Na. Innocent Kansha – Mahakama.
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ameuhakikishia Ujumbe
kutoka Benki ya Dunia kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kutekeleza shughuli
za mradi huo kwa kasi iliyokusudiwa na kwa ufanisi mkubwa ili kufanikisha
adhima ya kuleta mapinduzi makubwa katika tasnia ya utoaji haki nchini.
Akizungumza
na ujumbe huo uliomtembelea Ofisini kwake ukiongozwa na Mkurugenzi wa Benki ya
Dunia wa Kanda, Bw. Hassan Zamon Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam leo tarehe
07 Septemba, 2023, Prof. Ole Gabriel amesema katika kuhakikisha Mahakama
inajenga mfumo imara wa utoaji haki nchini ni lazima ishirikiane kwa karibu na
wadau wote wanaoshirikiana nao katika shughuli za utoaji haki ili kuimarisha
mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
“Hivi
karibuni Mahakama ya Tanzania imengia makubaliano hayo na wadau wake ili
kuimarisha mfumo wa utoaji haki na kusaidia mifumo kusomana, taasisi hizo ni pamoja na Ofisi
ya Mashitaka ya Taifa, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha
Mashitaka Mkuu wa Serikali, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Wakala wa Ufilisi, Vizazi
na Vifo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa na Wiziara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
hii itasaidia kuwarahishia Majaji na Mahakimu kutekeleza wajibu wao”, amesema
Mtendaji Mkuu.
Prof.
Ole Gabriel amesema muunganiko huo wa kitehama utachangia kuleta mageuzi
makubwa katika tasnia ya utoaji haki nchini. Lakini mafanikio yote hayo muhimu niliyoyataja
kwa Mahakama ya Tanzania yasigeweza kufikiwa kirahisi bila jitihada za Benki ya
Dunia na Serikali ya Tanzania kuiwezesha Mahakama kupiga hatua hiyo kubwa.
“Ukiongelea
Mradi wa Benki ya Dunia kwetu Mahakama unatazama maboresho mbalimbali sio tu
Fedha, Majengo, magari na uondoshaji wa mashauri mahakamani, bali ni matokeo ya kitehama yakieleweka vema kwa jamii yatasaidia kubadili mtazamo wa watu wakiwemo
wafanyabiashara na wawekezaji kwa kuona ni jinsi gani Mahakama inavyowajibika
kwa uwazi katika shughuli zake”, alifafanua Mtendaji Mkuu.
Prof.
Ole Gabriel akauambia ujumbe huo kuwa, katika kuhakikisha Mahakama inajipima
imekuwa ikiitumia Taasisi binafsi ijulikanayo kama REPOA kwa ajili ya kufanya
utafiti ili kujua kiwango cha kuridhika kwa wateja wa ndani na wa nje ili
kupima maboresho yanayoendelea kutekelezwa. Utafiti huo ulifanyika katika awamu
tatu kwa vipindi vya miaka minne minne kuanzia mwaka 2015 kiwango cha kuridhika
kwa wateja kutokana na huduma za Mahakama ilikuwa asilimia 61 ikilinganishwa na
mwaka 2019 kiwango kilipanda kwa asilimia 78 na mwaka 2023 kiwango cha
kuridhika kwa mteja kimepanda maradufu kwa kufikia asilimia 88, tafsiri yake ni
kuwa Mahakama inatoa huduma za uhakika kwa wateja na wadau wake kwa kiwango
kikubwa.
Kwa
upande mwingine, Prof. Ole Gabriel akaelezea mafanikio yanayotokana na
uanzishwaji wa Mifumo ya Mrejesho wa Huduma kwa Mteja ya kielektronik na kituo
cha huduma kwa mteja kwa njia ya kupiga simu, iliyoisaidia Mahakama kuendelea
kupima utendaji wa utoaji huduma kwa kuangalia namna bora ya kuimarisha utoaji
huduma ya haki kwa wananchi. Mifumo hii imechangia kwa kiasi kikubwa kujua wateja
wanakwama wapi na kutatua changamoto kwa haraka, ikiwa ni matokeo ya uboreshaji wa huduma.
Mtendaji
Mkuu akaumbia ujumbe huo kuwa, kupitia mradi wa maboresho wa Banki ya Dunia,
Mahakama imefanikiwa kuanzisha huduma ya Mahakama Inayotembea, kwa sasa huduma
hiyo inatolewa katika majiji mawili ya Mwanza na Dar es Salaam na kufanikiwa
kuwafikia wanufaika wapatao takribani elfu 45 hadi sasa toka kuanzishwa kwake mwaka 2019, na katika mpango wa
awamu ya pili wa maboresho Mahakama imepanga kununua mahakama zinazotembea sita
ili kuendelea kuwafikia watu wengi zaidi na kutanua wigo wa kutoa haki katika
maeneo mengine yenye uhitaji.
“Maboresho
pia yamesaidia kuondosha mlundikano wa mashauri mahakamani kwa kutumia mbinu
mbalimbali ikiwemo kuunda vikosi kazi vya Majaji na Mahakimu kupambana na
mlundikanao takwimu zinaonyesha mwaka 2015 mlundikano wa mashauri mahakamani ulikuwa
asilimia 13 ya mashauri yote yaliyosajiliwa, lakini kufikia mwaka 2023 mwezi
Juni mlundikano umefikia asilimia tatu (3), hii yote ni kutokana na msaada
mkubwa tunaowezeshwa na mradi wa Banki ya Dunia wa kujengea watu wetu uwezo wa
kutumia rasilimali tulizonazo”, aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Mtendaji
Mkuu huyo, akazungumzia matarajio ya Mahakama katika kuendelea kuboresha huduma
za hutoaji haki kwa kufafanua mambo kadhaa ikiwemo; matumiazi ya mfumo wa Akili
Bandia utakao rahisisha uendeshaji wa mashauri, kupanua wigo wa mfumo wa TEHAMA
ili uweze kutumika katika Mahakama za Mwanzo nchini, kwani takwimu zinaonyesha
asilimia 70 ya mashauri yapo katika Mahakama hizo.
Pia
kuboresha zaidi mfumo wa kusimamia mashauri “Advance Case Management” ili
kuongeza ufanisi na umakini katika kufanya mambo kwa usahihi na kutunza takwimu
za mashauri, kuongeza miundombinu ya kisasa ya kufanyia kazi hii itaongeza kujiamini
kwa watumishi wanapotekeleza majukumu yao na kuongeza ubunifu wa kufikiri na
kuboresha usawa wa kijinsia na mambo mengine.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa Benki ya Dunia wa Kanda, Bw. Hassan Zamon akaushuru Uongozi wa Mahakama kwa
kuendelea kushirikiana na Banki ya Duania katika safari ya kutekeleza mambo
makubwa yenye mafanikio kwa wananchi yanayolenga kuboresha mifumo ya utoaji
haki nchini kupitia mradi wa Banki ya Dunia. Ni jambo la kuvutia kuona mambo
yote hayo yaliyotajwa yametokana na jitihada za mradi huo ni jambo la kuvutia.
“Kwa
mtazamo wangu mimi mwenye uelewa ndogo kuhusu shughuli nyingi za mifumo ya
kimahakama katika sehemu nyingi za dunia hasa kwa nchi zenye kipato sawa na
Tanzania ambapo watu wanadanganywa ama kudhurumiwa na mifumo ya kimahakama na
huo ndiyo ukweli katika nchi nyingi”,
Mkurugenzi
Hassan akaipongeza Mahakama kwa kuanzisha mifumo imara ya kusaidia kutoa huduma
ya haki kwa uwazi kama mfumo wa huduma ya mrejesho kwa mteja na kuboresha mfumo
wa kusimamia mashauri na hivyo kuleta mageuzi na kuonesha utofauti mkubwa sana katika mfumo wa
utoaji haki nadhani hayo ni maendeleo makubwa.
“Ninapotazama
kwa ujumla Tanzania ipo katika safari ya ukuaji wa uchumi ukalinganisha na nchi
zingine, nafasi ya Mahakama katika kuboresha mifumo yake kama mfumo wa
kusimamia mashauri na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala na kupunguza hatua
za usikilizaji wa mashauri kwa uboreshaji huo utasaidia kuvutia wawekezaji na
kukuza uchumi, mifumo kama hiyo itasaidia kuwalinda wawekezaji katika sekta
mbalimbali ndani ya nchi”. Aliongeza Mkurugenzi huyo.
Mkurugenzi
Hassan amesema kwa sasa maboresho ya mifumo hiyo ya utoaji haki itaonekana inawasaidia
wananchi pekee la hasha bali inaongeza uamininifu si kwa wananchi pekee inakuza
jedwali la nchi na kuvutia wawekezaji wa nje wakiamini Tanzania ni sehemu
salama ya kuwekeza. Kwa jinsi mifumo ya kimahakama itavyoendelea kuboreshwa ni
njia sahihi ya kuendelea kuonyesha ni sehemu salama kwa wawekezaji wengi zaidi
na sit u kwa wawekezaji wa nje hata wandani watatamani kuwekeza zaidi.
“Utawala wa sheria ni kipengele cha msingi katika kukua kwa uchumi wa Taifa lolote na kuleta maendeleo ya kweli na penda nichukue nafasi hii kuipongeza Mahakama kwa maboresho makubwa na ahidi kuendelea kushirikiana nanyi na kutia nguvu katika maeneo yote unayoendelea kufanya maboresho ya kweli”, alisisitiza Mkurugenzi Hassan
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akifafanua mambo mbalimbali yanayohusu shughuli zinazofanyika za maboresho ya Mahakama ya Tanzania wakati alipotembelewa na Ujumbe wa Banki ya Dunia Ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es salaam leo tarehe 07 Septemba, 2023.
Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa Kanda, Bw. Hassan Zamon akielezea kufurahishwa kwake na jitihada kubwa zilizofikiwa na Mahakama ya Tanzania katika kuboresha mfumo wa haki nchini kupitia uwezeshaji wa mradi wa Banki ya Dunia.
Mtaalum Kiongozi wa Utawala kutoka Banki ya Dunia kutoka Tanzania, Bw. Benjamin Mtesigwa (kulia) akifafanua jambo wakati wa ziara hiyo, kushoto ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Jaji Mteule wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt akifuatilia.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (wa tatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe kutoka Banki ya Dunia, uliofika Ofisini kwake kufanya mazungumzo, wengine ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa Kanda, Bw. Hassan Zamon (wa tatu kushoto), Mtaalum Kiongozi wa Utawala kutoka Banki ya Dunia, Bi. Donna Andrew (wa pili kulia), Mtaalum Kiongozi wa Utawala kutoka Banki ya Dunia kutoka Tanzania, Bw. Benjamin Mtesigwa (wa kwanza kulia), Msaidizi wa Programu kutoka Banki ya Dunia, Bi. Catherine Mutagwa (wa pili kushoto) na Msaidizi wa Programu kutoka Banki ya Dunia, Bi. MaryIrene Singili (wa kwanza kushoto).
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa Kanda, Bw. Hassan Zamon (wa tatu kushoto), wakiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wengine kutoka Banki ya Dunia, uliofika kutembelea Mahakama Inayotembea kujionea shughuli zinazofanywa na Mahakama hiyo Temeke jijini Dar es salaam.
Afisa Ustawi wa Jamii Bi. Happiness Nyange (kulia) anayetoa huduma ndani ya Mahakama Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, akielezea namna anavyotoa huduma kwa watoto wenye uhitaji alipotembelewa na Ujumbe kutoka Banki ya Dunia.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliyeshika matoi ya kuchezea watoto akielezea namna yanavyosaidia kuratibu shughuli za watoto wanaofikishwa Ofisini hapo, kulia ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia wa Kanda, Bw. Hassan Zamon akimsikiliza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni