Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Morogoro iliyopo katika Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki
jana tarehe 21 Septemba, 2023 ilifanya kikao cha kusukuma mashauri ya jinai na kuhimiza
upande wa upelelezi kutekeleza wajibu wao kwa kukamilisha upelelezi kwa wakati.
Kikao
hicho kilichoendeshwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Livini
Lyakinana kilibainisha kuwa kuna mashauri 34 katika ngazi ya Mkoa ambayo yamefikisha
siku 100 bila kusikilizwa na Mahakama inasubilia upelelezi na ushahidi ili
iendelee kutekeleza majukumu yake.
Hivyo,
kikao kimeazimia mamlaka zinazohusika kutekeleza majukumu yao kwa wakati kwenye
mashauri hayo, huku upande wa Mahakama ukiahidi kuyasikiliza mfululizo na kufikia
tarehe 20 Novemba, 2023 yawe yameondoshwa na taarifa yake kusomwa katika kikao
kijacho.
Hata
hivyo, Mhe. Lyakinana aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa mashauri 13 kati
ya 22 yaliyojadiliwa katika kikao kilichopita kwa kukaa zaidi ya siku 100
yameshatolewa maamuzi, huku tisa yaliyobaki yakisubiria mamlaka husika zimalize
kazi yao ili Mahakama ifanye kazi yake ya kutenda haki.
Kikao
hicho kilichowashirikisha wajumbe mbalimbali ambao ni wadau wa Mahakama, wakiwemo
Waendesha Mashtaka, Mawakili wa Kujitegemea, TAKUKURU, Wapelelezi toka Jeshi la
Polisi, Afisa uangalizi na maafisa wa Mahakama, kilijadili mambo mbalimbali,
ikiwemo namna ya kupambana na Mawakili bandia, maarufu kama vishoka.
Hoja
hiyo ilifafanuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Kanda ya
Morogoro, Msomi Baraka Lweeka kwa kuiomba Mahakama kufanya uhakiki pale inapopata
mashaka na mtu anayejitambulisha kama Wakili kwa kutumia mifumo iliyopo au kwa
kuwasiliana na uongozi wa TLS Kanda ili kujiridhisha.
Kikao
hicho pia kilijadili namna ya kutoa kipaumbele cha kuwasikiliza kwanza wenye
mashauri yanayowahusu watoto, wazee, wagonjwa, mama wajawazito na walemavu, utoaji
wa nakala za hukumu kwa wakati, huku Mahakama ikipongezwa kufanya vizuri katika
eneo hili, utoaji wa adhabu ya vifungo vya nje na Wapelelezi kutekeleza
majukumu yao kwa wakati ili kesi ziweze kuendelea.
Sehemu nyingine ya wajumbe wakifuatilia wakati kikao kikiendelea, aliyekaa mbele ni Mwenyekiti wa kikao ambaye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mhe. Livini Lyakinana.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni