Ijumaa, 8 Septemba 2023

IJC KINONDONI YAPOKEA KESI ZA UKATILI WA KIJINSIA 121

Na Magreth Kinabo- Mahakama

Kituo cha Utoaji    Haki   Jumuishi (IJC), Kinondoni kilichopo jijini Dar es Salaam katika kipindi cha Januari hadi Agosti 2023 kimepokea kesi 121 za ukatili wa kijinsia.

Akizungumza hivi karibuni wakati akitoa elimu juu vitendo vya ukatili wa kijinsia, Inspekta wa Jeshi la Polisi, Zukra Semolitu amesema umri wa wahanga hao ni miaka 2-18. Amesema kesi hizo zinahusu matukio ya kubaka 53, kulawiti ,32 shambulio la aibu nane, kubaka na kulawiti 20, kumpa mimba mwanafunzi matatu,baba kufanya mapenzi na mwanae  manne.

Inspekta Zukra ameongeza kwamba wahanga wanaofanyiwa vitendo hivyo ni watoto wa kiume na kike, na watuhumiwa wa matukio hayo ni ndugu wa karibu, baadhi ya walimu na baadhi ya viongozi wa dini.

“Mazingira yanayochochea kuwepo kwa vitendo hivi ni ulevi, picha za ngono, umaskini kama vile kulaza watoto na watu wazima kitanda/ chumba kimoja na wazazi kutengana”amesema Zukra.

 Inspekta Zukra amebainisha kwamba ili kuweza kukabiliana na matukio hayo, madawati katika vituo vyote vya polisi yameanzishwa ikiwa ni hatua ya kushughulikia kesi hizo.

Aidha amefafanua kuwa Kituo hicho, kina dawati maalum kwa ajili ya kesi hizo, Polisi Jamii hutembelea mashuleni na sehemu za ibada kutoa elimu, huku akiitaadharisha jamii kuwa ‘Usimuamini mtu kirahisi vunja ukimya’.

Amesema Vyombo vya Ulinzi na Usalama vinatoa wito kwa kila mwananchi kulinda haki ya mtoto kwa kuwa “Mtoto wa mwenzio ni mwanao,”.

Jumla ya wateja 98 waliopatiwa elimu hiyo.

Wakati huohuo, Kituo cha Huduma kwa Mteja kilichopo kwenye jengo hilo, kilitoa elimu juu ya utendaji kazi wa huduma kwa mteja, ambapo wateja 115 walipatiwa elimu hiyo.

Akizungumza wakati akitoa elimu hiyo, mtoa mada, Hakimu Mkazi, Mhe. Denice Mlashani amesema toka kimeanzishwa tarehe 30 Agosti 2023 kimepokea jumla ya mirejesho 2,751. 

mirejesho hiyo ni maoni, mapendekezo, maulizo na malalamiko.  Hivyo Jumla ya mirejesho 2,740 imefanyiwa kazi na wateja kupatiwa mrejesho. 

“Hii ni sawa na asilimia 98.6%, huku malalamiko 11 yanasubiria ufuatiliaji,” amesema Mhe. Mlashani.

 Mhe. Mlashani alimezitaja njia za kuwasilisha maoni, malalamiko na mapendekezo katika kituo hicho ni kwa kupiga simu moja kwa moja kuongea na mtoa huduma. Wateja wanapiga simu kupitia namba 0752 500 400 na namba 0739 502 401. Hivyo wateja wanapiga simu na kuhudumiwa moja kwa moja na watoa huduma. Simu hizo zinakuwa hewani kwa masaa 24 siku saba kwa wiki.

 Njia  nyingine ni kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS), ambapo  mteja anaweza kuwafikia kwa nambari za Kituo ambazo ni 0752 500 400 na 0739 502 401, njia ya barua pepe ambayo ni maoni@judiciary.go.tz na email ya mirathi ya ccamirathi@judiciary.go.tz , ikiwemo tovuti ambayo ni www.judiciary.go.tz na mara baada ya kufungua website hiyo, moja kwa moja kuna boksi la kutoa maoni juu ya huduma za mahakama.

Kituo cha IJC-Kinondoni huwa kinatoa elimu mbalimbali ya masuala yanayohusu sheria kila Jumatano na Alhamisi.

Inspekta wa Jeshi la Polisi, Zukra Semolitu akitoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia.

 Hakimu Mkazi, Mhe. Denice Mlashani akitoa elimu kuhusu Kituo cha Huduma kwa Mteja.



 

Wananchi wakipata elimu.

(Picha na Delfina Mwakyusa)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni