Jumatano, 20 Septemba 2023

MAHAKAMA KUU MUSOMA YAIVA MATUMIZI YA TEHAMA

 

Na. Francisca Swai, Mahakama – Musoma.

Kutokana na maendeleo makubwa na ukuaji wa tasnia ya teknolojia na habari duniani, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imekuwa kichocheo cha kuleta ufanisi wa kazi katika Mahakama ya Tanzania. Uhitaji wa huduma za kimtandao ndani ya Mahakama ya  zinakuwa siku hadi siku. Watu wanatamani kurahisisha kazi kwa kutumia teknolojia na kutoa huduma bora na ya kisasa wanapotekeleza dira ya Mahakama. 

Katika kufikia azima yake na matarajio ya wateja na wadau, Mahakama ya Tanzania imewekeza rasilimali nyingi kujenga mifumo ya TEHAMA na matumizi katika maeneo mengi ikiwemo mfumo wa kusajili na usikilizwaji wa mashauri (JSDS II na e-case management), huduma za kimtandao zinazounganisha Mahakama na wateja wake (Virtual Court na teleconference) na mifumo mingine mingi.

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma kupitia kwa Afisa TEHAMA wake Bw. Simon Lyova, imebuni mfumo mpya wa kuita mashauri na kutoa matangazo kwa kutumia simu za mkononi na kompyuta mpakato. 

Awali Mahakama Kuu Musoma ilikuwa ikitumia mifumo ya vipaza sauti (microphone) ambazo wakati mwingine hushindwa kutoa huduma za viwango kwani zinaathiriwa na umbali pia ni gharama.

“Njia hii mpya ya kuita mashauri na kutoa matangazo kwa kutumia simu za mkononi na kompyuta mpakato imesaidia kupunguza gharama na kuboresha huduma kwani, sauti inatoka safi na iliyochujwa, inatoka kwa ubora na haiumizi masikio. Mfumo hauathiriwi na umbali (distance restricted connectivity) hata ukiwa nje ya jengo unaweza kuongea na sauti ikatoka kwenye mifumo ya ofisi. Unaweza kutumia mfumo kutoa sauti sehemu moja na kuacha nyingine (locality segregation of functionality)” anasema Lyova.

Bw. Lyova anaongeza kuwa  mfano, unaweza kutumia mfumo katika ukumbi wa Mahakama ya wazi kutoa sauti wakati wa usikilizwaji wa shauri ukiendelea chemba ya Jaji na sauti hiyo isitoke nje. Endapo ukumbi wa Mahakama au mkutano utakuwa umejaa na watu wengine wako nje ya ukumbi, mfumo utawawezesha kusikia huku wamekaa hata kwenye mabenchi ya kusubiria wateja. 

Aidha anasema gharama za betri kwa vipaza sauti vinaondolewa kabisa na mfumo huu. Mfumo huu ni wa kisasa na safi na unaendana na hadhi ya jengo la Mahakama Kuu Musoma.

Nao viongozi wa Mahakama hiyo, wamepongeza ubunifu huo na kusisitiza kuwa, upatikanaji wa mifumo sahihi na rafiki ya TEHAMA unaisaidia Mahakama kuwafikia watu wengi ndani ya muda mfupi hususani katika kufanikisha lengo kuu la utoaji wa haki kwa wote na kwa wakati. 

Viongozi hao wametoa rai kwa watumishi kuendelea kuwa wabunifu na kutumia mifumo iliyopo ambayo lengo lake kuu ni kuongeza ufanisi katika kazi, kufanya rasilimali kutumika kwa ufanisi na kuleta uwazi katika mifumo ya utendaji mambo ambayo yanachangia Mahakama  kufikika na kuaminika katika huduma zake za viwango.

 

 Msaidizi wa Kumbukumbu Bw. Simon Lubili, akitumia kompyuta mpakato kuita mashauri yanayosikilizwa mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Frank Moshi.


Msaidizi wa Kumbukumbu Bi. Neema Likuga, akitumia simu ya mkononi kuita mashauri yanayosikilizwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya.


   Afisa TEMAHA wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Simon Lyova akielezea namna mfumo huo ulivyounganishwa na mitambo ya TEHAMA ili kutoa huduma bora.

(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni