Alhamisi, 21 Septemba 2023

JAJI EBRAHIM AENDELEZA ZIARA YAKE MKOANI MTWARA

Na. Richard Matasha-Mahakama, Mtwara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim hivi karibuni aliendelea na ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Mtwara baada ya kutoka Lindi na kutembelea Mahakama za Wilaya Masasi na Nanyumbu pamoja na Mahakama ya Mwanzo Lisekese.

Akiwa katika Mahakama hizo, Mhe Ebrahim alipokea taarifa za utendaji na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na watumishi wa Mahakama hizo. Miongoni mwa mambo muhimu aliyosisitiza ni uwajibikaji, uadilifu na kuchapa kazi. “Jukumu mama la Mahakama ni utoaji haki kwa umma na sisi sote kuanzia mtumishi wa chini kabisa tunahusika moja kwa moja katika kufanikisha hili.

“Nimefurahishwa sana na utendaji kazi wenu na nimekuja mahsusi kwa ajili ya kuwapongeza kwa mafanikio mliyofikia,” alisema. Aliwapongeza Mahakimu wa Mahakama za Wilaya hizo kwa kuondosha mashauri ya mlundikano yaliyokuwa yakiwahelemea hapo awali.

Aidha, Jaji Mfawidhi alisisitiza masuala ya nidhamu na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kanuni za utumishi wa umma. “Mtumishi yeyote atakaye kiuka misingi, sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma atawajibishwa kwa mujibu wa sheria” Mhe. Ebrahim alionya.

Katika ziara yake, Jaji Mfawidhi aliambatana na Viongozi waandamizi wa Mahakama, wakiwemo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Fredrick Lukuna, Mtendaji wa Mahakama katika Kanda hiyo, Bw. Richard Mbambe, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mnzava na wengine.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim (katikati) akiwa na Viongozi wa Mahakama katika Kanda yake, Naibu Msajili, Mhe. Fredrick Lukuna (kushoto) na Mtendaji wa Mahakama, Bw. Richard Mbambe (kulia).

Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Nanyumbu wakisikiliza jambo kutoka Meza Kuu.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Fredrick Lukuna (aliyesimama) akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Nanyumbu.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mhe. Charles Mnzava (aliyesimama) akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Masasi.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Masasi, Mhe. Batista Kashusha akielezea jambo kwa Jaji Mfawidhi, Mhe. Rose Ebrahim.

Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Lisekese wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ebrahim (kulia).

Mtendaji wa Mahakama Kuu Mtwara, Bw. Richard Mbambe akizungumza jambo na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Masasi.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni