Jumatano, 9 Agosti 2023

TUMIENI NJIA YA USULUHISHI UTATUZI WA MIGOGORO

 Na Sade Soka - Mahakama (UDSM) 

 

Hakimu Mkazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Mohamed Burhani, ametoa rai kwa wananchi kutumia njia ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro mbali mbali ili kuendelea kuendeleza amani baina ya pande zote za mgogoro na shughuli za kiuchumi.

 

Alitoa rai leo tarehe 9 Agosti, 2023 wakati akitoa elimu kuhusu utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika eneo la Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi iliyopo jijini Dar  es Salaam kwa wananchi waliofika kupata huduma za haki katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na Divisheni hiyo.

 

Ambapo aliwaambia kwamba utatuzi wa migogoro kwa njia hiyo una faida kwa vile huokoa muda kwani hufanyika ndani ya siku 30, pia huokoa gharama wanazozitumia kufika mahakamani.

 

“Katika utaratibu huu ikitokea mmekubaliana mmefika mwisho, mtaandika hati ya makubaliano ambayo chini atasaini Msuluhishi na itakuwa ina nguvu sawa na maamuzi ya Mahakama kwa hiyo ndiyo faida ya usuluhishi” amesema Mhe. Burhani.

 

 

Pia aliwaaminisha wananchi kuwa migogoro yote inayotatuliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi huwa ni siri kati ya wadaawa na Msuluhishi, hivyo wasiogope kuleta migogoro yao ili iweze kutatuliwa na kurejesha amani baina ya pande zote mbili zinazohusika na mgogoro.

 

Kituo hicho hutenga siku ya Jumatano ya kila wiki kwa ajili ya kuwapa wananchi elimu juu ya suala hilo na fawaida zake. 

 

Hakimu Mkazi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi, Mhe. Mohamed Burhani, akitoa  elimu  kwa wananchi kutumia njia ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro mbalimbali  leo tarehe 9 Agosti, 2023 katika eneo la Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi iliyopo jijini Dar es Salaam.

 


Picha za chini na juu ni baadhi ya wananchi wamsikiliza Hakimu huyo.

 




(Picha na Magreth Kinabo – Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni