·Kuteta na mwenyeji wake Mustapher Siyani
·Kujionea jengo jipya Makao Makuu ya Mahakama Tanzania
Na.
Faustine Kapama-Mahakama
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda, Mhe. Dkt.Flavian Zeija leo tarehe 15 Agosti,
2023 amewasili nchini kwa ziara ya siku tano ya kikazi kuitembelea Mahakama ya
Tanzania kwa malengo mbalimbali.
Akiwa
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Mhe Zeija alipokelewa
na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu, Mhe. Latifa Mansoor pamoja na
viongozi wengine wa Mahakama, akiwemo Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu,
Masjala Kuu, Mhe. Arnold Kerikeano.
Taarifa
iliyotolewa inaonyessha katika siku ya pili ya ziara yake, Mhe Dkt. Zeija atakutana
na mwenyeji wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Mohamed Siyani na kufanya naye mazungumzo mafupi katika ofisi yake katika jengo
la Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Akiwa
katika ofisi hiyo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Uganda ambaye ameambatana na
Katibu Mkuu wa Mahakama Uganda, Dkt. Pius Bigilimana atapokea taarifa ya
maboresho ya Mahakama kutoka Kitengo cha Maboresho (JDU) na taarifa ya usimamizi wa mashauri na
utendaji wa Mahakama itakayotolewa na Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri.
Mhe. Dkt. Zeija pia
atatembelea Kituo
cha Uendeshaji wa Mtandao cha Mahakama ya Tanzania kabla ya kuelekea katika
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia Temeke na kupata maelezo
mafupi kuhusu Kituo hicho na baadaye kujionea namna Mahakamaa Inayotembea
inavyofanya kazi.
Katika
siku ya tatu ya ziara yake, Mhe. Zeija ataelekea jijini Dodoma kutembelea Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na pia kujionea jengo jipya la Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania ambalo lipo katika maeneo ya Tambuka Reli.
Siku ya nne ya ziara yake, Jaji Kiongozi Uganda atarudi jijini Dar es Salaam kwa shughuli zingine za kimahakama na siku ya tano atarudi Uganda. Ziara hii ni sehemu ya ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Uganda na ujirani mwema kati ya nchi hizi mbili.
Hii
ni mara ya pili kwa viongozi wakuu wa Mahakama Uganda kuitembelea Mahakama ya Tanzania.
Ziara ya kwanza ilifanywa na Jaji Mkuu wa Uganda, Mhe. Alfonse Chigamoy
Owiny-Dollo tarehe 24 Mei 2022 kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa mambo
mbalimbali.
Mhe
Owiny-Dollo alikutana na mwenyeji wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma ofisini kwake jijini Dar es Salaam na baada ya maongezi
mafupi yenye lengo la kujenga ushirikiano katika masuala mbalimbali ya
kimahakama alielekea Tanga kutembelea Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Akiwa
Lushoto, Jaji Mkuu Uganda na ujumbe wake alitapata fursa ya kubadilishana
uzoefu na viongozi wa Chuo hicho, ikiwemo namna kinavyofanya kazi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni