·Awataka kuwa huru, kuvumilia, kutopendelea mtu yoyote
Na Faustine Kapama,
Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 10 Agosti, 2023 amewaapisha Mahakimu
Wakazi 38 wapya na kuwataka kuwa huru, kuvumilia na kujiepusha na upendeleo wowote
ili kutekeleza kikamilifu jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
Akizungumza katika halfa
fupi ya uapisho huo uliofanyika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof.
Juma amewakumbusha Mahakimu hao umuhimu walionao katika jamii kwa kuwa ndiyo wanaoshughulikia
asilimia 70 ya mashauri yote yanayosajiliwa katika ngazi mbalimbali za Mahakama.
Amewahimiza kuendeza zifa zilizopelekea wao kupata nafasi ya kuhudumu katika
nafasi ya Hakimu Mkazi.
Mhe. Prof. Juma ametaja moja
ya sifa hizo ambazo ni muhimu ni uhuru wa Hakimu (independence of the magistrate)
unaomaanisha kutokuwa na uegemezi katika kuendesha mashauri na kutoa maamuzi. Akahimiza
kuwa maslahi yotote ambayo yapo nje ya kiapo chao yasisukume uamuzi wanaoutoa
katika mashauri.
“Jaji Mkuu hawezi hata siku moja kukupigia simu
na kukuambia katika shauri lililopo mbele yako unatakiwa kuliamua hivi. Ukipata
simu kama hiyo ujue kuna matatizo. Kwa hiyo, wewe ni huru, kilichopo mbele yako
unatakiwa kukiamua kwa uhuru bila nguvu ya rushwa wala ushawishi. Kiongozi wako
atakuingilia tu kama kutakuwa na ucheleweshaji au hufuati utaratibu,” amesema.
Jaji Mkuu amewakumbusha
Mahakimu hao kuwa uhuru waliokabidhiwa ni kiini cha ofisi ya Mahakama na kwa
kuzingatia kuwa Kikatiba Mahakama ya Tanzania ni Mhimili wa Tatu wa Dola na unatakiwa
kutekeleza majukumu yake kwa uhuru, ambao tafsiri yake ni kazi ambazo wanazifanya
kila siku.
Amewaambia kuwa maneno yaliyopo
katika kiapo chao kwamba watatekeleza majukumu yeo kwa mujibu wa Katiba na Sheria,
bila uwoga, upendeleo, chuki wa huba yanawakumbusha uhuru mkubwa ambao sheria
na Katiba imewapa.
“Kupitia maneno haya, mmeahidi
mtafanya maamuzi kwa mujibu wa sheria bila kujali matakwa binafsi. Unaweza kuwa
na mawazo yako kwamba huyo aliyeko mbele yako anastahili kuadhibiwa, lakini
kama ushahidi hausemi hivyo unatakiwa usifuate nafsi yako, fuata sheria na
ushahidi unavyosema,” amesema.
Jaji Mkuu amewaeleza
Mahakimu hao kuwa upendeleao ni moja ya dhambi kubwa ya kisheria ambayo hufanyika,
hivyo akawahimiza kutokuwa na upendeleo ambao unaweza kupelekea kupoteza uhuru
waliopewa na Sheria.
“Mtu anapofika mahakamani
anategemea shauri lake litaamuliwa bila upendeleo wowote. Kuna mambo mengine ya
kijamii mnatakiwa mjiepushe nayo ambayo yanaweza kutoa taswira kwamba utapendelea.
Itabidi uishi maisha ambayo yatakufanya uwe mpweke kidogo, lakini huo upweke
una lengo la kutotoa tafsiri au taswira kwamba wewe unaweza kuwa na upendeleo,”
amesema.
Kadhalika, Mhe. Prof.
Juma amewahimiza Mahakimu hao kuwa na uvumilivu, subira na hasa wanaposikiliza ushahidi
unaoghubikwa na mabishano kutoka pande zinazohusika, kwa kuwa wananchi wanaofika
mahakamani hawana uelewa wa sheria.
“Ni muhimu kuwavumilia,
kuwaelimisha taratibu na kuhakikisha wanaelewa kile kinachoendelea. Uvumilivu
ni muhimu sana. Hakumu au Jaji hatakiwi kukasirika, hata kama kuna maudhi ya aina
yoyote, ukifanya hivyo tafsiri itaonyesha uamuzi wako utaegemea upande wa pili,”
Jaji Mkuu ameonya.
Amewakumbisha pia kusikiliza
ushahidi kwa makini na kutafakari kia kina sheria kabla ya kufikia maamuzi kwa
vile sheria inawapa nguvu kubwa, ikiwemo kupeleka watu magerezani. “Sheria inawapa
nguvu hizo, lazima mtafakari sana, sikilizeni ushahidi kwa makini, some sheria
kwa makini ili hata kama unakosea moyo wako unakuwa thabiti na safi,” amesema.
Jaji Mkuu amesema kuwa kuna
mambo mengine wanayoamua hugusa maisha na mali za watu na hutoa maamuzi mazito
kwenye mambo ya talaka, ndoa, matunzo ya watoto, mgawanyo wa mali na ndoa
kuvujika.
“Haya ni maamuzi mazito
sana, yanaweza kubadili maisha ya binadamu mwenzako, ni maeneo ambayo lazima
utafakari, lazima ujiridhishe kuwa uamuzi wako ni sahihi na utausimamia,”
amesema.
Awali, akimkaribisha Jaji
Mkuu kuongea na Mahakimu hao, Kaimu Jaji Kiongozi, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dar
es Salaam, Mhe. Latifa Mansoor, aliwapongeza kwa kupata nafasi hiyo na kuwakaribisha
katika Mahakama ya Tanzania kwenye majukumu ya utoaji haki kwa mujibu wa Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliwaeleza kuwa baada ya
hapo watapata mafunzo ya ufahamu kwamba Hakimu lazima awe mwadilifu, mwaminifu
na aishi katika kiapo alichokula kuwa atafanya kazi kwa mujibu wa sheria,
tamaduni za kitanzani na kwa mujibu wa sheria bila hofu, huba, chuki na upendeleo.
Hafla ya uapisho huo imehudhuria
na Majaji Wafawidhi wa Divisheni mbalimbali za Mahakama Kuu na viongozi wengine
waandamizi wa Mahakama, akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma,
Watendaji pacha wa Mahakama Kuu, Bw. Leonard Magacha na Mary Shirima na Msajili
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni