Jumanne, 15 Agosti 2023

WANAFUNZI WA SHULE YA HOPE OF THE NATIONS WATEMBELEA MAHAKAMA KUPATA ELIMU

 Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma

Hakimu Mkazi  Mfawidhi  wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa, jana  tarehe 14, Augosti 2023, ameongoza  maafisa Mahakama kutoa elimu ya huduma za Mahakama kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Hope of the Nations, iliyopo kata ya Bangwe,Wilaya ya Kigoma, Mkoani Kigoma.

Elimu hiyo imetolewa baada ya wanafunzi pamoja na walimu wao walipo tembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, kwa lengo la kujifunza taratibu mbalimbali za uendeshaji wa mashauri Mahakamani hapo.

“Mnatakiwa kusoma kwa bidii na mimi nitaendelea kutoa elimu inayohusu sheria kwa kuwa ninyi ndio wanasheria na mahakimu wajao. Pia mnapaswa kuwa watu wema katika jamii hasa kutii sheria zilizopo mkianza na sheria za shule ili kutimiza ndoto zenu,” amesema Mhe. Rose. 

Aidha Mhe. Rose amewapongeza walimu wa shule hiyo kuchagua Mahakama ya Tanzania kuwa sehemu ya darasa katika kuwajengea watoto uwezo, weledi, na ujasiri wakingali wadogo kwani  wanafunzi  hao ndio viongozi wajao wa nchi.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina, amewaelezea wanafunzi hao kuhusu Muundo wa Mahakama ya Tanzania na utaratibu wa ufunguaji wa mashauri ya jinai na madai kwa Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama Kuu na namna ya kukata rufaa katika mahakama hizo huku akisema kuwa Mahakama ya Rufani ndio Mahakama ya juu hapa Tanzania. 

Ameongeza kwamba mbali na huduma zitolewazo mahakamani kila siku kwa wananchi wa Tanzania. Kama Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma ina vipindi vya radio kila mwanzo na mwisho wa mwezi kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi masuala ya sheria na hutoa elimu hiyo kila siku ya Jumatanoya wiki.

Naye Wakili wa Kujitegemea Bw. Sadiki Aliki, alipata fursa ya kutoa elimu inayohusu mawakili wa kujitegemea na shughuli zao ambapo amewataka wasome kwa juhudi na kufanya chaguo sahihi katika maisha yao ya elimu ili wasomee elimu wanayopenda ikiwemo sheria, maana ina manufaa makubwa katika maisha ya mwanadamu na maendeleo yake katika kujiletea maendeleo binafsi na ya Taifa.

Kwa upande wake Mwalimu Delphinus Mugalura, ameishukuru Mahakama  hiyo kwa mapokezi mazuri, na kuahidi kuendelea kuitembelea  kwa nia ya kujifunza zaidi ili watoto wanufaike uwepo wake katika eneo hilo.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa, akifafanua jambo wakati alipokuwa akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Hope of the Nations iliyopo Bangwe Kigoma, walipofika mahakamani hapo kwa ajili ya kupata elimu juu huduma zitolewazo na Mahakama, katika ukumbi wa Mahakama ya wazi uliopo katika jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma.

Wakili wa Kujitegemea Bw. Sadiki Aliki, akifafanua jambo kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Hope of the Nations ilipo Bangwe Kigoma, wakati akitoa elimu ihusuyo mawakili wa kujitegemea na huduma wanazotoa kwa wananchi wanaokuwa na mashauri mbalimbali mahakamani.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa, akielezea moja ya kazi kubwa za Mahakama ya Tanzania katika kuwahudumia wananchi, wakati akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Hope of the Nations ilipo Bangwe Kigoma.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Rose Kangwa akiwa  katika picha ya pamoja na wanafunzi na  walimu wao wa  shule hiyo.

(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo - Mahakama) 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni