Jumatano, 20 Septemba 2023

WADAU HAKI JINAI SINGIDA WASISITIZWA KUUNGA MKONO MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMANI

Na Eva Leshange- Mahakama, Singida

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Allu Nzowa amewasisitiza wadau mkoani hapo kutumia Mahakama mtandao hasa katika kufungua mashauri na kusikiliza mashahidi. 

Mhe. Nzowa aliyasema hayo hivi karibuni katika kikao na Wadau wa Haki jinai kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida ambapo alisema ni muhimu Wadau hao kwenda sambamba na kasi ya Mahakama katika matumizi ya TEHAMA.

“Nasisitiza Wadau tuhakikishe tunatumia Mahakama mtandao katika kufungua kesi na kusikiliza mashahidi kwa njia ya mtandao, Mahakama kwa sasa inaenda kasi katika masuala ya kiteknolojia ni vema na sisi tuhakikishe tunaenda sambamba na kasi hiyo ili kuhakikisha  suala zima la utoaji haki halikwami,” alisema Mhe. Nzowa.

Katika kikao hicho na wadau aliwaeleza wajumbe kuwa, Mahakama ya Tanzania kwa sasa ina mpango wa dhati katika kuondoa mashauri yote yaliyozidi mwaka mmoja (1). Hivyo basi jitihada zinahitajika kuhakikisha mashauri hayakai muda mrefu mahakamani kwa kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake ipasavyo.

Aidha, wajumbe wameunga mkono suala la kuhakikisha hakuna mlundikano wa mashauri mahakamani kwa kuweka mikakati ya kuondoa na kuzuia mlundikano pamoja na kuhakikisha mashauri ya mlundikano yanaondoka na kuzuia yale yanayo karibia yasiingie.

Mikakati iliyowekwa na wadau ni pamoja na kuwa na vikao maalum (special session) za mara kwa mara, upelelezi kukamilika mapema, uwepo wa Mawakili wa utetezi mahakamani bila kukosa pasipo na sababu za msingi katika mashauri yao na kuwa na vipaumbele vya mashauri yao, na kwa mashauri ambayo yana upelelezi wa muda mrefu wadau wamekubaliana yakae hadi upelelezi utakapokamilika ndipo yaletwe mahakamani kwani wana mamlaka ya kuwapa dhamana wadaawa.

Akihitimisha  kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo aliwapongeza Wadau wote kwa kazi nzuri na ushirikiano katika kuondoa mashauri ya mlundikaono na kuwasisitiza kuongeza juhudi zaidi ili kuepuka mlundikano wa mashauri.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mhe, Allu Nzowa aliyeketi mbele (katikati) akizungumza jambo wakati wa kikao na Wadau wa Haki Jinai kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida. Aliyeketi mbele kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Singida, Bi. Elizabeth Barabara  na  kulia Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Singida, Bw. Yusuph Kasuka.

Sehemu ya wajumbe wa Haki Jinai mkoani Singida wakiwa katika kikao  cha kusukuma mashauri ya jinai kilichofanyika hivi karibuni.

Sehemu ya wajumbe wa kikao hicho. Aliyeketi wa pili kushoto ni Afisa Upelelezi Mfawidhi wa Wilaya-Itigi, ASP Joseph Gobusa.

Sehemu ya wajumbe walioshiriki kikao hicho.


Sehemu ya wajumbe wakifuatilia kinachojiri katika kikao hicho.

(Taarifa hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni