Na. Mayanga Malingila – Mahakama, Sumbawanga.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
hivi karibuni alimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Makongoro Nyerere Ofisini
kwake na kufanya naye mazungumzo na kumshukuru kwa kushiriki hafla ya uzinduzi
wa Kikao cha kwanza cha Mahakama ya Rufani katika viwanja vya Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Sumbawanga.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa huyo mara baada ya
kukutana Mhe. Prof. Juma alisema kuwa, Mkuu wa mkoa na Wakuu wa Wilaya ni wenyeviti wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa
Mahakama hivyo haina budi kusimamia nidhamu na mienendo ya Maafisa hao katika
ngazi ya Mkoa na Wilaya. Kwa kufanya hivyo watakuwa wametimiza jukumu lao la
kisheria la kusimamia maadili ya Wahe. Mahakimu katika maeneno hayo kupitia
kamati hizo na kusisitiza haki itendeke kwa anaekiuka maadili.
“Nichukue fursa hii kukushukuru kwa kuja kushirikiana
na Mahakamama katika uzinduzi wa Kikao cha Mahakama ya Rufani kwa dhumuni la
kuanzisha Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufani ni kuhakikisha Mahakama
inatekeleza Nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wake ya Upatikanaji haki kwa wakati
kwa lengo la kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi”,
aliongeza Jaji Mkuu.
Mhe. Prof. Juma alisema faida za uanzishaji wa Masjali
hiyo ni nyingi mathalani wananchi kutosafiri umbali mrefu kutafuta haki zao,
kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri yao lakini pia kuhakikisha mashauri
yanachukua muda mfupi kusikilizwa ili wananchi hao wapate muda wa kutosha
kushiriki katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
“Katiba inatoa nafasi ya Mihimili kushirikiana katika
kutekeleza majukumu yao, kwa sababu Serikali inatuwezesha kwa kutuweka pamoja
katika Mpango wa Maendeleo ya Nchi. Nia ya Mahakama ya Tanzania ni kuona
ifikapo 2025 Mikoa yote isiyokuwa na huduma ya Mahakama kuu inapatikana ili
wananchi wapate huduma hiyo kwa ukaribu zaidi bila kutumia gharama za ziada”,
alisema Jaji Mkuu.
Mhe. Prof. Juma alisema kuwa, suala la Mahakama
kutumia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuimarisha
mfumo wa utoaji haki kwa wananchi inalenga kurahisisha utoaji haki kwa wakati.
‘’Mhe. Mkuu wa Mkoa nikutoe shaka,kuwa Mahakama
imejikita zaidi katika matumizi ya TEAHAMA ili kuboresha mfumo mzima wa utoaji
haki kwa wananchi, nakuahidi Mahakama ya Rufani itaendelea kusikiliza mashauri
kwa Kanda ya Sumbawanga na endapo kutakuwa na shauri la haraka Mahakama ya
Rufani itasikiliza kwa njia ya Mahakama Mtandao (Virtual court)”, alisema Prof.
Juma.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Makongoro Nyerere
aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuwa huru na kuelekeza nguvu kubwa katika
kuwatumikia Wananchi wa Tanzania na kutoingiliwa na Serikali jambo ambalo
linaifanya kuonekana ipo huru.
“Mahakama yetu ni huru ina heshima na nguvu, uhuru huo
unatokana na kwamba Serikali haiingilii Mahakama katika kutekeleza amri zake na
ndiyo maana kuna mabadiliko makubwa yamefanyika ndani ya Mahakama,ninakupongeza
Jaji Mkuu kwa kusimamia mabadiliko hayo’’,alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (alieketi mbele), akiendelea na
mazungumzo alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Ofisini kwake pamoja na ugeni
wageni aliyoambatana nao.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Makongoro Nyerere (kushoto), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Sumbawanga Mhe. Amir Mruma (katikati) na Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga Bw.Emmanuel Munda (kulia) wakifuatilia maongezi ya Jaji Mkuu wa Tanzania (hayupo pichani).
Msajili
wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe.Sylvester Kainda (kulia), Naibu Msajili
wa Mahakama Kuu kanda ya sumbawanga Mhe.Maira Kasonde (katikakti) na Naibu Msajili na Katibu wa Jaji Mkuu Mhe. Venance Mlingi (kushoto)
wakifuatilia mazungumzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof Ibrahim Hamis Juma akielezea jambo wakati wa ziara hiyo.
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa
Mkoa wa Rukwa Mhe Makongoro Nyerere (kulia) mara baada ya kuwasili Ofisini
kwake.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni