Na Seth Kazimoto-Mahakama Kuu, Arusha
Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto (IJA), kwa kushirikiana na wadau, kimeanza kikao kazi katika
Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha kupitia mtaala wake ili kuendana na hali
halisi ya soko la sasa la ajira na mabadiliko ya kiteknolojia na uchumi.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa kikao hicho hivi karibuni, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama wa IJA,
Mhe. Dkt. Patricia Kisinda alieleza kuwa mapitio ya mtaala wanayofanya
yanahusisha uingizaji wa Mwongozo wa Utoaji Adhabu (Sentencing Guidelines) ili
kuuboresha na hatimae Chuo kuweza kutoa wahitimu mahiri katika taaluma
wanazosoma.
Alisema katika kikao kazi
hicho kitakachohitimishwa tarehe 22 Septemba, 2023 kuwa kufanyika kwa mapitio
ya mtaala wa Chuo hicho kunatarajiwa kuleta mafanikio makubwa hasa katika
kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Wanachuo watakaokuwa
wanahitimu katika Chuo watakuwa na uelewa wa kina na uwezo mkubwa wa kufanya
kazi walizosomea. Chuo kitaongeza wigo wa mafunzo yake na hivyo kukuza
ushirikiano na waajiri pamoja na wadau, na hatimae kusaidia katika kukuza
uchumi wa nchi,” Mhe. Dkt. Kisinda alisema.
Alibainisha pia kuwa Mahakama
itanufaika kwa kuajiri wahitimu kutoka IJA wenye weledi wa kazi na hivyo
kuiwezesha kutimiza majukumu yake ipasavyo na kupelekea uwepo wa taswira chanya
ya wananchi kwa Mhimili huo.
Mkurugenzi huyo alisema imani
kubwa ya wananchi kwa Mahakama itawafanya kupeleka migogoro yao mahakamani na
kuwezesha utawala wa sheria kustawi nchini.
Wajumbe mbalimbali
wanahudhuria kikao Kazi hicho, wakiwemo Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Tafiti, na
Ushauri Elekezi, Bw. Goodluck Chuwa, Mkufunzi wa Chuo cha Utumishi wa
Umma-Magogoni Dar es Salaam, Bi. Khadija Ramadhani, Mkurugenzi Msaidizi wa
Utawala -Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha na Mkurugenzi wa Kumbukumbu
na Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Malimo Manyambula.
Kikao kazi hicho kimefadhiliwa
na programu ya kujenga mfumo endelevu wa mapambano dhidi ya rushwa nchini,
yaani Building Sustainable Anti-Corruption Action in Tanzania (BSAAT).
Afisa Mwambata wa Programu ya Kujenga Mfumo Endelevu wa Mapambano Dhidi ya Rushwa Tanzania (BSAAT), Bw. Nkrumah Katagira akiwa katika kikao kazi hicho. Kushoto ni Mkufunzi wa Chuo cha IJA, Bw. Zuberi Suddi.
(Habari hii imehaririwa na
FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni