Jumatatu, 18 Septemba 2023

HAKIMU MKAZI KIBAHA ATOA RAI KWA WANANCHI KUKATA RUFAA KWA WAKATI

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Pwani

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha-Pwani, Mhe. Felister Ng’hwelo ametoa rai kwa wananchi kukata rufaa kwa wakati dhidi ya maamuzi ya Mahakama yaliyotolewa dhidi yao endapo mtu hajaridhishwa ili kuepuka gharama zisizo na ulazima.

Wito huo umetolewa leo tarehe 18 Septemba, 2023 na Hakimu huyo alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi/wateja waliofika kupata huduma mahakamani hapo ambapo amesema japo Sheria inaruhusu mtu kuleta maombi ya kukata rufaa nje ya muda lakini kuchelewa kunaweza kugharimu muda na pesa lakini vilevile maombi hayo yanaweza kukubalika au kukataliwa.

“Nawasihi kuzingatia muda wa kukata rufaa maana unatamkwa na Mahakama, kwa hiyo, kama upande ambao haujaridhishwa na uamuzi ni vyema ukakata rufaa kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye hukumu husika,” amesisitiza Mhe. Ng’hwelo. 

Mhe. Ng’hwelo amebainisha kuwa, muda wa kukata rufaa ni siku thelathini (30)  kuanzia tarehe iliyosomwa hukumu hivyo, muda huo unatosha kukata rufaa badala ya kusubiri muda kuisha na kuanza kuomba kukata rufaa nje ya muda.

Akiendelea na utoaji elimu, Mhe. Ng’hwelo amegusia pia suala la kukata rufaa kwa pande zote mbili kama hawakuridhika na maamuzi yaliyotolewa ambapo amesema “kama pande zote mbili hazijaridhika na maamuzi ya Mahakama ya Mwanzo kila mtu kwa muda wake anaweza kukata rufaa Mahakama ya Wilaya maana sheria inaruhusu,” ameeleza.

Ameongeza kwamba, kila mtu ana sababu zake za kutokuridhika na maamuzi hata kama yametolewa upande wake.

Aidha, Mhe. Ng’hwelo amewataka wananchi kuhudhuria kila Jumatatu mahakamani hapo ili kupata elimu lakini pia kufika mahakamani wakati wote na kuuliza maswali yanayowatatiza ili kupata msaada.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha-Pwani, Mhe. Felister Ng’hwelo (kushoto) akitoa elimu kwa wananchi waliohudhuria Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha Pwani leo tarehe 18 Septemba, 2023 (hawapo katika picha). Kulia ni Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Wilaya Kibaha, Bw. Rashid Bazolo.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mahakamani hapo wakimsikiliza  Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha-Pwani, Mhe. Felister Ng’hwelo (hayupo katika picha).

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni