Na. Hilary Lorry – Mahakama Lindi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim hivi
karibuni amefanya ziara ya kikazi mkoani Lindi na kukagua shughuli
mbalimbali za kimahakama katika Wilaya tatu (3) zilizopo katika mkoa huo ambazo
ni Liwale, Nachingwea na Ruangwa.
Akizungumza na watumishi wa Mahakama katika Wilaya
hizo kwa nyakati tofauti akiwa katika ziara ya ukaguzi wa shughuli za Mahakama Jaji
Mfawidhi Mhe. Ebrahim aliwapongeza watumishi wa Mahakama za mkoa wa Lindi kwa kufanya
kazi kwa uadilifu, weledi na ufanisi mkubwa katika kuwahudumia wananchi.
“Nafahamu kazi yetu ya utoaji haki kwa wananchi ni
ngumu lakini nichukue fursa hii kuwapongeza Mahakimu wote wa Mkoa Lindi kwa jitihada
kubwa za uondoshaji wa mashauri ya mlundikano na mikakati mizuri mliyojiwekea yenye
lengo la kutozalisha mashauri ya muda mrefu (backlog cases)”, aliongeza Mhe. Ebrahim.
Mhe. Ebrahim alipata wasaa wa kufanya ukaguzi wa
Mahakama zilizopo chini ya Kanda ya Mtwara na ukaguzi wa Mirandi ya ujenzi
inayoendelea ikiwemo ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Liwale ambao upo katika
hatua za mwisho kabla ya kukabidhiwa kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kimahakama,
na pia alitembelea eneo ambalo hivi karibuni linakusudiwa kujengwa
Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea.
‘’Tujitahidi kufanya kazi kwa bidii, maarifa, weledi na
kwa ushirikiano hii itafanya Mahakama yetu ing’are na kuwa mfano bora wa
kuingwa.Kila mmoja wetu awajibike kwa nafasi yake na tufanye kazi kama timu
moja na siku zote tufanye kazi katika ubora unaotakiwa”, alisisitiza Jaji Mfawidhi huyo
Kwa upande wa
ushirikiano na wadau Mhe. Ebrahim alisema, ni jambo la msingi sana kiutendaji
kushirikiana na wadau kwa karibu. “Natambua ushirikiano na ushirikishwaji mzuri
uliopo kati ya Mahakama za Mkoa wa Lindi na wadau, mahusiano mema yanatija
kubwa katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kwa wote”, aliongeza
Mhe. Ibrahim.
Vilevile aliupongeza uongozi wa Mahakama Mkoa wa Lindi
kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya utoaji elimu kupitia vyomba vya Habari ikiwemo Radio Mashujaa FM, Mitandao
ya kijamii, Club za Mahakama katika shule mbalimbali za sekondari na utoaji wa
elimu kwenye mikusanyiko ya watu na kwa wateja wanaofika Mahakamani asubuhi kwa
ajili ya kusikiliza mashauri yao.
Katika ziara hiyo Mhe Jaji Mfawidhi Kanda ya Mtwara
aliongozana na viongozi mbalimbali waandamizi wa Kanda hiyo akiwepo Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara Mhe. Fredrick Lukuna,
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Mhe. Consolata Peter
Singano, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Bw.Richard
Mbambe na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Lindi Bi.Qiup Mbeyela.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe.Rose Ebrahim akiongea na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Liwale, Nachingwea na Ruangwa( Hawapo kwenye picha) alipofanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za kimahakama mkoani Lindi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara Mhe. Rose Ebrahim (Mwenye skafu) akiwa kwenye picha ya pamoja Watumishi
wa Mahakama ya Wilaya ya Liwale, Nachingwea na Ruangwa alipofanya ziara katika Mkoa huo.
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Mtwara Mhe. Rose Ebrahim akiandia neno la kumbukumbu katika
ubao wa kumbukizi Mahakama ya Wilaya ya
Ruangwa.
Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Rose Ebrahim akipanda mti katika viwanja vya
Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa na kulia ni Hakimu
Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Ruangwa Mhe.Mariam Mchomba akishuhudia.
Habari Hii imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni