Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi hivi karibuni amefanya ziara ya ukaguzi katika Mahakama za Wilaya, Mahakama za Mwanzo na Magereza katika mkoa wa Kagera.
Mhe. Banzi alifanya ukaguzi katika mahakama za wilaya Kyerwa, Karagwe na Missenyi pamoja na mahakama za mwanzo Nkwenda, Mabira, Kayanga, Bugene, Kyaka, Kassambya, Nsunga na kutembelea Gereza la Kitengule.
Akiwa katika Mahakama hizo, Mhe. Banzi alipokea taarifa za utekelezaji wa mashauri na utawalaambapo alipongeza kazi kubwa inazofanywa na watumishi wa Mahakama hizo. Miongoni mwa mambo muhimu aliyosisitiza ni uaminifu, uadilifu, na uwajibikaji.
“Kufanya kazi kwa bidii na uadilifu sio ombi ni sheria, uadilifu ni pamoja na kutunza siri, kuwa na mienendo mizuri kwenye kazi na hata nje ya kazi, pamoja na kujiepusha na vishawishi vya rushwa,” anasema Mhe. Banzi.
Aidha Mhe. Banzi amesisitiza utoaji wa huduma bora na nzuri eneo la kazi, kuendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wadau kwa masuala mbalimbali ya sheria muda wa asubuhi kabla ya kuanza ratiba za Mahakama, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), pamoja na watumishi kuendelea kupewa elimu juu ya Mpango Mkakati wa Mahakama wa Mwaka 2020/2021-2024/2025.
Sambamba na hayo aliwakumbusha watumishi kuendelea kutekeleza maelekezo mbali mbali ya viongozi, likiwemo maelekezo ya utoaji nakala ya hukumu siku hiyo hiyo.
Viongozi wengine waliokuwapo katika ziara hiyo ya ukaguzi ni pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mhe Amworo Odira, Mtendaji wa Mahakama, Bw. Lothan Simkoko, Mahakimu Wafawidhi Mahakama za Wilaya ya Kyerwa, Karagwe na Missenyi, wakiwemo wa Mahakama za Mwanzo za wilaya hizo na watumishi wengine.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mahakama pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kyerwa.
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Nkwenda wilayani Kyerwa Mhe. Dismas Gomano akimpokea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Immaculata Banzi (wa pili kushoto) ni Hakimu Mahakama ya Mwanzo Nkwenda.Mhe. Anajoyce Chrizostom .
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama )
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni