilizwa kabla.
Amesema
mashauri 34 yatasikilizwa kuanzia leo tarehe 14 Agosti, 2023 hadi
tarehe 1 Septemba, 2023 na yatasikilizwa na Majaji wa Mahakama ya
Rufani wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Juma ambaye ameambatana na Majaji wengine wa Mahakama ya
Rufani ambao ni pamoja na Mhe. Dr Gerald Ndika, Mhe. Rehema Kerefu
na Mhe. Sam Rumanyika.
Mhe. Kainda amesema
kikao hicho cha Mahakama ya Rufani ,Masjala Ndogo ya Songea kitatumia wiki tatu
kitasikiliza mashauri yanayohusu Rufani ubakaji Mauaji na matumizi madaraka ya
madaraka.
Naibu Msajili Mahakama
Kuu, Masjala Ndogo ya Songea Elizabeth Nyembere amemshukuru Jaji Mkuu kwa
uamuzi wake wa kuanzisha Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufani kwa kuwa itasaidia
kupunguza gharama kwao na kwa wadau ambao walikuwa wakitumia fedha nyingi
Kwenda Iringa.
Amesema watumishi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Songea na wadau wataokoa fedha ambazo walikuwa
wakizitumia kama nauli na posho kwa ajili ya kupeleka nyaraka na kufuatilia
Rufani mkoani Iringa na hivyo fedha hizo kuelekezwa katika shughuli nyingine za
utoaji haki.
“Hii ndio mara ya kwanza,
kwa kweli tunapenda kumshukuru sana Jaji Mkuu kwa uamuzi wake ambao umewasaidia
wananchi wa maeneo ya pembezoni kama vile Mbinga, Namtumbo kutoka kwao hadi
Iringa kufuatilia Rufani zao…kwani kutoka hapo Songea hadi Iringa ni karibu ni
Kilometa 400 bado hajatoka Mbinga na Namtumbo…hii ni Faraja kwetu na kwa wadau
wetu kuwa na Masjala Ndogo hapo” amesisitiza.
Tukio hilo pia
lilishuhudiwa na viongozi wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Kanda ya
Songea na Uongozi wa Mkoa wa Ruvuma ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Kamati ya
Ulinzi Mkoa na wageni mbalimbali.
Uzinduzi wa Masjala hiyo ndogo ya Mahakama ya Rufani inafanya zifike 17 baada ya ile iliyozinduliwa Mkoani Morogoro mwezi Aprili mwaka huu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiopokea salamu za heshima kutoka katika kikosi cha Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Ruvuma leo tarehe 14 Agosti 2023 ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa vikao vya Mahakama ya Rufani, Masjala Ndogo ya Songea.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akiongozwa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), David Mabula kukagua gwaride la Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Ruvuma ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa vikao vya Mahakama ya Rufani katika Kituo Jumuishi cha Mahakama Kuu Kanda ya Songea vilivyoanza leo 14 Agosti na kutarajia kufikia tamati Septemba 1, 2023.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni