Na. Hilary Lorry – Mahakama Lindi
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Mtwara, Mhe.Rose Ebrahim hivi
karibuni amefanya ziara ya kikazi katika gereza la Wilaya ya Lindi.
Akizungumza na mahabusu na wafungwa katika gereza hilo
Wilaya ya Lindi Mhe. Ebrahim
aliwataka wafungwa na mahabusu watakapo toka gerezani hapo kuwa mabalozi wazuri
wakupinga vitendo viovu pindi watakaporudi uraiani. Vilevile aliwaasa vijana
kutumia muda wao mwingi vizuri katika kujikita katika shughuli za kuichumi na
siyo kutenda mambo maovu.
“Nasikitika sana kusema Kanda hii ya Mtwara imekuwa na
kasumba ya matukio mengi ya ukatili wa kijinsia hasa matukio ya ubakaji hii
inafanya taifa kupoteza nguvu kazi, hivyo nawaomba kama Mama na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda
hii mtakapo toka hapa gerezani mkawe mabalozi wazuri wakupinga matendo maovu”,
aliongeza Jaji Ebrahim.
Mhe. Ebrahim
aliendelea kwa kutoa pongezi kwa Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Lindi pamoja na
watumishi wenzake kwa juhudi kubwa za kuwahudumia wateja wao ambao ni wafungwa
na mahabusu katika gereza hilo. vilevile aliwapongeza kwa jitihada wanazofanya katika kuhakikisha
gereza la Wilaya ya Lindi linakaa katika
hali ya usafi muda wote.
Jaji Ebrahim aliwataka
Mahakimu wa ngazi zote kuendelea kusaidiana kwa karibu na timu ya haki jinai
kuendesha mashauri kwa haraka ili kuepusha mashauri ya mlundikano (backlog
cases). Aidha aliwapongeza Mahakimu wa Mkoa wa Lindi kwa kutozalisha mashauri
ya mlundikano na kwa jitihada za kutoa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri
kwa wakati.
“Nafahamu Mkoa wa Lindi hauna mashauri mengi ya muda
mrefu, naomba jitihada zilizopo ziboreshwe ili tusizalisha mashauri ya muda
mrefu (backlog cases) ikiwa ni pamoja na kutoa nakala za hukumu na mienendo ya
mashauri kwa wakati. Aidha natambua mpango tuliojiwekee kama Kanda na Mkoa wa
Lindi wakutoa nakala za hukumu na mwenendo mara tu shauri linapofika tamati
naomba mpango huu uendelee kutiliwa mkazo ili tusije kuwakwamisha hawa ndugu
zetu wakati wa kukata rufaa” alisema Jaji Ebrahim.
Aidha, wakizungumza kwa nyakati tofauti Mkuu wa Gereza
la wilaya ya Lindi ASP.Dominic Byamungu,
wafungwa na mahabusu wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa
waliyoipiga katika masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHEMA)
yaani Mahakama Mtandao (video conference) kwakurahisha zoezi la usikilizaji wa
mashauri kwa wakati.
“Awali ilikuwa lazima mahabusu, mfungwa au hata shahidi
kufika katika mahakamani lakini kutokana na Mahakama kuboresha mifumo ya TEHAMA
sasa tunaweza tukawa na mahabusu na wafungwa
mwenye mashauri ya rufaa Mahakama
Kuu, Mahakama ya Rufani au Mahakama yoyote hapa nchini na wakasikilizwa wakiwa gerezani…,
…hii imepunguza suala la mashauri kuchukua muda mrefu
bila kusikilizwa na imepunguza gharama kwa Serikali na Magereza, imerahisisha
upatikanaji wa haki kwa wakati na pia imeongezea serikali kipato kwa kulinda
nguvu kazi kusafiri umbali mrefu”, alisema Mkuu wa gereza hilo.
Katika ziara hiyo
Jaji Mfawidhi Kanda ya Mtwara aliongozana na Mahakimu, Viongozi waandamizi wa Mahakama kwa
kanda ya Mtwara na Lindi pamoja na timu
ya haki jinai kwa Mkoa wa Lindi.
Ziara ya Jaji Ebrahim ni mwendelezo wa ziara yake katika Kanda ya Mtwara na Mkoa
wa Lindi, Ziara yake katika Gereza la Wilaya ya Lindi imelenga zaidi kusikiliza
na kuangali namna bora ya kutatua changamoto zinazo wakabili wafungwa na
Mahabusu katika gereza hilo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe.Rose Ebrahim (mwenye skafu) akiwa kwenye picha ya pamoja na Maafisa waandamizi wa Gereza Kuu la Wilaya ya Lindi alipofanya ziara ya ukaguzi hivi karibuni.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe.Rose Ebrahim (mwenye skafu kulia) akibadilishana mawazo na mwenyeji wake Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Lindi ASP. Dominic Byamungu alipowasili gerezani hapo.
(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni