Alhamisi, 21 Septemba 2023

WANANCHI MOROGORO WAASWA KUTOA TAARIFA KUHUSU UKATILI WA KIJINSIA

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Wananchi wa Mkoa wa Morogoro waliofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mjini hapa wamepewa elimu ya namna ya kutoa taarifa kwenye mamlaka husika wanaposhuhudia vitendo vya ukatili wa kijinsia vikifanyika kwenye jamii.

Zoezi hilo la elimu lililotolewa kwa muda wa siku tatu kuanzia Septemba 19, 2023 na maafisa kutoka Ustawi wa Jamii ambao ni wadau wa Mahakama katika muendelezo wa vipindi vya elimu, limehitimishwa leo tarehe 21 Septemba, 2023.

Akizungumza na wananchi wakati wa zoezi hilo lililokuwa linafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo hicho, Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Anna Makaranzi alisema kuwa jamii haipaswi kuwafumbia macho wale wote wanaotenda ukatili iwe kwa watoto na hata watu wazima.

Alikemea ukatili wa kingono ambao ni miongozi mwa kesi nyingi zilizopo mahakamani na kueleza masikitiko yake jinsi unavyofanywa zaidi kwa watoto na watu wa karibu, ikiwemo ndugu zao.

Afisa Ustawi wa Jamii alisema jamii isikae kimya kwani kumekuwa na tamaduni za baadhi ya watu kuficha vitendo vya ukatili kwa misingi ya kulindana. “Ni vyema unapokutana na tukio la ukatili ukatoa taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe,” alisema.

Alibainisha kuwa kuna baadhi ya fikra potofu kwenye tamaduni ambazo suala la kumpiga mwanamke linachukuliwa kama sehemu ya upendo, hivyo akawaomba wananchi kutonyamaze, bali watoe taarifa na wasaidie kusambaza elimu hiyo.

Sambamba na hilo, wananchi pia walielimishwa kuhusu taratibu za kufuata ili kuweza kuasili mtoto, elimu iliyotolewa na Afisa Ustawi wa Jamii mwingine, Bi. Judith Mbelwa ambaye alisema kuwa hatua ya mwisho ya kukabidhiwa mtoto inafanyikia mahakamani mara baada ya kufanikisha taratibu zote.

“Hata kama mtoto ameokotwa kwenye shamba lako hawezi kuwa wako mpaka taratibu zote zifuatwe ndipo ukabidhiwe na Mahakama,” alisema na kukumbushia kuwa hata baada ya kuasili mtoto hairuhusiwi kumfanyia ukatili wa aina yeyote.

Akichangia mada kuhusu masuala ya kijamii, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Augustina Mbando alisema kuwa wazazi wanapaswa kuwaweka wazi watoto wao wajue ndugu zao.

Mhe. Mmbando alibainisha kuwa kesi nyingi za mirathi zinazochukua muda mrefu mahakamani ni zile zinazojumuisha watoto waliozaliwa nje ya ndoa, huku baba au mama kutoweka wazi familia yake.

Maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro wameendelea kunufaika na elimu ya sheria ya msingi. Takwimu zinaonesha kwa mwaka 2022 kuanzia mwezi Machi watu zaidi ya 60,000 waliofika kwenye Kituo Jumuishi pekee wamefikiwa.

Kwa mwaka 2023, Mahakama zote za Kanda ya Morogoro zinatoa elimu ya msingi ya sheria kuanzia siku ya Jumanne na Jumatano. Elimu hii imechangia kupunguza makosa yaliyokuwa yanajirudia mara kwa mara.

Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Judith Mbelwa akitoa elimu kwa wananchi waliofika kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro (hawapo pichani).

Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Judith Mbelwa (aliyesimama kulia) akimsikiliza mteja (aliyekaa kushoto) wakati alipotaka ufafanuzi wa jambo lililofundishwa wakati wa zoezi la utoaji elimu.

Wananchi waliofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro wakifuatilia elimu toka kwa maafisa Utawi wa Jamii (hawapo pichani).

Wateja wakifuatilia utoaji wa elimu hiyo.

Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Anna Makaranzi akitoa elimu kuhusu kuepuka ukatili wa kijinsia wakati wa zoezi hilo.

Mteja wa Mahakama akinyoosha kidole kuuliza swali wakati wa kipindi cha elimu ya msingi ya sheria.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni