Na. Faustine Kapama-Mahakama
Timu
ya Wataalam na Baraza la Sheria nchini wanakutana jijini Dar es Salaam kwa siku
mbili kuanzia leo tarehe 18 Septemba, 2023 kupitia rasimu ya mtaala wa Shule ya
Sheria kwa Vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) kwa lengo la kupata mtaala
mpya.
Akizungumza
wakati anafungua mkutano huo unaofanyika katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya
Familia Temeke, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed
Siyani amesema ili taasisi yoyote iweze kupiga hatua ni lazima ifanye
maboresho.
“Kuhuisha
mtaala wa Shule ya Sheria ni moja kati ya maboresho makubwa ambayo inapaswa
kuyafanya ili kuendana na zama tulizonazo. Ninaamini kwamba mtaala ambao
umeandaliwa ili kukidhi mahitaji ya sasa utakuwa ni mapinduzi katika uboreshaji
wa elimu ya sheria katika nchi yetu,” amesema.
Jaji
Kiongozi, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Sheria, amewaomba wajumbe wa mkutano
huo kushiriki
kikamilifu katika kubadilishana maarifa na mawazo na kuongeza au kuboresha
mtaala unaopendekezwa, lengo pekee likiwa kuwa na mchakato wa uthibitishaji wa
kujenga na wenye tija.
Amesema
Shule ya Sheria kwa Vitendo Tanzania ilianzishwa kupitia Sheria ya Shule ya
Sheria Tanzania No.18 ya mwaka 2007 na ilianza kutoa Stashahada ya Juu ya
Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo mwaka uliofuata na sasa ni zaidi ya miaka kumi
ambayo imepita bila kuwa na mapitio ya kina ya mtaala wake.
Mhe.
Siyani ameeleza kuwa mtaala uliopo haukidhi mazingira ya sasa ya kijamii na
kiuchumi katika mazoezi ya kisheria ambayo yanaashiria mabadiliko makubwa hivi
karibuni katika teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Shule
ya Sheria Tanzania na Mahakama ya Tanzania walidhamiria kwa pamoja kuongoza
mageuzi yanayohitajika ili kupunguza pengo na pia kuhakikisha utoaji wa huduma
bora za kisheria ambazo ni miongoni mwa malengo makuu ya Mahakama katika
kufikia utoaji wa haki kwa wakati,” amesema.
Jaji
Kiongozi amesema anafahamu mchakato wa mapitio umepitia hatua mbalimbali
kuanzia zoezi la kuwashirikisha wadau na tathmini ya mahitaji ya utekelezaji wa
mtaala uliopo, mapitio ya kina ya mtaala wa Shule ya Sheria Tanzania na baadaye
uthibitishaji wa rasimu ya mtaala kwa wadau wa ndani na wa nje.
“Nachukua
fursa hii kuwapongeza wale wote ambao wamejitolea muda wao na juhudi zao bila
kuchoka katika kufanikisha kazi hii muhimu. Ninaamini kutokana na yale
niliyoyapata kutoka kwenye rasimu hii, mtaala unatarajiwa kutimiza matarajio ya
muda mrefu na yanayosubiriwa na jumuiya ya wataalamu wa sheria kwa ujumla,” amesema.
Awali,
akimkaribisha Jaji Kiongozi kufungua mkutano huo, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sheria
kwa Vitendo Tanzania, Prof. Sisti Mramba alielezea mchakato mzima waliopitia
katika kufikia hatua hiyo muhimu ambayo imehusisha ushirikishwaji wa wadau
mbalimbali.
“Tulianza
na mikutano ya kina ya mashauriano ambayo ilileta pamoja sauti na mitazamo ya
watendaji, wasomi, wahitimu, wanafunzi na wanajamii. Ufahamu wao muhimu umekuwa
na manufaa katika kutengeneza mtaala wetu,” amesema.
Prof.
Mramba amesema pia kuwa rasimu hiyo ilipitiwa kwa kina na wafanyikazi wa ndani ambao
utaalam wao na kujitolea kwao kumeonekana katika mchakato wote kwani walifanya kazi
bila kuchoka ili kuhakikisha kwamba mtaala unalingana na dhamira na maono ya taasisi
yao.
Kaimu
Mkuu wa Chuo amesema kulikuwepo pia na mchango uliopokelewa kutoka kwa wadau wa
nje ya taasisi ambapo mtazamo unaotokana na uzoefu na utaalamu wao mbalimbali
umewapatia uelewa mpana zaidi. Amesema wanathamini wakati na maarifa waliyoyatoa,
ambayo yameboresha mchakato wa kutengeneza mtaala huo.
“Hatulengi
tu kufikia viwango lakini pia kuweka vigezo vipya vya ubora katika mafunzo.
Mtaala tunaowasilisha unawakilisha maono yetu ya pamoja ya siku zijazo, ambapo
wanafunzi wetu watapokea elimu iliyokamilika inayowapa ujuzi na maarifa muhimu
ili kustawi katika ulimwengu unaoendelea kubadilika,” amesema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni