Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dr. Francis Kasabubu amewataka
wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo kusimamia Sheria,
kanuni, na miongozo inayotolewa na Tume ya Utumishi wa Mahakama wanapotekeleza
mashauri ya nidhamu kwa Maafisa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya.
Akifungua Mafunzo ya siku tatu kwa wajumbe wa Kamati za
Maadili ya Maafisa Mahakama wa mikoa ya Mbeya na Songwe yenye lengo la
kuzijengea uwezo kamati hizo, Dr. Kasabubu amesema endapo Sheria, kanuni na
miongozo itazingatiwa ni wazi kuwa wajumbe hao watatekeleza kwa usahihi
mashauri ya nidhamu kwa Maafisa Mahakama.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Maadili ya Maafisa Mahakama Mkoa wa Songwe alisema mafunzo hayo yanayotolewa na
Tume ya Utumishi wa Mahakama yatasaidia kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za
Maadili na kutatua changamoto zilizopo katika utekelezaji wa Sheria, kanuni,
taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma.
”Mafunzo haya ni moja ya misingi ya utekelezaji wa
utawala bora wa Tume ya Utumishi wa Mahakama inayozingatia Sheria, kanuni,
taratibu na miongozo katika usimamizi wa majukumu ya Kamati za Maadili ya
Maafisa Mahakama” alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwakumbusha wajumbe wa Kamati za
Maadili wajibu wao muhimu wa kuhakikisha kuwa haki za Maafisa Mahakama
zinalindwa pale inapotokea wamekiuka utaratibu katika utekelezaji wa majukumu
yao ya utoaji haki na si kuwakomoa.
Akizungumzia mafunzo hayo, Dr. Kasabubu alisema baadhi ya
mada zitakazotolewa kwenye mafunzo hayo ni kuhusu historia ya Tume ya Utumishi
wa Mahakama, uwasilishwaji wa malalamiko ya wananchi kwenye Kamati za Maadili
na utaratibu wa kuyashughjulikia malalamiko hayo.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru amewataka wajumbe wa Kamati za
Maadili kuyatumia mafunzo hayo kama chachu katika kushughulikia mashauri ya
kinidhamu kwa Maafisa Mahakama.
”Naishukuru Tume ya Utumishi wa Mahakama na kuipongeza
kwa kuandaa mafunzo haya muhimu, naamini
mafunzo haya yatakuwa ni endelevu kwa
kuwa wajumbe wake wamekuwa wakihama mara kwa mara vituo vyao vya kazi na
wengine kuteuliwa wapya hususan wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya”, alisema.
Baada ya kukamilika kwa mapitio ya Sheria ya Usimamizi wa
Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011 sura ya 237 ambazo ni kanuni za Uendeshaji wa
Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama wa Mikoa na Wilaya za mwaka 2023, Tume imeanza
kutoa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za Maadili ili kuboresha utendaji kazi wa
Kamati hizo.
Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Tume imepanga
kufanya mafunzo katika mikoa sita nchini ambayo ni Mbeya, Songwe, Iringa,
Njombe, Manyara na Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya mkoa huo Dr. Francis Kasabubu akifungua Mafunzo ya siku tatu yanayolenga kuimarisha utendaji kazi wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama yaliyoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa wajumbe wa kamati hizo wa Mikoa ya Mbeya na Songwe pamoja na wilaya zake.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili
ya Maafisa Mahakama mkoani humo Bw. Juma Homera (Katikati) akiwa katika Picha
ya pamoja na Viongozi wengine wakati wa Mafunzo yanayolenga kuimarisha utendaji kazi wa Kamati za Maadili
yaliyoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa Wajumbe wa Kamati hizo wa
Mikoa ya Mbeya na Songwe na wilaya zake . Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dr. Francis Kasabubu na wa pili
kushoto ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Lameck Mlacha, akifuattiwa na Jaji
Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Nidhamu na
Maadili) Bi. Alesia Mbuya.
Sehemu ya Wajumbe wa Kamati za
Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mikoa na Wilaya wakiwa kwenye Mafunzo yanayolenga kuimarisha Utendaji kazi wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama yaliyoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa
wajumbe wa kamati za Mikoa ya Mbeya na Songwe pamoja na wilaya zake.
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Nidhamu na Maadili) Bi. Alesia Mbuya akizungumza wakati wa Mafunzo yanayolenga kuimarisha Utendaji kazi wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama yaliyoandaliwa Tume kwa wajumbe wa kamati hizo wa Mikoa ya Mbeya na Songwe pamoja na wilaya zake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni