Na Festor Sanga- Mahakama, Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Jaji Lameck Mlacha amefurahishwa na namna Hifadhi ya Taifa ya Gombe inavyoendesha shughuli za utalii na kupongeza tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Jane Goodall iliyoanzishwa nchini mwaka 1977.
Hifadhi hiyo ina kilometa za mraba 54 ikipatikana mwambao wa Mashariki mwa ziwa Tanganyika.
Mhe. Jaji Mlacha alisema hayo katika ziara hiyo iliyofanyika tarehe 13 Agosti, 2023 kwenye hifadhi hiyo iliyokuwa na lengo la kufanya utalii na kujifunza, ambapo aliambatana na Mhe. Jaji Stephen Magoiga na walipata fursa ya kutalii hifadhi hiyo yenye umaarufu mkubwa unaotokana na kivutio chake kikubwa cha Sokwe.
Hifadhi hiyo ilipata umaarufu zaidi baada ya mtafiti wa tabia za sokwe duniani , Jane Goodall kufanya utafiti juu ya maisha na tabia za sokwe pamoja na kuandika vitabu kuhusu viumbe hao.
Wakiwa katika ziara hiyo Wahe. Majaji hao walipata fursa ya kuonana na mwuanzilishi wa Taasisi ya Jane Goodall ambaye alifurahia ujio wao na kuwakaribisha kujionea vivutio vya hifadhi ya Gombe.
Mwuanzilishi huyo Mama Jane Goodall mwenye miaka 90 ambaye bado ana nguvu na ari ya kuendeleza utalii kwa kutembea mwenyewe pamoja na tafiti alizozifanya ziliwapa hamasa Majaji juu ya umuhimu wa mazoezi, kuzingatia vyakula na kutunza afya.
“Nimeona utafiti wa tabia za sokwe unaendelea lakini ule uliofanyika awali na mama huyu umeitangaza hifadhi hii ya Gombe katika dunia hivyo utafiti uendelee”, alisema Jaji Mlacha.
Aidha Jaji Mlacha aliitaka Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyama Pori (TANAPA) kuendelea kuwa wabunifu na kujitangaza kwa njia za kisasa ili kuongeza mapato zaidi ikiwa ni utekelezaji kwa vitendo maono ya Serikali kuhusu mwelekeo wa utalii siku za usoni kuongezeka, huku akiwasisitiza kuendelea kuboresha miundombinu ya majengo na usafiri kwa ajili ya kuwahudumia watalii.
Upekee wa hifadhi ya Gombe unatokana na kutokuwa na Wanyama wakali kama Simba na Chui hivyo kufanya hifadhi kuwa rafiki kwa watalii kutembea kwa miguu wakishuhudia mandhari na vivutio vyake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha akisalimiana na Jane Goodall ambaye ni mwanzilishi wa Taasisi ya Jane Goodal mara walipokutana katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe Jaji Lameck Mlacha(katikati) na Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe Jaji Stephen Magoiga(wa kwanza kulia) wakipewa taarifa ya Hifadhi ya Taifa ya Gombe iliyotolewa na Muongoza wageni Paulo Ngelela.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe.Lameck Mlacha akipiga picha ya kumbukumbu ya Sokwe mara baada ya kuwaona katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Stephen Magoiga(wa pili kulia) akiwa katika mazungumzo na moja ya mtalii kutoka nchi Israel aliyefika katika hifadhi hiyo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe.Lameck Mlacha(wa tatu kulia) na Jaji Stephen Magoiga (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Jane Goodall ambaye ni mwuanzilishi wa Taasisi ya Jane Goodall(kushoto wa tatu). Wengine ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Bw. Benjamin Mlimbila(wa kwanza kulia) .
Moja kati ya aina sokwe wanaopatikana katika hifadhi hiyo.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni