Na Mary Gwera, Mahakama
Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amewasisitiza Mahakimu Wakazi wapya kuzingatia matumizi ya TEHAMA ili kutekeleza azma ya Mahakama nchini ya kuwa Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.
Akizungumza wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu wakazi wapya 37 wa Mahakama za Mwanzo jana tarehe 14 Agosti, 2023 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Chuma aliwataka Mahakimu hao kujifunza matumizi ya mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayosimamiwa na Mahakama ili wasipate ugumu wanapotekeleza majukumu yao.
Mhe. Chuma aliibainisha Mifumo hiyo kuwa ni pamoja na Mfumo ulioboreshwa wa Kusajili na Kuratibu Mashauri kwa njia ya Kielektroniki (ACM), TANZLII, Mfumo wa Kielektroniki wa Mawakili (e-Wakili), Maktaba Mtandao ‘e-Library’ na mingine.
Akisisitiza kuhusu matumizi ya TEHAMA, Msajili Mkuu alirejea hoja hii ambayo iliwahi kusisistizwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakati wa hafla fupi ya kuwaapisha Mahakimu Wakazi wapya 41 tarehe 27 Novemba, 2020, ambapo Jaji Mkuu alisema, “katika karne hii ya 21 yenye kusukumwa na ushindani na matumizi ya TEHAMA, pamoja na kusikiliza mashauri kama Hakimu, mtawajibika kuwa sehemu ya programu za maboresho.”
Mbali na matumizi ya TEHAMA, Mhe. Chuma aliwasihi Mahakimu hao kulinda afya zao na kujiepusha na vitendo vitakavyowapa sonona au msongo wa mawazo au kuharibu afya ya akili.
“Miongoni mwa mambo yanayoweza kutatiza afya ya akili ni pamoja na ulevi wa kupindukia, madeni, mahusiano mabaya na watu au marafiki wasiofaa. Mambo haya licha ya kuwa na madhara kwenye ustawi wenu pia kiafya yanaweza kuwaletea matatizo ya kiajira na utendaji kazi wenu,” alisema Msajili Mkuu.
Alisisitiza kwamba, hatopenda kuona kati yao atakayefukuzwa kazi kutokana na vitendo visivyofaa. “Jitunzeni maisha yenu na kuheshimu viapo vyenu, vilevile, jitahidini kuuliza mara kwa mara ili msitende jambo lolote linalokinzana na sheria na taratibu,” alisema.
Pamoja na kupata umahiri katika masuala ya kijinai na kimadai na taratibu zake (hard skills) na mengine watakayopata katika mafunzo hayo, Msajili Mkuu aliwaeleza Mahakimu hao kuwa, anatarajia wapate pia ujuzi (soft skills) katika kusikiliza (listening skills), kuandika (writing skills), kuwasiliana (communication skills), uwezo wa kutafakari na kutatua changamoto mbalimbali, uwezo wa kuandika hukumu au maamuzi thabiti.
Kadhalika, Mhe. Chuma amewataka Mahakimu hao kulinda taswira ya Mahakama kwa kujenga imani kwa umma kwa kuzingatia miiko na utamaduni wa Mhimili huo na kujiepusha na matumizi yasiofaa ya mitandao.
“Epukeni matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii bali itumieni kwa manufaa na tija, sitegemei mtumie mitandao ya kijamii mathalani kudai stahiki zenu badala ya kutumia taratibu za kiutumishi zilizopo kwa mujibu wa miongozo. Matumizi yasiyofaa ya mitandao ya kijamii yanaweza kuwaingiza kwenye makosa ya kimaadili kwa kuwa mtakuwa mnakinzana na kanuni za maadili kwa Maafisa wa Mahakama za 2020,” alisisitiza.
Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yanafanyika Chuoni hapo kwa siku tano hadi tarehe 18 Agosti, 2023.
Programu hii ya mafunzo elekezi imeandaliwa kwa lengo la kuwaongezea weledi, miongoni mwa mada watakazopatiwa Mahakimu hao ni pamoja na maadili ya kimahakama, usimamizi wa mashauri, tathmini ya ushahidi, uandishi bora wa hukumu na namna bora ya kutoa adhabu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni