·
Wafanya kikao cha
mwaka
·
Wapigwa msasa
katika mashauri ya utekelezaji, mirathi
·
Wafanya hafla ya
kuwaaga wenzao
Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania
(JMAT) katika Mkoa wa Pwani jana tarehe 4 Agosti, 2023 kimefanya mkutano wa
mwaka, kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji baada ya kupata mafunzo katika
maeneo muhimu yanayohusu ukazaji na utekelezaji wa hukumu na masuala ya mirathi.
Kadhalika,
kulifanyika hafla fupi katika ukumbi wa VIP lounge Ruvu -JKT Mlandizi Kibaha kwa
ajili ya kuwaanga wenzao ambao wamehamia sehemu mbalimbali katika utumishi wa Mahakama.
Kabla ya kuzama
katika Mkutano huo wa mwaka, wajumbe walipata mafunzo kutoka kwa mwezeshaji
ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam,
Mhe. Elimo Masawe.
Mhe. Masawe
aliwaeleza wajumbe hao kuwa kila maamuzi yanayofanyika ni lazima Hakimu
ahakikishe amesoma sheria na kuielewa inataka afanye nini na aamue nini na
mwisho atoe maamuzi sahihi kwa mujibu wa sheria na sio matakwa yake.
Alieleza Hakimu
sio Refarii au Kamisaa anayesubiri kupuliza filimbi pale makosa yanapotokea na
kusema nani kashinda na nani kashindwa, bali yeye ni mtu anayetakiwa kuongoza ili
kufika mahali ambapo ataona nani amethibitisha madai yake na sio nani ameshinda
au ameshindwa.
Naibu Msajili aliwataka
wafawidhi wote kabla ya kuanza usikilizaji wa shauri kujiridhisha kama madai
yaliyoletwa mbele yao yako kisheria na yamekidhi matakwa yote ya sheria.
Baada ya mafunzo
hayo, Mwenyekiti ya JMAT Pwani, ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi alimshukuru Mhe. Masawe kwa
kuwafundisha na kuwakumbusha wajibu wao katika kazi.
Alimuomba Naibu
Msajili Masawe asichoke pindi watakapomhitaji tena kutoa elimu katika maeneo
mbalimbali yanayohusu utoaji haki.
Baada ya mafunzo
hayo, Kikao cha Mwaka kiliendelea ambapo wajumbe waliongelea masuala ya
ushirikiano na kusaidia katika hali zote na kuimarisha ufanisi katika utendaji
kazi wa kila siku. Akiongelea jambo hilo, Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Pwani,
ambaye pia ni Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Mkuranga, Mhe.
Herieth Mwailolo alisema.
“....kuna baadhi yetu
ambao wametutangulia wanaweza kuwa msaada mkubwa sana, tuwatumie hao na wao
wakati mwingine wakikutana na kitu ambacho sio sahihi watuite na kutushauri,
hii itasaidia sana kuleta ufanisi wa kazi zetu.”
Baada ya Mkutano
huo, kulifanyika hafla fupi ya kuwaanga watumishi saba waliohamishwa vituo vya
kazi. Katika halfa hiyo, waaga watatu wameenda kuwa wasaidizi wa Majaji na
wengine kwenda katika Kituo Jumuishi Temeke.
Waagwaa wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa JMAT Pwani, Mhe. Mhoi
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni